Malindi hali mbaya Ligi Kuu Zanzibar

TIMU ya Malindi FC inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar, imepoteza matumaini baada ya kutoka kuwania ubingwa wa ligi hiyo hadi kupambana isishuke daraja.

Sababu mojawapo inayotajwa kuiangusha timu hiyo ni mabadiliko ya mara kwa mara ya uongozi uliosababishwa na wengine kujiuzulu huku baadhi ya wachezaji muhimu nao kuondoka katikati ya msimu.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa timu hiyo, Mohammed El Jabir, alijiuzulu nafasi hiyo bila ya kutoa sababu ya kufanya hivyo.

Awali, timu hiyo ilisitisha mkataba wa ajira wa Ofisa Habari na Mawasiliano, Namala Suleiman na Mpiga picha wake, Maulid Salum.

Kabla ya kutokea hayo, timu hiyo ilipata mwekezaji mpya aliyedumu kwa robo msimu huku ikidaiwa kujiondoa kwenye timu hiyo na kusababisha hali kutokuwa nzuri hadi sasa.

Chanzo kutoka ndani ya timu hiyo, kimeliambia Mwanaspoti kuwa, wawekezaji hao walitoa taarifa kwa watu ambao waliwahitaji kufanya nao kazi kuwa wanaondoka.

“Wawekezaji walioniomba nifanye nao kazi wameondoka, wameiacha timu ndio wakanipa taarifa, tukaaagana rasmi,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kimesema kuwa, baada ya kuondoka wawekezaji hao, hali ya timu hiyo ilianza kupoteza matumaini hali iliyofanya wachezaji waliosajiliwa kutoka nje ya Zanzibar kuondoka.

Mwandishi wa gazeti hili alifanya juhudi ya kumtafuta Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hababuu Ali ili kufahamu mikakati na mipango ya kuinusuru timu kushuka daraja ambapo alisema kwasasa hawezi kuwa na mipango hiyo hadi timu itakapokaa sawa kwani haijulikani ipo chini ya nani.

“Walioichukua timu wameiacha na Mwenyekiti wa timu (Mohamed) kajiuzulu, kwa maana hiyo haieleweki ipo chini ya nani,” alisema Hababuu huku akibainisha kwamba, endapo timu hiyo itakuwa sawa yupo tayari kuitumikia kwa kila hali.

Kabla ya jahazi hilo kuingia maji na kuanza kuzama, ilielezwa timu hiyo ilifanya mabadiliko msimu wa 2025-2026 ikiweka malengo ya kuuza wachezaji kimataifa na kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar.

“Malindi ina hamu kubwa ya kuchukua ubingwa wa ZPL na ndio maana inafanya juhudi mbalimbali kuhakikisha hilo linatimia, ikiwa haijafanikiwa Ligi Kuu, tutajipanga kuchukua Kombe la Shirikisho (FA cup),” alisema mmoja wa viongozi wa timu hiyo mwanzoni mwa msimu.

Malindi ambayo baada ya mechi sita za kwanza ilikuwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar ikikusanya alama 14 huku ikitajwa kuwa miongoni mwa timu zinazoweza kuwania ubingwa, mambo yamebadilika na sasa imeporomoka hadi nafasi ya 13 katika mstari wa kushuka daraja ikiwa na alama 24 baada ya kucheza mechi 20. Imefunga mabao 19 na kuruhusu 22, huku ikibakiwa na mechi kumi kuhitimisha msimu huu.