Unguja. Wakati mvua za masika zikiendelea, Zanzibar itatumia fursa hiyo kupanda miti milioni 3.273 itakayooteshwa katika vitalu mbalimbali kisiwani hapa.
Kati ya miti hiyo, milioni 2.227 itaoteshwa katika vitalu binafsi, na miche milioni 1.045 itaoteshwa katika vitalu vya serikali.
Miche hiyo, inayojumuisha ya matunda na viungo 2,117,458, misitu 637,173, minazi 16,200, mikarafuu 336,703 pamoja na mikoko au mikandaa 165,620, imeoteshwa katika vitalu vilivyopo idara tano za wizara hiyo na jumuiya binafsi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Jumatatu Machi 16, 2026, kuhusu upandaji wa miti hiyo, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Suleiman Masoud Makame, amesema sehemu kubwa ya miche hiyo itagawiwa bure kwa wananchi, ili wakapande katika maeneo yao.
“Miche iliyopo, ikijumuisha misitu, matunda na viungo, itapatikana kwa bei nafuu kutoka katika vitalu vya serikali vilivyopo katika maeneo ya Mwanyanya, Kibele, Dunga, Kitogani, Selem, Mwanakombo, Machui, Mwera na Makunduchi kwa Unguja,” amesema Waziri Suleiman.
Kwa upande wa Pemba, ni katika maeneo ya Konde, Wingwi, Weni, Dodeani, Chanjaani, Wesha na Kigope. Wananchi wameombwa kufika katika vitalu vilivyo karibu nao ili kujipatia miche hiyo.
Kwa miche ya minazi na mikarafuu, itatolewa bila malipo kwa utaratibu maalumu uliopangwa na wizara kwa kushirikiana na wilaya husika.
Lengo kuu la upandaji miti katika msimu huu wa masika 2026, kwa mujibu wa wizara, ni kuhifadhi mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ili kukamilisha lengo hilo, kwa upande wa mashamba ya Serikali, Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kupitia Idara ya Misitu imepanga kupanda jumla ya hekta 100 katika mashamba ya Serikali yaliyopo Chaani-Masingini, Kibele, Dunga-Jendele kwa Unguja na Maziwangombe Pemba.
Kwa upande wa misitu ya jamii, Serikali imeweka lengo la kusambaza na kupanda miti katika eneo lisilopungua hekta 50 katika maeneo mbalimbali ya jamii Unguja na Pemba.
“Upandaji huu utahusisha taasisi za Serikali, jumuiya zisizo za kiserikali, kamati za uhifadhi na wananchi wa kawaida. Miche hiyo itapandwa katika maeneo ya kingo za barabara, maeneo yaliyochimbwa mchanga pamoja na maeneo ya wazi mijini na vijijini.
Pia, barabara mbalimbali Unguja na Pemba, ikiwemo Miwani-Mwachealale, Selem-Mbuzini, Masingini-Kijichi, Msikiti wa Waarabu-Mbuzini, Kizimbani-Bumbwisudi, zitapandwa miti katika msimu.
“Kama nilivyosema awali, msimu wa masika umeshaanza, tuitumie fursa hii kupanda miti mbalimbali katika makaazi yetu, maeneo ya wazi, barabarani, shuleni na katika mashamba yetu,” amesema.
Kupanda miti ni jambo moja na kuitunza ni jambo lingine, hivyo waziri amewataka wananchi kuitunza ili kutoa matunda na manufaa yanayotarajiwa sambamba na kurudisha urithi wa kijani, kwani miti ina umuhimu mkubwa kupitia nyanja za kiuchumi, kimazingira na kijamii.
Pia, amesema inasaidia kupata hewa safi na salama, kuzuia mmong’onyoko wa ardhi, kutunza vyanzo vya maji, mazalia ya viumbe vya baharini wakiwemo samaki, makazi ya wanyamapori, kukuza kipato cha Serikali na jamii.
Baadhi ya wananchi wamesema hatua hiyo itasaidia kurejesha uasili wake kutokana na shughuli mbalimbali za miradi, ambazo zimepelekea kukatwa kwa miti mingi.
“Ukiangalia kwa sasa, kuna miti mingi imekatwa kutokana na miradi ya maendeleo, hususan ujenzi wa barabara na mahoteli katika maeneo mbalimbali,” amesema mmoja wa wananchi.,” amesema