Jesca Magufuli: Nyumbani alikuwa baba wa nidhamu, kwa Taifa alikuwa kiongozi wa dhamira

Miaka mitano tangu kifo cha Rais wa awamu ya tano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, familia yake imeendelea kumkumbuka si tu kama kiongozi wa Taifa bali pia baba mwenye mafunzo makubwa ya maisha.

Akizungumza katika kumbukumbu ya miaka mitano ya kifo cha baba yake (Magufuli), Jesca Magufuli amesema kwa familia yao siku hiyo hubeba hisia nyingi kwa sababu wanamkumbuka mtu ambaye kwao alikuwa zaidi ya kiongozi maarufu aliyefahamika na Watanzania.

 “Kwa familia leo ni siku yenye hisia tofauti kwetu, tunamkumbuka baba, babu, kaka na mjomba ambaye upendo wake kwetu haukuwa na maneno mengi bali vitendo zaidi,” amesema Jesca ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu.

Jesca amesema kwa Watanzania wengi baba yake alifahamika kama Rais, waziri, mbunge na mshauri wa Taifa, lakini nyumbani alikuwa mtu wa nidhamu, unyenyekevu na mwenye imani thabiti kwa Mungu.

Amesema mara nyingi aliwasisitiza watoto wake kwamba mafanikio hayawezi kupatikana bila kufanya kazi kwa bidii, akiwataka kuthamini juhudi katika kila walichokifanya.

“Alituasa mara nyingi kwamba kama unataka heshima katika maisha fanya kazi, kama unataka nchi yako iendelee fanya kazi,” amesema.

Amesema ujumbe huo baadaye ulijulikana kwa Watanzania wote kupitia kauli maarufu ya “Hapa Kazi Tu”, ambayo amesema haikuwa kaulimbiu ya kisiasa pekee bali ilikuwa falsafa ya maisha ya baba yao.

Amesema hata alipokuwa Rais, Magufuli aliendelea kuishi kwa nidhamu ileile aliyojijengea tangu alipokuwa mwalimu na mtumishi wa umma, akiamini katika kuamka mapema, kufanya kazi kwa bidii na kutarajia uwajibikaji kwa kila aliyekabidhiwa jukumu la kulitumikia Taifa.

Jesca amesema kwa baba yake Tanzania haikuwa tu eneo la kijiografia bali ilikuwa dhamana ya kizazi kilichopo na kile kijacho, hivyo aliamini kila Mtanzania ana wajibu wa kuilinda na kuijenga nchi.

Amesema moja ya mafunzo makubwa aliyowapatia watoto wake ni unyenyekevu, akieleza kuwa licha ya nafasi aliyokuwa nayo hakuwahi kujitenga na wananchi wa kawaida.

“Aliwasikiliza wakulima, walimu, wafanyakazi, vijana na watu wenye mahitaji maalumu. Aliamini uongozi wa kweli ni ule unaosikiliza na kuchukua hatua,” amesema.

Mbunge huyo ameeleza imani hiyo ndiyo iliyosababisha sera nyingi alizosimamia zililenga moja kwa moja kuboresha maisha ya wananchi wa kawaida.

Amesema Magufuli pia aliamini Tanzania inapaswa kusimama kwa nguvu zake, huku akisisitiza kuwa rasilimali za Taifa lazima ziwanufaishe wananchi wake na miundombinu iwe chachu ya kufungua fursa mpya za uchumi.

Jesca amesema baba yake alisisitiza umuhimu wa elimu, akiamini kuwa ndiyo chombo kikubwa cha kuleta usawa katika jamii.

“Mara nyingi alikuwa akisema bila elimu kijana wa kawaida kutoka Chato asingepata nafasi ya kuiongoza Tanzania,” amesema.

Ameongeza kuwa alipokuwa akizungumzia maendeleo, Magufuli hakuzungumzia nadharia bali maisha halisi ya wananchi kama mkulima anayehitaji barabara kufikisha mazao sokoni, mwanafunzi anayehitaji darasa na familia inayohitaji huduma za maji na umeme.

Jesca amesema baba yake pia alikuwa na maono makubwa kuhusu Afrika, akiamini bara hilo lina rasilimali, akili na nguvu ya kujijenga lenyewe.

“Nakumbuka siku moja alisema changamoto ya Afrika si ukosefu wa rasilimali bali ni kutojiamini katika uwezo wetu,” amesema.

Amesema Magufuli aliwahimiza Watanzania kujivunia Taifa lao na Waafrika kujiamini katika uwezo wao, akiamini maendeleo ya kweli ya Afrika yataanza pale bara hilo litakapojiamini.

Hata hivyo, Jesca amesema kwa familia kumpoteza baba yao lilikuwa pigo kubwa, lakini katika miaka mitano iliyopita wamefarijika kusikia simulizi nyingi nzuri kutoka kwa Watanzania kuhusu maisha na mchango wa kiongozi huyo.