Mkuranga. Wadau mbalimbali wakiwemo wananchi, taasisi wezeshi na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga wamekutana kujadili mpango kabambe wa maendeleo wa wilaya hiyo wa miaka 20 kuanzia mwaka 2026 hadi 2046, wakisisitiza umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wake, ili kuendana na kasi ya ukuaji wa eneo hilo.
Kikao hicho cha wadau kimefanyika leo Jumatatu, Machi 16, 2026, mjini Mkuranga, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Ally.
Baadhi ya wananchi walioshiriki katika mjadala huo, akiwemo Mohamed Kisuguru, Rabia Mohamed na Shukuru Ngwaishani, wamesema wameupokea mpango huo kwa ari kubwa na kuwataka wataalamu kuhakikisha unatekelezwa haraka bila vikwazo, ili kuleta maendeleo ya haraka kwa wakazi wa eneo hilo.
Mpango huo umeandaliwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambapo mmoja wa wataalamu hao, Dk Nestory Yamungu, amesema upembuzi uliofanywa umebaini kuwa Wilaya ya Mkuranga ina eneo kubwa na inakua kwa kasi, hivyo kuna haja ya kuigawa na kuunda manispaa tatu za kiutawala, ili kurahisisha usimamizi wa maendeleo.
Amesema ili kufanikisha hilo, mpango huo unapendekeza kuwepo kwa vitovu vitatu vya miji vitakavyoongoza maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo tofauti ya wilaya hiyo.
Hata hivyo, Dk Yamungu amesema changamoto kubwa waliyoibaini ni mwingiliano wa matumizi ya ardhi katika baadhi ya maeneo, jambo linalohitaji kufanyiwa kazi kupitia mipango madhubuti ya upangaji ardhi.
“Uchambuzi wetu unaonesha kuwa eneo la Mkuranga linakua kwa kasi na lina uwezo wa kuhudumia wakazi wengi zaidi, ambapo tunatarajia ifikapo miaka ijayo idadi ya watu inaweza kufikia zaidi ya milioni nne,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Ally, amesema mpango huo ni muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya wilaya hiyo, akisisitiza umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wake kupitia mifumo mbalimbali, ikiwemo ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP).
“Wilaya ya Mkuranga ina wakazi zaidi ya milioni moja na idadi hiyo inaendelea kuongezeka kila mwaka, hivyo ni muhimu mpango huu utekelezwe kwa wakati ili kuongoza maendeleo kwa mpangilio mzuri,” amesema.
Ameongeza kuwa ni vema mpango huo uwasilishwe haraka katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, ili ujadiliwe na kupitishwa katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC).
Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Waziri Kombo, amesema mpango huo utakuwa chachu ya maendeleo endelevu kwa wananchi na kuleta mwelekeo mpya wa upangaji na matumizi bora ya ardhi.
Amesema hivi sasa halmashauri hiyo inakadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya laki saba, na idadi hiyo inaendelea kuongezeka siku hadi siku, huku akisisitiza kuwa mafanikio ya mpango huo yatategemea ushirikiano wa karibu kati ya wananchi, serikali na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa.
Kihistoria, Wilaya ya Mkuranga ni moja ya wilaya za Mkoa wa Pwani ambazo zimekuwa zikikua kwa kasi kutokana na ukaribu wake na Jiji la Dar es Salaam. Halmashauri yake ilianzishwa mwaka 1995 baada ya mgawanyo wa kiutawala, ikiwa na jukumu la kusimamia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wake.
Katika miaka ya hivi karibuni, halmashauri hiyo imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara, huduma za afya, elimu pamoja na mipango ya upangaji ardhi ili kuendana na ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi.
Kutokana na ukuaji huo, wadau wanaamini kuwa mpango kabambe wa maendeleo wa miaka 20 utasaidia kuongoza ukuaji wa miji, kuboresha matumizi ya ardhi na kuifanya Mkuranga kuwa moja ya maeneo muhimu ya maendeleo katika ukanda wa Pwani.
