INADES YAZINDUA BWAWA LA KUNYWESHEA MIFUGO MIGORI IRINGA

Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

SHIRIKA la INADES-Formation Tanzania limezindua ujenzi wa bwawa la kunyweshea mifugo (water trough) katika Kijiji cha Migori, Wilaya ya Iringa, kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa maji salama na ya uhakika kwa punda na mifugo mingine midogo.

Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano na Brooke East Africa, kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa pamoja na jamii ya Kijiji cha Migori.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya eneo la mradi, Diwani wa Migori ambaye ndio alikuwa mgeni rasmi, Fatma Moge, ameipongeza hatua hiyo akisema itasaidia kupunguza vifo visivyo vya lazima vya punda na mifugo mingine, hasa wakati wa kiangazi.

Ameeleza kuwa kata hiyo, inayojumuisha vijiji vitano, hukumbwa na uhaba mkubwa wa maji na malisho wakati wa vipindi vya ukame. Hali hiyo husababisha mifugo kupelekwa umbali mrefu kutafuta malisho, ambapo mara nyingi maji hayapatikani kwa urahisi.

Fatma pia ameitaka mamlaka ya wilaya kuendelea kutafuta ushirikiano zaidi ili kupanua ujenzi wa mabwawa ya kunyweshea mifugo katika vijiji vingine vinavyokabiliwa na changamoto kama hizo.

Kwa upande wake, Afisa Mifugo wa Wilaya ya Iringa, Isidori Karia, ambaye pia ni mratibu wa mradi wa ustawi wa punda na uboreshaji wa maisha ya jamii, amesema mradi huo tayari umechangia kuboresha maisha ya wananchi kupitia utunzaji bora wa punda.

Amesisitiza kuwa bwawa hilo jipya litanufaisha si punda pekee bali pia mifugo mingine katika eneo hilo.

Naye Dkt. Charles Bukula, daktari wa mifugo kutoka INADES-Formation Tanzania, ameeleza kuwa Kijiji cha Migori kilichaguliwa kutokana na changamoto kubwa zinazowakabili mifugo wakati wa kiangazi pamoja na idadi kubwa ya mifugo iliyopo eneo hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wafugaji wa kijiji hicho, Sokoine Seketu, aliukaribisha mradi huo akisema umefika wakati muafaka na utasaidia si Migori pekee bali pia jamii za jirani.

Tangu mwaka 2019, INADES-Formation Tanzania imekuwa ikitekeleza mradi wa “Kusaidia maisha ya jamii kupitia uendelezaji wa ustawi wa punda” katika mikoa ya Singida, Iringa na Dodoma.

Mradi huo unalenga kuboresha maisha ya jamii, hasa makundi yaliyo hatarini yanayotegemea punda kwa kipato. Unajikita katika kuimarisha afya, uzalishaji na ustawi wa punda kupitia juhudi zinazoongozwa na jamii, ikiwemo matumizi sahihi ya vifaa vya kufungia (harness), huduma za mifugo, na elimu ya ufugaji bora.

Fatma Moge, Diwani wa Kata ya Migori (aliyevaa kofia), ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa hafla ya makabidhiano ya eneo la ujenzi wa bwawa la kunyweshea mifugo kijijini humo, akipatiwa maelezo kuhusu mradi huo.

Jamii ya Migori, inayoundwa kwa kiasi kikubwa na wafugaji, wakikusanya na kupeleka vifaa vya ujenzi katika eneo la mradi.