Israel yadai kuwaua vigogo wengine wa Iran, Mojtaba asema…

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz amesema vikosi vya nchi hiyo vimemuua mkuu wa usalama wa Iran, Ali Larijani, anayechukuliwa kuwa mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa, pamoja na Gholamreza Soleimani, aliyekuwa akiongoza kikosi cha wanamgambo wa kujitolea cha Basij, ambacho kina mchango mkubwa katika usalama wa ndani.

Taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel imesema Benjamin Netanyahu ameamuru kuondolewa kwa viongozi waandamizi wa utawala wa Iran.

Hata hivyo, hakukuwa na majibu ya haraka kutoka Tehran kufuatia kauli za Katz. Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vilichapisha ujumbe wa mkono unaodaiwa kuandikwa na Larijani, ukikumbuka mabaharia wa Iran waliouawa katika shambulizi la Marekani, ambao mazishi yao yalitarajiwa kufanyika Jumanne.

Iwapo kifo chake kitathibitishwa, Larijani atakuwa kiongozi wa juu zaidi kuuawa tangu kifo cha kiongozi mkuu Ayatollah Khamenei aliyefariki siku ya kwanza ya mashambulizi ya anga ya Israel na Marekani Februari 28, 2026.

Mapigano hayakuonyesha dalili ya kupungua mapema leo Jumanne huku Iran ikirusha makombora kuelekea Israel usiku kucha, hatua inayodhihirisha kuwa nchi hiyo bado ina uwezo wa kufanya mashambulizi ya masafa marefu, licha ya kushambuliwa kwa zaidi ya wiki mbili na silaha za Marekani na Israel.

Jeshi la Iran pia limetoa taarifa likisema limelenga vituo vya teknolojia ya mtandao nchini Israel kwa kutumia droni, pamoja na vituo vya kutengeneza silaha vya kampuni ya Israel ya Rafael.

Jeshi la Israel limesema makumi ya ndege zake za kivita zimeshiriki katika mashambulizi ya pamoja yaliyofanyika katika miji ya Tehran, Shiraz na Tabriz nchini Iran na kufanikiwa kuwaua viongozi wawili wa kijeshi.

Mashambulizi hayo yamefanyika usiku wa jana Machi 16, 2026 ikiwa ni siku ya 18 tangu kuanza kwa mashambulizi hayo yanayotekelezwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran, yaliyosababisha kifo cha Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo, Ayatollah Ali Khamenei.

Israel imedai kuwa katika mji mkuu wa Tehran, mashambulizi yalilenga vituo vya uongozi wa vikosi vya usalama vya Iran, ikiwa ni pamoja na Wizara ya Ujasusi na kikosi cha wanamgambo cha Basij huku maeneo ya kuhifadhi na kurushia droni, makombora na mifumo ya ulinzi wa anga pia yakilengwa.

Katika mji wa Shiraz, makao makuu ya kamandi ya usalama wa ndani ya Iran pamoja na ghala la kuhifadhi makombora yalilengwa huku mifumo ya ulinzi ikiharibiwa katika mji wa Tabriz, kwa mujibu wa jeshi hilo.

Kwa mujibu wa Al Jazeera, mapema leo Machi 17, 2026, imesikika milipuko mikubwa katika maeneo mbalimbali ya Tehran. Mashambulizi hayo hayajaishia katika mji mkuu pekee, bali pia yameripotiwa katika miji mingine nchini humo, ikiwamo Ahvaz, Isfahan na Shiraz.

Duru zinaonyesha kuwa majengo muhimu yamelengwa katika mji mkuu huo pamoja na watu wawili muhimu ambao ni kamanda wa kikosi cha Basij cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Gholamreza Soleimani na katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, Ali Larijani.

Haya yote ni sehemu ya picha pana zaidi ambapo uongozi wa kisiasa wa Iran kuanzia wanajeshi hadi viongozi wa kisiasa unaonekana kuafikiana juu ya kuendelea kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi, mradi tu mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel yanaendelea.

Soleimani alizaliwa mwaka 1964, alijiunga na IRGC akiwa kijana na kupanda ngazi taratibu ndani ya taasisi hiyo.

Aliwahi kuhudumu kama kamanda wa kikosi wakati wa vita vya Iran na Iraq, na baadaye kuongoza vikosi kadhaa vya IRGC.

Tangu mwaka 2019, alikuwa mkuu wa kikosi cha Basij, jeshi la kujitolea la wanamgambo lenye takriban wanachama 450,000 chini ya IRGC na hivyo kuwa mmoja wa watu muhimu katika mfumo wa usalama wa ndani wa Iran.

Akiwa mtetezi mkubwa wa serikali ya Iran, Soleimani amewekewa vikwazo na nchi na mashirika kadhaa ya Magharibi, ikiwamo Marekani, Umoja wa Ulaya (EU), Uingereza na Canada.

Ali Larijani amekuwa akijulikana kwa miongo kadhaa kama kiongozi mwenye msimamo wa kati na wa vitendo ndani ya mfumo wa utawala wa Iran. Alikuwa katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na alisaidia kuongoza mkakati wa nchi hiyo katika vita dhidi ya Marekani na Israel.

Alizaliwa mwaka 1958 mjini Najaf, Iraq, katika familia yenye uwezo kutoka Amol. Larijani anatoka katika ukoo wenye ushawishi mkubwa ambao jarida la Time liliwahi kuufananisha na familia ya Kennedy wa Iran.

Baba yake alikuwa mwanazuoni mashuhuri wa dini, na akiwa na umri wa miaka 20 alimuoa Farideh Motahari, binti wa mshirika wa karibu wa mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ruhollah Khomeini.

Tofauti na wengi wa wanasiasa wenzake, Larijani alikuwa na elimu isiyo ya kidini, akihitimu masomo ya hisabati na sayansi ya kompyuta kabla ya kupata shahada ya uzamivu katika falsafa ya Magharibi, akijikita katika mawazo ya Immanuel Kant.

Baada ya mapinduzi ya mwaka 1979, alijiunga na IRGC kabla ya kuingia serikalini, akihudumu kama waziri wa utamaduni na baadaye mkuu wa shirika la utangazaji la taifa (IRIB).

Mwaka 2005, aliteuliwa kuwa katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na pia mkuu wa mazungumzo ya nyuklia ya Iran, kabla ya kujiuzulu mwaka 2007.

Aliingia bungeni mwaka 2008 na kuwa spika kwa vipindi vitatu mfululizo, akisimama kwenye nafasi muhimu katika kupitisha makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015.

Larijani alirejea tena katika nafasi ya katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa   Agosti 2025, na kujitokeza upya kama mmoja wa watu muhimu katika uongozi wa Iran.

Mojtaba akataa usuluhishi

Wakati huohuo, Kiongozi Mkuu mpya wa Iran amekataa mapendekezo ya kupunguza mvutano yaliyowasilishwa Iran kupitia wapatanishi, akisisitiza kuwa Israel na Marekani lazima kwanza wapige magoti, kwa mujibu wa ofisa mmoja mwandamizi wa Iran aliyenukuliwa na Reuters.

Ayatollah Mojtaba Khamenei alifanya kikao chake cha kwanza cha sera za nje tangu ateuliwe kuwa kiongozi mkuu, na alichukua msimamo mkali wa kulipiza kisasi dhidi ya Marekani na Israel ambao ulielezwa kuwa mkali zaidi na wa dhati, ofisa huyo alisema, bila kufafanua kama alihudhuria ana kwa ana au kwa njia ya mtandao.

Ofisa huyo mwandamizi, aliyeomba kutotajwa jina, amesema nchi mbili za upatanishi ziliwasilisha mapendekezo kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kuhusu kupunguza mvutano au kusitisha mapigano na Marekani. Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi kuhusu mapendekezo hayo wala nchi zilizohusika.

Kiongozi huyo mkuu alijibu kuwa sio wakati sahihi wa amani hadi Marekani na Israel wapige magoti, wakubali kushindwa, na walipe fidia.

Kiongozi mkuu ndiye mwenye uamuzi wa mwisho katika masuala yote ya taifa ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hadi sasa, hakuna picha yake mpya iliyotolewa tangu alipochaguliwa zaidi ya wiki moja iliyopita na baraza la wanazuoni wa dini kumrithi baba yake, Ayatollah Ali Khamenei.