Kilichotokea dakika 90, Mnyupe alivyoimaliza Dar Derby

ILE Dar es Salaam Derby kati ya Azam dhidi ya Yanga, imelizika kinyonge sana kwa timu hizo zikitoka bila kupatikana mshindi huku changamoto za waaamuzi zikiendelea kushika nafasi kwenye michezo hiyo mikubwa nchini.

Mchezo huo uliopigwa Jumapili Machi 15, 2026 pale Benjamin Mkapa jijini Dar, umezifanya timu hizo ndani ya dakika 90 kushindwa kuonyesha mambo makubwa kwenye hatua ya umaliziaji wa nafasi.

Kumbuka msimu huu timu hizo mbili mechi hii ndiyo zililkutana kwa mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu Bara lakini nje ya hapo zilitangulia kukutana katika Fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 kule Pemba na kumaliza dakika 120 bila kufungana, kisha Yanga kwenda kushinda kwa penalti 5-4 na kuchukua taji hilo.

Azam ambao ndio walikuwa wenyeji, walikuwa bora sana kipindi cha kwanza, mpango wao wa mchezo uliwabana vizuri wageni ambapo sio rahisi kuifanya Yanga isifanye shambulizi lolote la maana katika dakika 26 za kwanza ikikosa kuonyesha mpango wowote wa kutengeneza nafasi.

Matajiri hao wa Chamazi, walikuwa bora karibu kila eneo na kama wangekuwa makini walitakiwa kumaliza kipindi hicho kuwa mbele lakini haikuwa hivyo, huku Yanga tena ikibebwa na ubora wa kipa wake Djigui Diarra ambaye alikuwa makini kuzima hata makosa yaliyofanywa na baadhi ya mabeki wake.

Timu zote hazikuonyesha kiwango kikubwa sana ndani ya dakika 90, ilikuwa kama zimeamua kutunziana heshima kwani Azam ambayo haikuanza na washambuliaji wake halisi, ilikuwa na nguvu sana katikati ya uwanja lakini kule mbele haikuwa na makali ambapo hata Yanga ilipofanya makosa bado walikuja kuyasahihisha wenyewe.

Yanga nao hawakuwa bora kuanzia katikati ya uwanja kwenda mbele, eneo lao la kiungo halikuwa na ubunifu zaidi ya viungo wake kuwa na majukumu mengi ya kukaba kuliko kutengeneza nafasi hatua ambayo iliwapa wakati mgumu washambuliaji wake Prince Dube na Laurindo Aurelio ‘Depu’ kuonekana katika kumalizia nafasi.

Azam wachezaji wao wengi walicheza vizuri lakini aliyefanya vizuri zaidi alikuwa kiungo wake Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye alisukuma mashambulizi na kutawanya mipira alivyotaka na mara mbili alikaribia kuifunga timu yake ya zamani kwa kosa la Bakari Mwamnyeto mwanzoni mwa kipindi cha kwanza lakini pia dakika 56 akamchungulia vizuri Diarra aliyetoka ila hesabu zikapungua kidogo.

Yanga wao wataendelea kufurahia kazi ya kipa wao Diarra ambaye kwa mara nyingine tena alikuwa kizuizi kwa wapinzani kufunga mabao, akisahihisha makosa ya wenzake ambayo yangeweza kuwapa ushindi wenyeji.

Kuonyesha Yanga haikuwa bora kwenye mchezo huo ilimaliza dakika 90 ikiwa imepiga shuti moja lililolenga lango kupitia kichwa cha Depu dakika ya 83, takwimu ambazo hazijazoeleka kwa mabingwa hao kuwa na kiwango cha namna hiyo katika mechi kubwa kama hiyo.

IBENGE FRESH, PEDRO KAZI ANAYO

Kocha wa Azam Florent Ibenge ametoka salama kwenye dabi ya pili nchini kwenye ligi akiwafunga Simba 2-0 lakini akailazimisha 0-0 na Yanga huku kikosi chake kikicheza vizuri, Mkongomani huyo alionekana kufanya hesabu zake sawasawa katika kumkabili bingwa mtetezi.

Pedro Goncalves wa Yanga ana kazi nzito ambapo bado mashabiki wanataka kuona timu yao ikiendelea kutawala kwenye mechi kubwa hatua ambayo sasa inakosekana. Mchezo dhidi ya Simba na huu wa juzi zote Yanga ilionekana kuwa chini mambo ambayo hayajazoeleka.

AZAM, YANGA ZIMEGOMA KUFUNGIKA

Matokeo hayo ni kama yamezitunzia heshima timu zote kwani zimeendelea kuwa timu ambazo hazijapoteza mchezo wowote msimu huu, Yanga ikiendelea kuwa juu ya msimamo ikiwa na pointi 36 wakati Azam ikibaki nafasi ya pili na pointi 28.

Mwamuzi wa mchezo huo alikuwa Ally Mnyupe kutoka Morogoro akisaidiwa na Mohammed Mkonowa Tanga na Janeth Balama kutoka Iringa, lakini kuna maamuzi makubwa walishindwa kuyapa tafsiri vizuri za sheria na kuharibu ladha ya mchezo huo.

Mnyupe ataingia lawamani kwa kushindwa kuamua tukio la wazi la kuangushwa eneo la hatari kwa mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube kwenye mchezo huo na beki wa Azam, Fuentes Mendoza akiona kwamba haikustahili kuwa penalti.

Tukio lingine ni beki Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ alikuwa na matukio mengi ambayo kama mwamuzi angefuata sheria zake sawasawa asingemaliza mchezo huo huku pia akishindwa kuongeza muda sawasawa baada ya kumalizika dakika 90 akiongeza mbili pekee licha ya kuwa na matukio mengi ya kupoteza muda.

Mkono naye mwanzoni tu wa kipindi cha kwanza aliamua tukio la Depu akidai aliotea wakati alikuwa eneo sahihi kabisa sambamba na matukio mengine ya kushindwa kuona sawasawa mtu wa mwisho kutoa mpira.