Urithi wa Magufuli; mafanikio, changamoto na mjadala wa haki za binadamu

Dar es Salaam. Miaka mitano imepita tangu kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli, lakini jina lake bado linaendelea kuibua mijadala katika siasa, uchumi, na utawala wa umma.

Moja ya vipengele vilivyomfanya ashikilie kumbukumbu ya wananchi ni majina ya utani aliyoyapata ya JPM, Buldoza, Jiwe na Chuma.

Kila jina linaashiria sifa maalumu za utendaji wake na mtazamo wa kipekee kuhusu utumishi wa umma. Kifupi cha jina lake, JPM (John Pombe Magufuli), lilitumika kama njia ya kumtambua kwa heshima na urahisi.

Buldoza ni jina lililotokana na uthubutu wake wa kusukuma miradi mikubwa ya maendeleo bila woga, kama buldoza inavyosukuma ardhi kwa nguvu.

Jiwe, kwa upande mwingine, linahusiana na uthabiti wake, alijulikana kama kiongozi mgumu kumshawishi au kubadilisha msimamo wake, kama jiwe lisiloyeyuka.

Chuma linatambua nguvu, akithibitisha uthabiti na utendakaji wa lazima bila upole.

Majina haya yote yanadhihirisha uthubutu, uthabiti na nguvu ya kutekeleza uamuzi, sifa zilizomfanya Magufuli ashikilie msimamo wake bila hofu, hususan katika kutetea wananchi wanyonge, maendeleo ya Taifa na kurejesha nidhamu katika utumishi wa umma.

Hadi sasa, majina haya ni sehemu ya urithi wa kipekee unaoendelea kuzungumzwa na wanahabari, wanasiasa na wananchi, wakitathmini mafanikio yake pamoja na changamoto za mtindo wake wa uongozi.

Kwa baadhi ya wadau, anaendelea kukumbukwa kwa uthubutu wa kusukuma miradi mikubwa ya maendeleo na kurejesha nidhamu katika utumishi wa umma, hata hivyo, kwa wengine utawala wake uliibua mjadala mpana kuhusu demokrasia na haki za binadamu.


Samia atangaza kifo cha Magufuli

Miaka mitano bila uwepo wake, tathmini ya urithi wake inaonekana kugawanyika kati ya mafanikio ya kiutendaji na maswali kuhusu athari za kisiasa zilizoachwa na mtindo wake wa uongozi, huku mema yake yakitajwa kama nguzo za maendeleo alizoziasisi kwa Taifa.

Nidhamu ya utumishi na ulinzi wa rasilimali

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda, anasema mjadala wa urithi wa Magufuli unapaswa kufanywa kwa uwiano unaokubali mafanikio na upungufu wake kwa wakati mmoja.

“Magufuli si kuwa alikuwa mkamilifu kama binadamu, alifanya mazuri na ambayo hayakuwa mazuri, alishambulia demokrasia na kipindi chake kulikuwa na kumomonyoka kwa haki za binadamu. Kama Mwalimu Julius Nyerere alivyosema kila uongozi ana mema yake na mabaya yake,” anasema.

Mbunda anasema licha ya ukosoaji, utawala wa Magufuli uliweka alama katika kurejesha nidhamu kwa watumishi wa umma na kuhimiza uwajibikaji serikalini, jambo ambalo linaonekana kushuka kwa Taifa baada ya kifo chake.

Aidha, alionesha uzalendo mkubwa katika ulinzi wa rasilimali za Taifa, hasa sekta ya madini, kwa kufumua mikataba na kuiweka mikononi mwa wananchi.

Dk Mbunda pia anasema uthubutu wake ulihamasisha ujenzi wa miundombinu na kupambana na ufisadi, lakini anakemea kuwa mafanikio haya yangekuwa thabiti zaidi kama yangeambatana na mifumo imara ya uwajibikaji.


Magufuli alivyomtumbua DC na kumrudisha

“Leo viongozi wa umma, Waziri Mkuu anasimama anakutana na malalamiko mengi huko kwa sababu viongozi hawajajengewa mifumo ya kuwajibika. Pia, vita ya ufisadi; tumekuwa kimya sana lakini ripoti za ukaguzi za CAG (Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali) zikitoka zimekuwa zikiibua mengi sana,” anasema.

Uongozi wa uthubutu na vita dhidi ya rushwa

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza anamtaja Magufuli kama kiongozi wa uthubutu na mfano binafsi.

Kwa mtazamo wake, sifa hiyo ndiyo iliyomfanya aonekane tofauti na baadhi ya viongozi waliomtangulia, akiweka wazi kuwa kiongozi huyo, “alikuwa anajituma, hakutuma. Alikuwa tayari kupendwa na kuchukiwa.”

“Alikuwa na uthubutu wa kuikemea rushwa. Sasa hivi rushwa inawakemea viongozi,” anaongeza Bagonza huku akikiri kuwa katika eneo la haki za binadamu kulikuwa na ukosoaji mkubwa kuhusu mtindo wa uongozi wa Magufuli na kumtaja kuwa, alikuwa mgeni mno katika eneo la haki za binadamu.

Bagonza anasema uthubutu wake ulionekana zaidi katika vita dhidi ya rushwa na kuhimiza uwajibikaji wa viongozi wa umma, akibainisha kuwa nguvu hiyo sasa imeshuka.


‘Magufuli hana mpango wa kuongeza muda’

Hata hivyo, anakiri kuwa hakukuwa na msimamo thabiti katika haki za binadamu, akimtaja Magufuli kuwa, “mgeni mno katika eneo hilo.”

Mabadiliko ya hali ya uchumi na jamii

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani na Maadili kwa Madhehebu ya Dini, William Mwamalanga anasema miaka mitano baada ya kifo cha Magufuli, hali ya uchumi na jamii nchini imeonesha mabadiliko makubwa.

Anasema baadhi ya sekta za uchumi zimekumbwa na changamoto, hususan ajira za vijana katika biashara ndogo ndogo.

“Kiuchumi tumedorora sana, ajira za vijana kwa maana ya machinga zimeyumba, kama siyo kupotea kabisa,” anasema, akibainisha kuwa Magufuli aliwatetea sana vijana katika eneo hili.

Mwamalanga anasema jamii pia inakabiliwa na matukio yanayozua mjadala kuhusu usalama na maadili, ikiwamo mauaji yanayofanywa na wasio julikana, kuongezeka kwa chuki, ufisadi serikalini, na biashara ya dawa za kulevya.

Kuhusu miundombinu, Mwamalanga anasema baadhi ya miradi inaonekana kukosa mwendelezo, akikumbusha enzi za Magufuli; barabara hazikuruhusiwa kujengwa chini ya kiwango au kuchelewa ukarabati wa mashimo.

“Siyo kulegalega tu, bali miradi mingi imekufa kabisa. Barabara za Mwenge, Tegeta, Kimara na Mbagala ni mfano unaoonekana sasa, safiri Dar es Salaam hadi Tunduma ni mashimo tu,” anasema.


Kauli ya Magufuli usajili wa meli

Aidha, anaongeza kuwa, nidhamu katika utumishi wa umma iliyoshuhudiwa wakati wa utawala wa Magufuli ilianza kupungua muda mfupi baada ya kifo chake, jambo linaloathiri utendaji wa Serikali na miradi ya maendeleo.

Mtindo wa kisiasa uliobua mijadala

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, Denis Konga anasema tathmini ya urithi wa Magufuli inapaswa kuzingatia pia athari za kisiasa zilizobaki kutokana na mtindo wake wa uongozi.

“Kila mabaya tunayoyashuhudia sasa yalijengwa kipindi cha 2016–2019,” anasema akibainisha kuwa mfumo wa uamuzi uliotegemea nguvu ya kiongozi mmoja badala ya taasisi uliibuka.

“Hali hii ilichangia kujengwa kwa makundi ya wafuasi waliomuona kama kiongozi mwenye nguvu, huku uhuru wa maoni ukibana na nafasi ya wasomi kupunguzwa katika mijadala ya sera za Taifa.


Safari ya Magufuli kisiasa

“Alibana mno uhuru wa maoni na hakuwapenda wasomi ingawa aliwateua, huenda ndiyo ile Waingereza husema, waweke rafiki zako karibu na adui zako karibu zaidi,” anasema.

Miradi ya maendeleo na uwajibikaji

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Anna Henga anasema moja ya alama kubwa za utawala wa Magufuli ilikuwa kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Anataja miradi kama reli ya kisasa ya SGR na ujenzi wa barabara kama sehemu ya urithi unaoonekana hadi leo

“Uwajibikaji serikalini ulikuwa mzuri, pengine kutokana na ukali wake,” anasema.

Hata hivyo, Dk Henga anakiri kuwa pamoja na mafanikio hayo, kulikuwa na ukosoaji mkubwa kuhusu haki za binadamu, akibainisha kwamba, Magufuli aliamini zaidi katika kazi na kasi ya utekelezaji kuliko masuala ya haki za binadamu, wanawake au uhuru wa vyombo vya habari.