Unguja. Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed amezindua majaribio ya ushushaji wa mizigo katika Bandari ya Mpigaduri.
Bandari hiyo inatajwa kuwa mwarobaini wa msongamano katika bandari ya Malindi ambayo imekuwa ikilalamikiwa kutokana na kuzidiwa, hivyo kufanya shughuli kuzorota.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Mpigaduri, Maruhubi, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja leo Machi 17, 2026, Dk Khalid ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya majaribio hayo huku akisema ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupunguza msongamano katika Bandari ya Malindi.
“Hatua ni nzuri inaridhisha, tumeona namna ambavyo inafanya kazi, Aprili mwaka huu ndiyo itaanza rasmi kazi ya ushushaji mizigo baada ya kukamilika kwa majaribio ya awali,” amesema.
Ameongeza kuwa uwepo wa bandari hiyo ya kisasa utasaidia kuongeza ufanisi katika sekta ya uchukuzi na biashara.
Amebainisha kuwa bandari ya Malindi kwa sasa imezidiwa na msongamano wa abiria na mizigo, hali inayosababisha ucheleweshaji wa huduma.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar, Akif Ali Khamis amesema bandari hiyo imejengwa na kampuni ya ZF Devco kwa kushirikiana na Serikali, ikiwa ni sehemu ya kuboresha miundombinu ya usafiri visiwani Zanzibar.
Ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri inayotumia zaidi ya Sh627 bilioni, unatajwa kuwa hatua muhimu katika kukuza uchumi na kuboresha huduma za usafiri wa baharini Zanzibar.
Kwa upande wake, Meneja wa Azam Marine, Ali Mohamed amesema bandari hiyo itasaidia kupunguza muda wa kushughulikia mizigo na kuongeza ufanisi.
