Beki Yanga ampa mtihani Camara, wakongwe watia neno

KIPA raia wa Guinea, Moussa Camara, anakabiliwa na mtihani mzito unaomuweka njiapanda ya kuendelea kuitumikia Simba ambapo hivi sasa ameondolewa kwenye mfumo wa usajili na mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.

Kuondolewa kwa Camara katika mfumo wa usajili, kunatokana na majeraha ya goti aliyoyapata na kumuweka nje kwa muda mrefu hali iliyofanya dirisha dogo Januari 2026 kusajiliwa Djibrilla Kassali.

Wakati Camara akibaki njiapanda ya kurejeshwa Simba au la, hadi sasa kwa wachezaji wa kigeni wa Simba na Yanga, ni Yao Kouassi Attohoula pekee, beki wa Yanga aliyeshinda mtihani wa viongozi wa klabu hizo na kurejea tena kikosini baada ya kukaa nje kwa muda mrefu akiuguza majeraha.

Simba na Yanga kuna maproo kadhaa ambao baada ya kupata majeraha makubwa, waliondolewa katika mfumo wa usajili na waliendelea kusalia katika klabu hizo wakisubiri wapone ili waweze kurejea kwa mara nyingine, lakini haikuwa hivyo, wakaishia kuondolewa moja kwa moja.

Yao aliyezaliwa Desemba 20, 1996 (umri wa miaka 29), alijiunga na Simba 14/07/2023. Baada ya kuumia msimu wa 2024-2025 aliondolewa katika mfumo wa usajili na baada ya kupona amerejeshwa kupitia dirisha dogo msimu huu 2025-2026, hivyo kumfanya kukaa nje kwa zaidi ya miezi minane.

Katika msimu wa 2023-2024, Yao alicheza mechi 25, alifanya faulo 18, hakuwa na kadi na alifunga bao moja. Kiwango chake kilikuwa cha juu kabla ya majeraha kumrejesha nyuma.

Mwingine ambaye aliwahi kuondolewa katika mfumo wa Yanga na aliendelea kusalia klabuni hapo ni Yacouba Songne, lakini hakufanikiwa mtihani wa kurejea tena kikosini. Kwa sasa mshambuliaji huyo anaichezea Mbeya City.

Mtihani huo kwa sasa unamkabili kipa wa Simba, Moussa Camara, ambaye baada ya kuumia akatafutwa mbadala Djibrilla Kassali ambaye kwa sasa ana clean sheets nne. Kiwango cha kipa huyo mwisho wa msimu kitaamua kama Camara atarejea kikosini ama kuaga jumla.

Camara alijiunga na Simba 01/08/2024 akitokea klabu ya Horoya AC ya Guinea na msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu alimaliza akiwa kinara wa clean sheets 19. Nyuma yake alikuwa Djigui Diarra wa Yanga aliyekuwa na 17 na katika ligi inayoendelea ana nane kabla ya jana kucheza na Azam.

Ujio wa Camara ndiyo uliyomuondoa kipa Ayoub Lakred aliyekuwa amewekwa pembeni baada ya kuumia. Ilikuwa akipona endapo kama mbadala wake asingeonyesha kiwango basi angeendelea kusalia kikosini.

Pia ilimkuta winga Muivory Coast, Aubin Kramo aliyesajiliwa na Simba Agosti 2023 akitokea ASEC Mimosas, lakini hakucheza mechi yoyote ya mashindano msimu mzima wa 2023-2024 kutokana na majeraha yaliyomuandama, baadaye kipindi cha dirisha dogo msimu huo, akatolewa kwenye mfumo wa usajili, ndiyo ikawa tiketi ya moja kwa moja kwani Agosti 2024 akatimkia Olympic Azzawiya ya Libya.

Katika hilo, mtazamo wa staa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, William Mtendawema alisema: “Jambo la kwanza linatokana na mtazamo wa mchezaji. Kwa Yao naamini alikuwa mvumilivu, alifanya bidii ya mazoezi ambayo kocha ama viongozi walishawishika kumbakiza, vinginevyo Simba na Yanga huchezi kwa sababu unahurumiwa.”

Aliongeza: “Anachotakiwa kufanya Camara kama amepona awe anafanya mazoezi kama vile anaanza kikosi cha kwanza hata kama anakaa pembeni. Hilo litampa changamoto huyo mbadala wake kuona akifanya mchezo anadondosha nafasi ya kuendelea kuwepo Simba. Kwa kufanya hivyo ni faida kwa klabu kuwa na ushindani kila idara.”

Mchezaji mwingine wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Emmanuel Gabriel alisema: “Kuwekwa kando ni jambo la kawaida kwani mpira wa miguu ni ushindani. Kikubwa kila mtu aonyeshe mapambano yake, atakayekuwa vizuri basi atafanikiwa kuendelea Simba.”