Simba, Yanga zapigana vikumbo saini ya Fofana

YANGA jana usiku ilikuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa ikipambana kwenye Dar es Salaam Dabi dhidi ya wenyeji wa Azam FC lakini kuna vurugu mabosi wao wameifanya nchini Ivory Coast itakayomfanya mtani wake Simba kujipanga sawasawa kivita.

Mabosi wa Yanga wamevamia pale ASEC na wamepima maji na kuona yule mshambuliaji Souleyman Fofana anawafaa kwa matumizi ya kikosi chao msimu ujao huku wakiweka nguvu kubwa kuinasa saini yake.

Simba ndiyo ilikuwa ya kwanza kumpigia hesabu Fofana, ambaye anamudu kucheza nafasi tofauti za kiungo mshambuliaji, na tayari wekundu hao walishafanya vikao vya mawasiliano na wasimamizi wa mchezaji huyo wakimtaka kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.

Kitu pekee ambacho Simba haikufanya mpaka wiki iliyopita ilikuwa ni kuzungumza na mabosi wa ASEC Mimosas kutokana na klabu hiyo bado inamkataba halali na Fofana na waliona njia sahihi ni kuanza na uongozi wa mchezaji, ukiridhia wanakwenda moja kwa moja mezani ASEC.

Ingawa mabosi wa Yanga wanafanya siri lakini Mwanaspoti linafahamu kwa uhakika kwamba juzi Jumamosi usiku Machi 14, bosi mmoja wa juu wa Yanga alifanikiwa kuzungumza moja kwa moja na wasimamizi wa mchezaji huyo wakiuliza uwezekano wa kumpata mwishoni mwa msimu huu.

Kama haitoshi leo Jumatatu Yanga imeweka miadi na bosi mmoja wa idara ya ufundi ya ASEC kuanza mazungumzo ya kutafuta saini ya mshambuliaji huyo ambaye kwasasa yupo moto kwenye Ligi Kuu ya Ivory Coast.

“Tulikuwa tunamfahamu Fofana muda mrefu hatujamfuata kutokana na Simba kumtaka, sisi ndio timu tuliyechukua wachezaji wengi moja kwa moja kutoka pale na tuna watu wengi, tulishaletewa hili jina muda ila sasa tumeona yuko sawa kusajililiwa.

“Tumeshazungumza naye si unaona (anaonyesha simu za mchezaji huyo na zile za wasimamizi wake sambamba na picha mnato za simu za video), kuna kiongozi wa ASEC tutazungumza naye Jumatatu (leo) aliomba tumpigie siku hiyo..

“Kama Simba wanamtaka basi na sisi tunamtaka, tutaona nani atafanikiwa kumpata kulingana na ofa ya kila mmoja, sisi kumkosa labda aende klabu nyingine na sio za hapa nchini siku hili likikamilika nitakupa siri kubwa zaidi.”

Mapema Rais wa ASEC Roger Ouegnin akiongea kwa njia ya simu na Mwanaspoti alisema bado hawajapokea ofa rasmi ya Simba wala klabu yeyote Tanzania ingawa hawana shida ya kumuuza mshambuliaji huyo endapo makubaliano yakifikiwa.

“Naweza kukuthibitishia kwamba mpaka sasa hatujapokea ofa yoyote kutoka klabu ya Simba kama unavyouliza, Fofana ni mchezaji wetu anaendelea kutumikia mkataba wake, tunafurahia kiwango chake,”alisema Ouegnin.

“ASEC hatuna shida kwenye kufanya biashara kwa wachezaji, kama tukikubaliana kila kitu kinawezekana lakini huyu Fofana ana ofa nyingi sana hapa Afrika na hata Ulaya, kwetu sisi tutaangalia timu itakayofikia mahitaji tunayoyataka na tunaweza kumuachia mchezaji.”

Msimu huu namba za Fofana zipo juu akiwa ameshafunga jumla ya mabao 11 kwenye mechi 21 alizocheza akiwa ndio mfungaji kinara ndani ya timu hiyo.

Achana na kufunga Fofana pia ni mjuzi wa kutengeneza mabao akiwa na jumla ya asisti tano na kumfanya kuhusika kwenye jumla ya  mabao 16 kwenye timu yake kabla msimu haujamalizika.