Mashambulizi mapya yamezuka katika vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati baada ya Iran kushambulia Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) leo Jumanne, hatua inayotafsiriwa kama kulipiza kisasi dhidi ya Marekani na washirika wake.
Mashambulizi hayo yanakuja wakati vita kati ya Iran na muungano wa Marekani na Israel ikiingia wiki ya tatu, huku zaidi ya watu 2,000 wakiripotiwa kupoteza maisha na hali ikiendelea kuwa tete bila dalili za kumalizika hivi karibuni.
Rais wa Marekani, Donald Trump amekiri kuwa mashambulizi hayo dhidi ya washirika wake wa ghuba hayakuwa yametarajiwa, ingawa vyanzo vya ndani vimedai kuwa kulikuwa na tahadhari kabla ya mapigano hayo kuanza.
Wakati huohuo, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani, Mlango wa Hormuz, imeendelea kufungwa hali inayochochea kupanda kwa bei za nishati na kuongeza hofu ya mfumuko wa bei duniani. Baadhi ya washirika wa Marekani wamekataa ombi la Trump la kushiriki katika operesheni ya kufungua njia hiyo.
Mashambulizi kati ya pande zote mbili hayajapungua, ambapo Iran ilirusha makombora kuelekea Israel usiku wa kuamkia leo, ikionyesha kuwa bado ina uwezo wa kufanya mashambulizi ya masafa marefu licha na mengine kutoka kwa Marekani na Israel.
Kwa upande wake, jeshi la Israel limesema linaendelea kulenga miundombinu ya serikali ya Iran ndani ya mji mkuu, Tehran, pamoja na maeneo ya kundi la Hezbollah katika mji wa Beirut. Jeshi hilo pia limedai kuwa limeandaa mipango ya kuendeleza vita kwa angalau wiki tatu zijazo.
Katika tukio jingine, makombora na ndege zisizo na rubani zilishambulia ubalozi wa Marekani mjini Baghdad, ambapo vyanzo vya usalama vya Iraq vimesema huo ulikuwa ni mashambulizi makali zaidi tangu vita hiyo ianze.
Hata hivyo, maofisa wa Marekani wamesema hakuna majeruhi walioripotiwa hadi sasa.
Hali inaendelea kuwa ya wasiwasi mkubwa katika ukanda huo huku jumuiya ya kimataifa ikionya juu ya athari za kiuchumi na kiusalama endapo vita hivyo vitaendelea kwa muda mrefu zaidi.
Vilevile, Rais wa Marekani, Donald Trump, ameendelea kuikosoa Serikali ya Uingereza kufuatia msimamo wake wa kutojihusisha moja kwa moja na vita vinavyoendelea dhidi ya Iran, akisema hatua hiyo inakatisha tamaa juhudi za kimataifa.
Kauli hiyo imekuja baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer kusisitiza kuwa nchi yake haitajiingiza katika vita licha ya kuendelea kushirikiana na washirika wake kutafuta suluhisho la pamoja.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumatatu, Trump amesema hafurahishwi na msimamo wa Uingereza, akiongeza kuwa taifa hilo lilipaswa kushiriki kwa nguvu katika juhudi za kufungua njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta ya Mlango wa Hormuz.
“Uingereza ilipaswa kuwa mstari wa mbele kwa hamasa kubwa. Kuna baadhi ya nchi zimenikatisha tamaa sana,” amesema Trump.
