Athari ya kiu ya ufaulu kwa wanafunzi  na Taifa

Shinyanga. Katika jamii nyingi leo, ufaulu umegeuka kuwa lengo kuu la elimu. Kila mzazi, mwalimu na mwanafunzi anatamani kuona alama za juu, vyeti vingi na matokeo yanayovutia.

 Hata hivyo, katika harakati hizo, mambo muhimu kama maadili, utu na ujuzi wa vitendo yameachwa nyuma au kupewa nafasi finyu.

Takwimu na hali halisi ya kijamii vinaonyesha kuwa shinikizo la kufaulu limeongezeka kwa kasi. Wanafunzi wanahimizwa kupata alama za juu bila kujengewa misingi imara ya maadili na ujuzi wa kujitegemea. Matokeo yake ni kuzalishwa kwa wahitimu wenye vyeti, lakini wasio na huruma, wasiothamini uadilifu na wasio tayari kuwajibika ipasavyo katika jamii.

Kamishna wa Elimu Dk Lyabwene Mtahabwa, anaonya kuwa jamii imesahau ukweli muhimu kwamba ufaulu hauna maana ikiwa haujaambatana na makuzi ya utu.

“Utu wa mtu hujengwa wakati wa ukuaji wa awali, kuanzia umri wa miaka minane. Jamii inapokazania ufaulu na kusahau kumjenga mtoto katika misingi ya utu mapema, ndipo Taifa linapozalisha mafisadi wa baadaye,” anasema alipohojiwa na Kituo kimoja cha televisheni nchini

Anaeleza kuwa mfumo wa elimu umewatoa watoto katika maarifa ya uzalishaji kama uvuvi, ufugaji na uchimbaji madini, na kuwaingiza katika mkazo wa kufaulu mitihani ya nadharia.

Badala ya kujifunza kwa vitendo, wamebaki kujadili vishazi, aina za tungo na hata masuala ya mazingira bila kupanda mti hata mmoja.

“Tumekuwa na ugonjwa wa ufaulu, ufaulu, ufaulu. Hatujiulizi kama ufaulu una maana bila kuzingatia maadili. Masuala ya kitaaluma ni jambo moja, lakini masuala ya kimaadili ambayo Rais Samia amekuwa akiyasisitiza ni makubwa zaidi,” anasisitiza.

Kwa mtazamo huo, ni dhahiri kwamba jamii inapaswa kubadili mwelekeo. Elimu inahitaji kurejesha mizani kati ya maarifa ya darasani na makuzi ya utu, ili kuzalisha watu wanaoweza kufanya kazi kwa uadilifu na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Mwalimu mstaafu katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, Lucas Matanganya, anaona kiu ya ufaulu ya sasa kwa kiasi fulani, inachochewa na utekelezaji wa sera ya kuhakikisha kila mtoto anamaliza angalau kidato cha nne.

“Kwa sasa shule zimeongezeka, watoto ni wengi na nafasi za juu zimepanuka. Maelekezo ya Serikali kwamba kila mtoto asome angalau mpaka kidato cha nne yameongeza mashindano ya ufaulu kila mwaka,” anasema.

Anaongeza kuwa zamani kulikuwa na mchujo mkali kutokana na uchache wa shule na wanafunzi.

“Ukifaulu kipindi kile, ilikuwa ni kazi kubwa. Tulichujwa kweli kweli,” anasema.

Kwa upande wa malezi, Matanganya anasisitiza kuwa jukumu la kumjenga mtoto si la mwalimu pekee. Anabainisha kuwa msingi wa maadili huanzia nyumbani, ambako mtoto huanza kujifunza hofu ya Mungu, uwajibikaji na nidhamu kabla ya kuingia shuleni.

“Sio walimu pekee wanaopaswa kuwalea watoto kuwa viongozi sahihi wa baadaye. Wazazi wana jukumu kubwa, kwa sababu mtoto anaanza shule akiwa na miaka sita au saba. Msingi wa maadili hujengwa nyumbani, mwalimu anaongeza tu,” anasema.

Kiu ya ufaulu kisaikolojia

Mtaalamu wa saikolojia na mshauri wa masuala ya kijamii, Mwalimu Yatabu, anaeleza kuwa kiu ya ufaulu imeleta athari kubwa kisaikolojia kwa watoto na vijana.

“Masomo ya darasani pekee hayatoshi kumwandaa mtoto kuwa mtu sahihi na mwenye tija. Ufaulu wa darasani umekuwa ukiua vipaji na kuwatengeneza watu kuwa wasomi tu, ilhali kuna tofauti kubwa kati ya msomi na mwenye elimu,” anasema.

Kwa mtazamo wake, msomi ni yule anayekariri alichofundishwa na kuamini kuwa hawezi kufanya chochote nje ya taaluma yake. Mara nyingi huamini katika kuajiriwa na kulipwa mshahara, kuishi kwenye nyumba za kampuni au serikali na kutegemea mfumo rasmi wa ajira.

Tofauti na hilo, mwenye elimu hutumia uwezo wake asilia kuendesha maisha na kuibua ubunifu unaoweza kuleta mabadiliko chanya bila kuathiri mazingira.

Yatabu anaonya kuwa kumkaririsha mtoto tangu utotoni kwamba maisha mazuri yanategemea alama za juu pekee, kunamjengea hofu ya kushindwa na kumwondolea uwezo wa kutambua kipaji chake.

“Mtoto anaweka nguvu kwenye alama za juu bila kufundishwa namna ya kutambua uwezo wake wa ndani. Akifeli, anajiona hana akili, anapoteza kujiamini na kuathirika kisaikolojia,” anasema.

Anahoji pia mfumo wa mitihani unaoweka watoto wenye vipaji tofauti kwenye kipimo kimoja, akisema hali hiyo inaweza kumjenga mtoto kujiona duni maisha yake yote, bila kuzingatia kuwa uwezo wake uko katika eneo tofauti.

Kwa mtazamo wa kiuchumi, Yatabu anaona kuwa mfumo wa sasa unazalisha kizazi kinachoamini zaidi katika matumizi kuliko uzalishaji.

“Robo tatu ya vijana wanaamini katika kuajiriwa. Haya ni matokeo ya mfumo wa elimu unaong’ang’ania masomo ya darasani bila kuwajengea uwezo wa kuzalisha mawazo mapya,” anasema.

Anafafanua kuwa wanafunzi hufundishwa kutatua maswali ya mitihani, lakini hawapati elimu ya fedha, namna ya kuizalisha na kuisimamia. Matokeo yake ni wahitimu wenye vyeti vya shahada, stashahada na uzamili, lakini wasio na mchango halisi katika uchumi wa jamii.

Anaeleza kuwa mafanikio ya Taifa hutegemea ubunifu wa mara kwa mara. Hata hivyo, mfumo wa sasa unajenga ushindani wa kuficha maarifa badala ya kushirikiana. Hali hiyo inazuia mzunguko mpana wa maarifa na fursa za kiuchumi.

Mtaalamu na mtafiti mbobezi katika sekta ya elimu, Zaida Mgala, anaeleza kuwa athari za kiu ya ufaulu kwa watoto ni pana na za muda mrefu.

Anasema walimu wengi hulazimika kubobea katika mbinu za kukaririsha wanafunzi ili waweze kufaulu mitihani, badala ya kuwasaidia kuelewa kwa kina na kutumia maarifa kwa vitendo.

Hali hiyo husababisha msongamano wa kazi za ziada, hata wakati wa likizo. Wanafunzi hukosa muda wa kupumzika au kukuza vipaji vyao kwa sababu ya presha ya kutafuta alama za juu, ilhali soko la ajira linahitaji zaidi ujuzi na ubunifu kuliko makaratasi ya matokeo.

Zaida pia anaonya kuhusu mtazamo potofu wa jamii unaompima mtoto aliyefanikiwa kwa alama za juu pekee, huku elimu ya ufundi kama inayotolewa katika vyuo vya VETA ikionekana ya daraja la pili.

Anabainisha kuwa ushindani wa ufaulu umechangia baadhi ya walimu kujiingiza katika udanganyifu wa mitihani ili kuvutia wazazi na kujenga taswira ya shule zao.

“Wazazi wenye uwezo hawapeleki watoto wao katika shule zisizoonyesha ushindani mzuri wa ufaulu. Hali hii inachochea udanganyifu kwenye mitihani, jambo linalokiuka maadili ya ualimu na kuwanyima haki wanafunzi,” anasema Zaida aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Uwezo Tanzania.

Zaida anashauri kuwa maandalizi ya watoto kwa ajili ya soko la ajira yaanze katika hatua ya uandaaji wa mitalaa.

Anasema wataalamu wa elimu wanapaswa kushirikiana na waajiri tangu mwanzo ili kubaini mahitaji halisi ya soko na kuyaingiza katika mfumo wa elimu.

Kwa kufanya hivyo, elimu haitakuwa tu safari ya kutafuta alama, bali mchakato wa kumwandaa mtoto kuwa mbunifu, mwadilifu na mwenye mchango chanya katika uchumi na maendeleo ya Taifa.