Kamati ya Bunge yaonya uhaba wa wataalamu wa afya, vituo vya umahiri

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiendelea kujikita katika kuimarisha umahiri wa sekta ya afya, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeonya juu ya uwepo wa upungufu mkubwa wa watumishi wa afya nchini.

Kutokana na hali hiyo, kamati hiyo imeitaka Serikali kuchukua hatua za haraka na stahiki kukabiliana na changamoto hiyo ili uwekezaji unaofanywa katika miundombinu ya afya Katika Kituo Cha Umahiri wa Afya Mloganzila, kilichopo chini ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) uweze kuleta matokeo chanya.

Kauli hiyo imetolewa Machi 17,2026 Dar es Salaam na  Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga, Husna Sekiboko, baada ya kamati hiyo kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Tiba katika Kampasi ya Mloganzila chini ya Chuo cha MUHAS.

“Haitapendeza kuona tunajenga majengo mazuri kisha yanabaki bila wataalamu wa kutoa huduma. Ni muhimu Serikali ihakikishe majengo haya yanakuwa na wataalamu wa kutosha,” amesema Sekiboko.

Aidha, ameagiza kuwa barabara za ndani ya kituo hicho zijumuishwe katika bajeti ya mwaka 2026/2027 ili kuboresha mwonekano wake na kuendana na hadhi ya miundombinu iliyopo.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Afrika Mashariki kinachojikita katika magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, kilicho chini ya MUHAS, umekamilika.

Amesema Serikali tayari imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali itakayounganishwa na kituo hicho, hatua itakayokifanya kuwa miongoni mwa vituo bora zaidi katika masuala ya sayansi, tiba na magonjwa ya damu.

“Hospitali hii itakuwa na utofauti kwani wataalamu wake watatoa huduma za tiba, kufanya tafiti pamoja na kutoa elimu,” amesema Profesa Mkenda.

Ameongeza kuwa mkakati wa kuanzisha kituo cha umahiri katika huduma za meno umekamilika, ambapo kituo hicho kitajihusisha na tafiti, utoaji wa huduma za meno na mafunzo kwa wataalamu.

“Lengo la hapa Mloganzila ni kuwa na vituo vingi vya umahiri, tutakuwa pia na kituo cha umahiri wa saratani kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), ambacho kitajikita katika elimu, tafiti na tiba, tofauti na hospitali nyingi zinazotoa matibabu pekee,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET) kutoka Chuo cha Muhas, Profesa Nathanael Siriri, amesema mradi huo unalenga kuimarisha uwezo wa vyuo vikuu kuzalisha wataalamu wengi na bora zaidi watakaochangia maendeleo ya uchumi.

Amesema kupitia mradi huo, watumishi 33 wamewezeshwa kusoma katika ngazi za uzamili na uzamivu, ambapo tisa wanasoma ndani ya nchi na 24 nje ya nchi. Kati yao, 20 wanasoma uzamili na 12 tayari wamehitimu.

Profesa Siriri amesema mradi huo pia unalenga kuboresha ubora wa mafunzo ya wataalamu wa afya na kuongeza uwezo wa vyuo kupokea wanafunzi wengi zaidi, hatua itakayosaidia kupunguza uhaba wa watumishi wa afya nchini.

Kwa sasa, inakadiriwa kuwa kuna upungufu wa takribani asilimia 55 ya watumishi wa afya, ambapo mahitaji ni watumishi 391,950 huku waliopo wakiwa 177,711 pekee.

Amesisitiza kuwa pamoja na kuongeza wataalamu, mradi huo pia utaimarisha tafiti za afya na kuboresha huduma za afya kwa ujumla nchini.