Dar es Salaam. Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba ameagiza kukamatwa kwa watu wote waliohusika na ununuzi wa mabati yasiyokidhi viwango yenye thamani ya takribani Sh200 milioni yaliyokusudiwa kutumika katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya wavulana Katavi.
Pia, ameagiza viongozi wa vyama vya ushirika wanaodaiwa kuhusika katika ubadhirifu wa fedha za mbolea katika Mkoa wa Katavi kuondolewa madarakani baada ya kesi yao kukamilika.
Akizungumza na wananchi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, leo Jumatatu ya Machi 16, 2026, Dk Nchemba amesema Serikali haitavumilia matumizi mabaya ya fedha za umma wala matumizi mabaya ya nafasi za uongozi katika taasisi zilizoundwa kuwahudumia wananchi hususan wakulima.
Waziri Mkuu kwa sasa yupo katika ziara ya kikazi Mkoa wa Katavi, ambako anakutana na wananchi, kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowasilishwa na wakazi wa maeneo hayo.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu ameongea kwa hasira wakati akizungumzia matumizi ya takribani Sh200 milioni kununua mabati 4,000 kutoka Mwanza kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Katavi, ambayo baadaye iligundulika kuwa hayafai kutumika katika mradi huo.
Amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi kumkamata mkandarasi aliyenunua mabati pamoja na maofisa wote wa umma waliohusika katika mchakato wa ununuzi huo hadi Serikali itakapopata fedha zake na kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi yao.
“Mlifuata mabati hadi Mwanza, sasa kwa nini mkanunua mabati yasiyofaa? Ni nani aliyefanya uamuzi huu ambao umeilazimu Serikali kutumia fedha mara mbili?” amehoji.
“RPC, mkamate mkandarasi aliyesambaza mabati hayo pamoja na maofisa wote waliohusika hadi fedha zirudishwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.”
Dk Nchemba ameeleza kuwa, uzembe wa aina hiyo hausababishi tu upotevu wa rasilimali za umma bali pia huchelewesha utekelezaji wa miradi muhimu ya maendeleo inayolenga kuwanufaisha wananchi hasa katika sekta ya elimu.
Amesema Serikali inatarajia uwajibikaji kutoka kwa watumishi wote wa umma na makandarasi wanaotekeleza miradi ya Serikali, akisisitiza kuwa yeyote atakayebainika kutumia vibaya rasilimali za umma atachukuliwa hatua za kisheria.
“Fedha ambayo tungenunua madawati, watoto wasikae chini imeenda kununua mabati ya hovyo, na fedha inaendelea kubaki huko inafanya nini, fedha ya Serikali, mabati siyo imebaki kule inafanya nini,” amehoji.
Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda, Sophia Kumbulia amesema baada ya tukio hilo waliendelea kuwasiliana na Mkandarasi arejeshe fedha zote na mpaka sasa hajarejesha huku mawakili wa Serikali wakiendelea na kazi.
Katika hilo, Dk Mwigulu amesema: “Mnasumbua mawakili, mmempa fedha ameleta bati tusizozitaka, mnasumbua mawakili katika jambo lililo wazi hivi, kamanda wa Takukuru muelekeze kamanda mwenzako wa polisi Mkoa, (mkandarasi) akamatwe asiwe huru hadi arejeshe hizi fedha. Kamanda wa Takukuru chunguza wote hawa kila mmoja tuone ushiriki wake, mnatumia makandarasi marafiki zetu kutanguliza fedha ya Serikali ili mgawane,” amesema.
Amesema suala hilo lilisababisha halmashauri kuchepusha fedha nyingine za matumizi, ili kununua mabati hayo jambo ambalo amesema fedha za umma hazihitaji majadiliano.
“Hatuwezi kubembelezana juu ya fedha ya umma, mnajua Watanzania wanaolipa kodi wana maisha gani, kuna mama huko ana mtoto mgongoni anashindwa hata kitumbua, anadaiwa alipie kibanda ushuru nyie mtu anachukua fedha mnamuangalia au mmegawana,” amesema.
Ametaka wote waliohusika wakiwamo walioweka saini ununuzi huo wakamatwe, warudishe fedha na wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Pia, amemtaka Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa (Tamisemi) kufuatilia watumishi wote ili wakimaliza kesi ya jinai wafunguliwe faili la nidhamu.
“Kama siyo mnashirikiana nao ni nini, kamanda wasakeni wote wakamatwe na msiwaachie hadi hiyo fedha irudi, hatuwezi kuwa tunabembelezana hiyo fedha ya umma,” amesema.
Amesema Watanzania wamekuwa wakilipa kodi kwa kujibana na wengine wanapochelewa huingia katika misukosuko na Serikali wakati baadhi yao hata kupata Sh20,000 ni kazi.
“Halafu tunaelezewa tu tuliagiza haya mabati yakaonekana siyo yale yaliyoelekezwa, hivyo tukaomba hela nyingine serikalini, ujinga,” amesema.
Waziri Mkuu pia ametumia nafasi hiyo kuzungumzia taarifa za madai ya ubadhirifu wa fedha za mbolea ndani ya Vyama vya Ushirika (AMCOS) katika mkoa huo.
Ameagiza viongozi wote wa ushirika wanaoshukiwa kuhusika katika wizi huo kuondolewa madarakani mara moja, hata kama kesi zao bado zinaendelea mahakamani.
Amesema kuruhusu viongozi hao kuendelea kubaki madarakani kunadhoofisha uadilifu wa harakati za ushirika na kupunguza imani ya wakulima kwa taasisi zilizoundwa kuwasaidia.
“Haikubaliki kwa mtu anayeshutumiwa kuiba rasilimali za umma kurudisha fedha kisha kuendelea kushika nafasi ya uongozi kana kwamba hakuna kilichotokea,” amesema.
“Watu wanapaswa kusoma alama za nyakati. Hatuwezi kuunda mfumo ambao watu wanaiba wakidhani hakuna anayewaona, wakikamatwa wanarudisha fedha kisha wanaendelea na nafasi zao kana kwamba hakuna kilichotokea.”
Dk Nchemba amesema amepokea taarifa kuwa baadhi ya viongozi wa AMCOS waliotuhumiwa kuiba fedha za mbolea wamerudisha fedha hizo, lakini bado wanaendelea kushika nyadhifa zao.
“Nimeambiwa baadhi ya viongozi wa AMCOS walioiba fedha za mbolea wamerudisha fedha hizo, lakini bado wako madarakani. Hilo haliwezi kuendelea kuruhusiwa,” amesema.
Amemuagiza msajili wa vyama vya ushirika kwa kushirikiana na waziri wa kilimo kuhakikisha wote wanaotuhumiwa wanaondolewa mara moja katika nafasi zao huku kesi zao zikiendelea kusikilizwa mahakamani.
“Serikali imejipanga kuimarisha uwajibikaji na uwazi katika vyama vya ushirika ambavyo vina mchango mkubwa katika kuwasaidia wakulima kupata pembejeo za kilimo na masoko ya mazao yao na Serikali itachukua hatua kali dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kutumia vibaya rasilimali za ushirika au fedha za umma,” amesema.
