Wanawake wanufaika wa Tasaf wafungua kiwanda cha kusaga karanga

Mwanza. Wanawake 15 wa kikundi cha Wasikivu katika Mtaa wa Kabangaja, Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, wameazisha kiwanda kidogo cha kukaanga na kusaga karanga pamoja na kutengeneza sabuni, baada ya kuwezeshwa mtaji wa Sh11.5 milioni kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (Tasaf).

Kikundi hicho, chenye wanachama wote wanawake na walengwa wa mpango huo, kilianzishwa mwaka 2022 kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.

Kupitia awamu ya nne ya Tasaf, mwaka 2024 walipokea mtaji huo uliowawezesha kununua mashine ya kukaanga na kusaga karanga inayotumia umeme na gesi, pamoja na kuanzisha uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, ikiwemo siagi ya karanga, unga wa lishe na sabuni.

Akizungumza leo Jumatatu, Machi 16, 2026, wakati kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ilipotembelea kukagua mradi huo, mwenyekiti wa kikundi cha Wasikivu, Laurencia Lugendo, amesema waliibua wazo la mradi mwaka 2022 na baadaye kupata ufadhili kupitia Tasaf uliowasaidia kuanzisha shughuli za uzalishaji.

Amesema mradi ulianza kutekelezwa Agosti 2024, chini ya usimamizi wa kamati ya usimamizi wa jamii kwa kushirikiana na viongozi wa mtaa na wataalamu wa halmashauri, na kukamilika Septemba 2024.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Wasikivu, Laurencia Lukendo (wa kwanza kushoto) akitoa maelezo ya kikundi chao kilichoanzisha kiwanda kidogo cha kukaanga na kusaga karanga kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala, Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro (wapili kushoto).

“Kupitia uwezeshaji huu, sasa tumeanza safari ya kujitegemea kiuchumi huku tukitoa mfano wa jinsi miradi ya kijamii inavyoweza kubadilisha maisha ya wananchi masikini. Hadi sasa kikundi chetu kimepata faida ya zaidi ya Sh3 milioni na pia kimenunua kiwanja cha kujenga ofisi ya kudumu ya shughuli zetu,” amesema Laurencia.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji wa Mtaa wa Kabangaja, Chiku Said, amesema kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi, kamati ya usimamizi wa miradi ngazi ya jamii pamoja na viongozi wa mtaa walipatiwa mafunzo ya siku tatu ili kuwajengea uwezo wa kusimamia vyema mradi huo.

“Mafunzo hayo yalihusisha masuala ya bajeti ya mradi, utunzaji wa fedha, wajibu wa kamati za usimamizi, utunzaji wa stoo, mpango wa manunuzi pamoja na tathmini ya athari za mazingira na kijamii,” amesema.

Kupitia ujuzi waliopata kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), kikundi hicho sasa kinazalisha na kuuza bidhaa zake kwa wananchi, hatua iliyowawezesha kuongeza kipato.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesema matokeo ya uwezeshaji wa wanawake kupitia Tasaf yanaonekana kutokana na mafanikio ya kikundi hicho.

“Matokeo mazuri tunayoyaona leo si tu kwamba wanatengeneza faida, bali pia wanazalisha bidhaa zinazotumiwa na wananchi, huku wakijiongezea kipato,” amesema.

Amekitaka kikundi hicho kutangaza bidhaa zake ili kujipatia soko la uhakika ndani na nje ya Mkoa wa Mwanza.

Katika kuunga mkono juhudi zao, Serikali imetoa Sh7 milioni kwa kikundi hicho, huku Ridhiwani akieleza mbunge wa Ilemela, William Kafiti, aliyekuwa kwenye majukumu mengine, kaahidi kutoa Sh3 milioni fedha zitakazotumika kutunisha mfuko wa maendeleo wa kikundi hicho.

Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dk Neema Majule, amesema mafanikio hayo yanaonesha namna miradi ya Tasaf inavyowezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala, Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro akizungumza na wananchi baada ya kamati yake kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Mihama iliyopo Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.

Amesema kamati hiyo imekuwa ikisoma taarifa za mafanikio ya miradi ya Tasaf kwenye makaratasi, lakini ziara hiyo imewapa nafasi ya kuona matokeo halisi kwa wananchi.

“Hii ni hatua kubwa. Tutapeleka habari zenu kwa wanawake wengine, kwa sababu ukimkomboa mwanamke umekomboa familia na jamii nzima,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Shedrack Mziray, amesema hadi Julai 2024, kaya 400,000 zimeboresha hali zao za kiuchumi na kuhitimu kwenye mpango wa Tasaf.

Amesema zaidi ya miradi 1,500 ya kuendeleza miundombinu katika sekta ya elimu, afya, maji na kuongeza kipato imetekelezwa, huku zaidi ya vikundi 74,967 vyenye wanachama zaidi ya 900,000 viliundwa na kukusanya akiba ya zaidi ya Sh17.5 bilioni.

Katika hatua nyingine, kamati hiyo imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa zahanati ya Mihama, iliyojengwa kwa zaidi ya Sh232 milioni, ikijumlisha jengo la wagonjwa wa nje, nyumba ya watumishi, jengo la ukunga na vyoo.

Mradi huo umetekelezwa na wananchi kwa kushirikiana na Tasaf awamu ya nne kupitia mradi wa kupunguza umasikini (Opec) awamu ya nne.

Akizungumza baada ya kukagua zahanati hiyo, mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Damas Ndumbaro, ametaka ikabidhiwe Manispaa ya Ilemela na kutoa maelekezo ya kujengwa miundombinu ya kuzuia maji ya mvua yanayojaa eneo lililopo zahanati na kuleta adha kwa wagonjwa na wakazi wa maeneo jirani.

“Jukumu la kwanza ni kudhibiti maji ya mvua hapa… kuwe na mtaro wa juu na wa chini wa kutiririsha maji… sisi kamati tumeridhika, kazi ni nzuri,” amesema Dk Ndumbaro.