Watanzania washauriwa kumuenzi Magufuli kwa kuwajali wenye uhitaji

Chato. Wakati Makamu wa Rais, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi, amewasili wilayani Chato kwa ajili ya maadhimisho ya kumbukizi ya miaka mitano ya kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, hayati Dk John Magufuli, Watanzania wametakiwa kuendelea kumuenzi kwa kuwasaidia wenye uhitaji katika jamii.

Makamu wa Rais anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo yatakayofanyika kesho, Machi 17, 2026, mjini Chato mkoani Geita.

Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa dini, wanasiasa, wanajamii na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Wito huo umetolewa leo Machi 16, 2026 na Jesca Magufuli, mtoto wa Magufuli, ambaye amesema kuenzi urithi wa baba yake kunapaswa kuendana na kuendeleza falsafa yake ya kujali wanyonge.

Jesca ambaye ni mbunge wa Viti Maalumu (Vijana), amesema jamii inapaswa kuonesha mshikamano kwa kuwasaidia wenye mahitaji maalumu, hasa katika hospitali ambako baadhi ya wananchi hushindwa kumudu gharama za matibabu kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.

“Nitoe wito kwa wana-Chato na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuwasaidia wenye mahitaji ili wajisikie kuwa nao wana ndugu. Utamaduni wetu siku zote ni undugu, hivyo tuendelee kuwashika mkono wenzetu katika nyakati ngumu,” amesema.

Mtoto wa Hayati John Magufuli, Jesca Magufuli akichangia damu katika kuadhimisha miaka mitano ya kifo cha baba yake.

Miongoni mwa shughuli zilizofanyika leo ni maandamano ya amani kutoka stendi ya zamani ya Chato hadi Hospitali ya Wilaya, ambapo pia kulifanyika zoezi la uchangiaji damu likiongozwa na Jesca pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Musa Mwakitinya.

Jesca pia ameishukuru Serikali kwa kuboresha miundombinu ya afya katika Hospitali ya Wilaya ya Chato, akisema awali huduma na majengo ya hospitali hiyo yalikuwa duni, lakini sasa imepiga hatua kutokana na uwekezaji wa Serikali.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Chato, Dk Madili Sakumi, amesema msaada uliotolewa utasaidia wagonjwa wengi, hasa wanaotoka visiwa vya Ziwa Victoria ambao mara nyingi hushindwa kumudu gharama za matibabu.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Chato, Dk Madili Sakumi akizungumza wakati wa uchangiaji damu katika kumuenzi aliyekuwa Rais ya Tanzania, Hayati John Magufuli.

Amesema hospitali hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya nyumba za watumishi pamoja na uzio wa hospitali ambao umechakaa kutokana na kudumu kwa muda mrefu.

“Hata walinzi wetu wanapata changamoto kwa sababu hospitali haina uzio imara, hivyo mgonjwa anaweza kutoroka kupitia sehemu yoyote,” amesema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma za Maabara na Mpango wa Damu Salama katika hospitali hiyo, Ngolo Ngusa, amesema hospitali inakabiliwa na uhaba wa damu kutokana na mwitikio mdogo wa wananchi katika uchangiaji damu.

Amesema kwa muda mrefu hospitali imekuwa ikitegemea zaidi wanafunzi wa shule kama wachangiaji wakuu wa damu, hali inayosababisha upungufu mkubwa kipindi cha likizo.

Ngusa ametoa wito kwa jamii kujitokeza kuchangia damu mara kwa mara ili kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa, hususan wajawazito, watoto wachanga, waathirika wa ajali, wagonjwa wa selimundu na wenye matatizo ya ini, ambao mara nyingi huhitaji damu kwa dharura.