BEKI wa Tanzania, Julietha Singano ameandika rekodi ya kuwa miongoni mwa wachezaji waliocheza mechi nyingi katika kikosi cha FC Juarez Femenil kinachoshiriki ligi ya wanawake ya Mexico.
Singano ambaye ni beki tegemeo wa timu hiyo, ameonyesha uimara mkubwa tangu alipojiunga na klabu hiyo, akifanikiwa kucheza jumla ya mechi 103 katika ligi.
Katika kipindi hicho, beki huyo ameonyesha mchango wake sio tu katika kulinda safu ya beki bali pia kwenye ushambuliaji, akifunga mabao mawili na kutoa asisti nne.
Msimu huu Singano amecheza mechi 26, akifunga bao moja na kutoa asisti moja akionyeshwa kadi tano za njano.
Msimu wa 2024/2025 uliendelea kuwa mzuri kwake baada ya kucheza mechi 33, akifunga bao moja, asisti moja na kuonyeshwa kadi sita za njano.
Katika msimu wa 2023/2024, alicheza mechi 30, hakufunga bao lakini alitoa asisti tatu, huku akionyeshwa kadi nane za njano.
Mbali na Singano Mtanzania mwingine anayekipiga ligi hiyo ni kiungo mshambuliaji, Enekia Lunyamila ambaye alijiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Mazaltan ya nchini humo.
Msimu wake wa kwanza 2022/2023 kujiunga na timu hiyo akitokea Simba Queens alicheza mechi 14, hakufunga wala kutoa asisti.
Kwa jumla, takwimu hizo zinaonyesha jinsi Singano alivyokuwa mchezaji muhimu kwenye safu ya mabeki ya timu hiyo na kuonyesha ushindani mkubwa na nyota wakubwa.
Uwezo wake wa kucheza mechi nyingi unaonyesha kiwango cha kuaminiwa na benchi la ufundi la timu hiyo, jambo ambalo limeendelea kumfanya kuwa mmoja wa mabeki wa kuaminika kikosini hapo.