KITILA AWASHUKURU VIONGOZI WA DINI UBUNGO

Mbunge wa Jimbo la Ubungo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais–Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo akimzungumza wakati wa hafla ya Iftar iliyoandaliwa na Ofisi ya Mbunge kwa kushirikiana na Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC)

******

Na Mwandishi Wetu.

Mbunge wa Jimbo la Ubungo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais–Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amewashukuru viongozi wa dini wilayani humo kwa mchango wao uliomsaidia kupata ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Prof. Kitila alitoa shukrani hizo jana Jumapili, Machi 15, 2026, wakati wa hafla ya Iftar iliyoandaliwa na Ofisi ya Mbunge kwa kushirikiana na Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC), iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kituo hicho wilayani Ubungo, Dar es Salaam.

Akizungumza mbele ya mamia ya waumini na wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Prof. Kitila aliwashukuru Masheikh wa Ubungo kwa uamuzi wao wa kumuunga mkono hadharani katika chaguzi zilizopita.

Mbunge wa Jimbo la Ubungo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais–Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo akimzungumza wakati wa hafla ya Iftar iliyoandaliwa na Ofisi ya Mbunge kwa kushirikiana na Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC).

Alisema msaada na mshikamano ulioonyeshwa na viongozi wa dini ulikuwa na mchango mkubwa katika ushindi wake, huku akiahidi kuendelea kushirikiana nao katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Katika hafla hiyo, Prof. Kitila alimtaja Mkurugenzi Mkuu wa EACLC, Catherine Wang, kuwa mshirika muhimu wa maendeleo na kuwahimiza wananchi kukisemea vizuri kituo hicho ili wanufaike na fursa za biashara zilizopo.

Kwa upande wake, Catherine Wang alisema EACLC si mradi wa majengo pekee bali ni jukwaa la kitaalamu linalolenga kuimarisha mahusiano mema kati ya kituo hicho na jamii inayokizunguka.

Mkurugenzi Mkuu wa EACLC, Catherine Wang.

Naye Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Maulid Salim Kidebe, alimshukuru Prof. Kitila kwa kuandaa Iftar hiyo akisema mbunge huyo ana sifa ya kuwajali wananchi wake wakati wote na kwamba viongozi wa dini wataendelea kumuunga mkono hata katika siku zijazo.

Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Maulid Salim Kidebe.