Moto wateketeza vibanda 20 Masai Market, Iringa

Iringa. Moto mkubwa umeharibu vibanda takribani 20 vya wafanyabiashara katika soko la Masai Market lililopo mjini Iringa.

Tukio hilo limetokea katika eneo la Garden, lililopo mkabala na ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, baada ya kuzuka usiku wa kuamkia leo Machi 16, 2026, na umesababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara wanaojishughulisha na biashara za utalii katika soko hilo.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, moto huo ulizuka ghafla saa tano usiku na kusababisha taharuki miongoni mwa wafanyabiashara pamoja na wakazi wa maeneo ya jirani.

Wananchi waliokuwa karibu na eneo la tukio wamesema walijaribu kuokoa baadhi ya mali, lakini juhudi zao hazikufanikiwa kutokana na kasi ya moto kusambaa katika vibanda vilivyokuwa karibu.

Vibanda vya Masai Market Manispaa ya Iringa vilivyokuwa vikiteketea kwa moto usiku wa kuamkia Machi 16, 2026. Picha na Christina Thobias

Soko la Masai Market linamilikiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na hutumiwa na zaidi ya wafanyabiashara 50 wanaouza bidhaa mbalimbali za utalii. Bidhaa zinazopatikana katika soko hilo ni pamoja na vinyago, shanga, mapambo ya asili, na vitu vingine vinavyovutia watalii.

Baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa na vibanda katika eneo hilo wameathirika moja kwa moja baada ya vibanda pamoja na bidhaa zao kuteketea kabisa kwa moto huo, huku wengi wao wakiwa wamehifadhi bidhaa zao ndani ya vibanda wakati tukio hilo lilipotokea.

Akizungumza katika eneo la tukio leo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, amesema moto huo ulizuka ghafla na hadi sasa chanzo chake bado hakijajulikana. Amesema mamlaka husika zinaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo chake.

Vibanda vya Masai Market Manispaa ya Iringa vilivyokuwa vikiteketea kwa moto usiku wa kuamkia Machi 16, 2026. Picha na Christina Thobias

Aidha, amesema Serikali imeanza kufanya tathmini ya haraka ili kubaini kiwango halisi cha uharibifu na hasara iliyosababishwa na tukio hilo.

“Mpaka sasa, hakuna taarifa ya mtu kupoteza maisha au kujeruhiwa, jambo tunalolishukuru licha ya uharibifu mkubwa wa mali uliotokea,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na Mwananchi wamesema tukio hilo limewaathiri kwa kiasi kikubwa kiuchumi, kwa kuwa wengi wao walitegemea biashara hiyo kama chanzo kikuu cha kipato kwa familia zao.

Wamesema pia baadhi yao walikuwa wamechukua mikopo kupitia mpango wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, hali inayowatia wasiwasi kuhusu uwezo wa kurejesha mikopo hiyo baada ya kupoteza bidhaa zao.

Muonekano wa masalia ya vibanda vya biashara eneo la Masai Market Manispaa ya Iringa baada ya kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia Machi 16, 2026. Picha  na Christina Thobias

Mmoja wa wafanyabiashara hao aliyejitambulisha kwa jina la Ras Kibodya amesema vibanda vingi pamoja na bidhaa zilizokuwa ndani vimeteketea.

“Wafanyabiashara wengi tumewekeza fedha nyingi kununua bidhaa za utalii, na wengine tulijiandaa na msimu wa wageni wanaotembelea Mkoa wa Iringa na hifadhi za karibu,” amesema Kibodya.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Masai Market, Oscar Onesmo, amesema alipokea taarifa ya tukio hilo kutoka kwa walinzi wa soko hilo na kufika haraka katika eneo la tukio na kukuta kibanda namba 17 kikiwa tayari kinawaka moto.

“Tulijaribu kuwasiliana na Jeshi la Zimamoto ili kuja kudhibiti moto huo, huku baadhi ya watu nao wakijaribu kuokoa mali zao,” amesema Onesmo.

Hata hivyo, amesema wakati zimamoto ikiwasili, vibanda viwili tayari vilikuwa vimeungua na moto ulikuwa umeanza kusambaa kwa kasi kubwa kwenye vibanda vingine vilivyokuwa jirani.

Muonekano wa masalia ya vibanda vya biashara eneo la Masai Market Manispaa ya Iringa baada ya kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia Machi 16, 2026. Picha  na Christina Thobias

Kutokana na hali hiyo, moto uliendelea kuenea na hatimaye kuteketeza vibanda takribani 20, hali iliyosababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara wa soko hilo na kuwaacha wengi wao wakihitaji msaada ili kurejea katika shughuli zao za biashara.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Iringa, Jackline Mtui, amesema walipofika eneo la tukio, moto ulikuwa umesambaa kwenye vibanda kadhaa.

Amesema mpaka sasa chanzo cha moto huo bado hakijafahamika, huku uchunguzi ukiendelea ili kubaini kilichosababisha.

“Hata hivyo, hatujapokea wala kushuhudia madhara kwa binadamu yaliyotokea, ila mali na vibanda vimeungua kwa kiwango kikubwa,” amesema kamanda huyo.