Operesheni maalumu ya Polisi, Maliasili yanasa meno ya tembo Morogoro

Morogoro. Operesheni maalumu iliyofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na askari wa Maliasili imefanikiwa kunasa mtandao unaodaiwa kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo baada ya watuhumiwa wawili kukamatwa wakiwa na vipande 12 vya meno ya tembo mkoani hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Machi 16, 2026 mjini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema watuhumiwa hao walikamatwa katika maeneo tofauti ya Wilaya ya Mvomero wakiwa na vipande hivyo vinavyokadiriwa kuwa sawa na tembo watatu waliouawa kinyume cha sheria.

Kamanda Mkama amesema tukio la kwanza lilitokea Machi 14, 2026 katika Kitongoji cha Mambosije Darajani, Kata ya Mlandizi, wilayani Mvomero ambako polisi kwa kushirikiana na askari wa maliasili walimkamata mfugaji mkazi wa Kijiji cha Mangae, Omary Ali (58).

Wakati wa kukamatwa kwake, mtuhumiwa huyo alikutwa na vipande vinane vya meno ya tembo vinavyodaiwa kuwa sawa na tembo wawili.

“Baada ya kukamatwa kwa Omari, siku iliyofuata ya Machi 15, 2026, eneo la Kibaoni, Kijiji cha Melela wilayani Mvomero, askari hao walimkamata mkulima, mkazi wa Kijiji cha Kidodi wilayani Kilombero, Abdulkarim Mashaka (56) na alikutwa na vipande vinne vya meno ya tembo vinavyokadiriwa kuwa sawa na tembo mmoja,” amesema Kamanda Mkama.

Amesema watuhumiwa hao wamekamatwa katika operesheni zilizofanywa kwa nyakati tofauti na wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wakati uchunguzi unaendelea ili kubaini mtandao mzima wa biashara hiyo haramu.

Amesema baada ya uchunguzi kukamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili kwa mujibu wa sheria za uhifadhi wa wanyamapori.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limewakamata watu watatu wakituhumiwa kumiliki bastola kinyume cha sheria katika operesheni iliyofanyika katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Kamanda Mkama amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Stanislaus Zumbi (51), Salim Omar (33) na Ibrahim Yusuf (45), wote wakazi wa Kinondoni wakiwa na bastola aina ya Browning yenye namba B.395661 ikiwa na risasi tano katika magazine.

Watuhumiwa hao walikamatwa baada ya kufanyika kwa operesheni maalumu iliyolenga kukabiliana na uhalifu wa matumizi na umiliki haramu wa silaha za moto.

Uchunguzi wa matukio hayo unaendelea, watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani baada ya taratibu za kisheria kukamilika.