Mkurugenzi huduma za wakunga ataja mikakati ya kuokoa maisha ya wajawazito

Dar es Salaam. Wakati dunia ikiendelea kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani Machi 8 ya kila mwaka, mjadala kuhusu haki, afya na ustawi wa wanawake unapewa uzito katika sekta mbalimbali, ikiwamo ya afya ya uzazi.

Kwa Tanzania, moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele katika kulinda maisha ya wanawake ni kupunguza vifo vinavyotokana na ujauzito na uzazi. Lengo hilo linatajwa kuwa sehemu muhimu ya jitihada za kuboresha ustawi wa mama na mtoto pamoja na kuimarisha mfumo wa huduma za afya nchini.

Hospitali ya Taifa Muhimbili imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuboresha huduma za afya ya uzazi na kuhakikisha wanawake wanapata huduma salama wakati wa ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga wa hospitali hiyo, Redemta Matindi anasema hospitali hiyo ina jukumu la kuhakikisha kila mama anapata huduma salama kupitia mfumo wa kitaifa wa afya unaohusisha vituo vya ngazi zote.

Anasema hospitali hiyo si tu kituo cha juu cha rufaa, bali pia ni kitovu cha utaalamu na ushauri wa kitaalamu kwa vituo vingine vya afya nchini.

“Hospitali ya Taifa, tuna jukumu la kuhakikisha kila mama anapata huduma bora popote alipo. Kuna taratibu mbalimbali ambazo zimewekwa ili kuhakikisha tunafikia lengo la kupunguza vifo vya wajawazito,” anasema.

Matindi anasema moja ya hatua muhimu inayotekelezwa ni kufanya mapitio ya kina ya kila tukio la kifo cha mama mjamzito kinapotokea.

 Lengo la utaratibu huo ni kubaini sababu za kifo hicho na kujifunza namna ya kuzuia tukio kama hilo lisijirudie.

Anasema tathmini hiyo hufanywa kwa umakini mkubwa ili kubaini iwapo kulikuwa na changamoto katika utoaji wa huduma, ucheleweshaji katika mfumo wa rufaa au sababu nyingine zilizochangia tukio hilo.

“Tunafanya tathmini ya kila tukio la kifo cha mama ili kujifunza. Tunaangalia wapi kulikuwa na changamoto, nini kingeweza kufanyika tofauti na namna ya kuboresha huduma,” anasema.

Matindi anabainisha kuwa, utaratibu huo hauishii katika Hospitali ya Taifa Muhimbili pekee, bali unatekelezwa katika ngazi zote za mfumo wa afya, kuanzia hospitali za rufaa za mikoa na wilaya hadi vituo vya afya na zahanati.

Kwa kufanya tathmini hizo katika kila ngazi ya huduma za afya, wataalamu wanaweza kubaini upungufu uliopo na kuweka mikakati ya kuyatatua ili kuzuia vifo vinavyoweza kuepukika.

Maboresho katika huduma za uzazi

Matindi anasema juhudi hizo pia zimechangiwa na maboresho makubwa yaliyofanyika katika vituo vya afya vya ngazi za chini, jambo linalosaidia mama kupata huduma mapema kabla ya kufikia hospitali za rufaa.

Anaeleza kuwa maboresho hayo yanatokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya afya, hasa katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya ya uzazi.

Katika hilo, Matindi anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto.

“Vituo vingi vya afya vya ngazi za chini vimeboreshwa ili kuhakikisha mama anapata huduma salama kuanzia anapopanga kupata ujauzito, wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na hata baada ya kujifungua,” anasema.

Kwa mujibu wake, maboresho hayo pia yamewezesha kusambazwa kwa vifaa tiba muhimu katika vituo vya afya vya ngazi za chini, wakati hapo awali vifaa hivyo vilipatikana zaidi katika hospitali kubwa pekee.

Huduma hizo ni pamoja na huduma za dharura za uzazi, upasuaji wa kujifungua pamoja na uangalizi maalumu wa watoto wanaozaliwa na uzito mdogo.

Kwa kuimarisha huduma hizo katika vituo vya afya vya karibu na jamii, mama wengi wanaweza kupata huduma mapema na kupunguza hatari ya matatizo makubwa ya kiafya.

Matindi anasema hatua nyingine muhimu katika kuboresha huduma za afya ya uzazi ni kuimarisha uwezo wa wataalamu wa afya, hasa wakunga na wauguzi.

Anasema wataalamu hao hupatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza wakati wa ujauzito na kujifungua.

Mafunzo hayo hufanyika kwa njia mbalimbali, ikiwamo warsha za kitaalamu na programu za kujifunza kwa njia ya mtandao.

Kwa mujibu wa Matindi, mafunzo hayo mara nyingi hulenga kuwajengea uwezo wataalamu katika kukabiliana na changamoto za dharura zinazoweza kujitokeza wakati wa kujifungua.

Anasema pale kifo cha mama kinapotokea na kubainika kuwa kingeweza kuepukika, wataalamu kutoka hospitali husika hukutana na madaktari bingwa kutoka Muhimbili ili kufanya uchambuzi wa kina.

Kupitia vikao hivyo, wataalamu hupitia tukio hilo kwa undani na kutoa mapendekezo ya kitaalamu ya namna ya kuboresha huduma na kuzuia tukio kama hilo lisitokee tena.

Changamoto katika mfumo wa rufaa

Licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kuboresha huduma za afya ya uzazi, Matindi anakiri kuwa bado kuna changamoto katika mfumo wa rufaa wa wagonjwa.

Changamoto hizo anasema, zinahusiana zaidi na miundombinu ya barabara pamoja na msongamano wa magari katika baadhi ya maeneo.

Anaeleza kuwa wakati mwingine mama anaweza kuanza safari ya kwenda hospitali mapema, lakini akakutana na ucheleweshaji njiani kutokana na foleni au hali mbaya ya barabara.

“Hakuna njia maalumu za dharura kwa magari ya wagonjwa katika baadhi ya maeneo, hivyo mama anaweza kuchelewa kufika hospitali kutokana na msongamano wa magari au miundombinu ya barabara,” anasema.

Hata hivyo, anasema vituo vya afya vinapokutana na changamoto kubwa ya kitabibu, vinaweza kuwasiliana moja kwa moja na madaktari bingwa wa Muhimbili kwa njia ya simu ili kupata ushauri wa haraka.

Anasema ushauri huo hutolewa kabla ya mgonjwa hajawasili hospitalini na mara nyingi husaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Takwimu zinaonyesha mafanikio

Matindi anasema juhudi zinazofanywa na Serikali pamoja na wadau wa sekta ya afya zimeanza kuonesha matokeo chanya katika kupunguza vifo vya wajawazito.

Anasema takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 2019 kulikuwa na vifo 556 vya wajawazito vilivyorekodiwa, lakini kufikia mwaka 2023 idadi hiyo ilishuka hadi vifo 104.

Hali hiyo inaonesha kuwa juhudi zinazofanywa katika kuboresha huduma za afya ya uzazi zinaanza kuzaa matunda.

Lengo la Taifa ni kupunguza vifo vya wajawazito hadi kufikia 70 kwa kila vizazi hai 100,000.

“Kwa ushirikiano wa pamoja tunaamini tunaweza kufikia lengo hilo,” anasema Matindi.

Ushirikiano wa sekta mbalimbali

Matindi anasisitiza kuwa, kupunguza vifo vya wajawazito si jukumu la sekta ya afya pekee, bali linahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali.

Anataja sekta za miundombinu, elimu na jamii kuwa na nafasi muhimu katika kuhakikisha mjamzito anapata huduma kwa wakati.

Kwa mfano, barabara zisizo rafiki au umbali mrefu wa kufika kituo cha afya vinaweza kuwa hatari kwa mjamzito anayehitaji huduma ya haraka.

Aidha, ukosefu wa uelewa katika jamii kuhusu dalili hatarishi za ujauzito unaweza kusababisha kuchelewa kufika hospitalini.

“Ni muhimu jamii ifahamu dalili hatarishi. Mjamzito akipata dalili kama kizunguzungu au changamoto nyingine, ni muhimu kuwahi hospitali mapema,” anasema.

Matindi anataja mimba katika umri mdogo kuwa moja ya changamoto zinazoweza kuhatarisha maisha ya mama wakati wa kujifungua.

Anasema wasichana wanaopata ujauzito katika umri mdogo mara nyingi miili yao haijakomaa vya kutosha kukabiliana na changamoto za uzazi.

Kwa sababu hiyo, anasisitiza umuhimu wa kuimarisha elimu ya afya ya uzazi kwa vijana pamoja na kuongeza juhudi za kuwafikia vijana katika jamii.

Kulinganisha tamaduni na tiba ya kisasa

Katika juhudi za kupunguza vifo vya wajawazito, Matindi anasema wataalamu wa afya wanapaswa pia kuzingatia tamaduni za jamii.

Hata hivyo, anasisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha tamaduni hizo hazihatarishi maisha ya mama na mtoto.

Anasema wataalamu wa afya wamekuwa wakitoa elimu kwa wakunga wa jadi na wahudumu wa afya katika jamii ili waweze kutambua dalili hatarishi na kuwapeleka wajawazito hospitalini mapema.

“Hatuondoi kabisa tamaduni, lakini tunataka kuwe na uwiano kati ya tamaduni na huduma za kisasa ili kulinda maisha ya mama na mtoto,” anasema.

Akihitimisha mahojiano hayo, Matindi anasema lengo la wataalamu wa afya ni kuona kila mama anajifungua salama na kuendelea kuishi baada ya kuleta maisha mapya duniani.

“Kama mama, naamini hakuna mama anayepaswa kupoteza maisha wakati wa kuleta uhai wa binadamu mwingine. Kila maisha yana thamani,” anasema.