KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA MRADI WA HEET KUFIKIA 70% MUHAS

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeridhishwa na maendeleo ya mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ambao umefikia asilimia 70.

Akizungumza leo wakati wa ziara ya kutembelea Kampasi ya Mlonganzila, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Husna Sekiboko alisema lengo la mradi huo ni kuongeza miundombinu na upanuzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kiweze kukua kama inavyotarajiwa.

Sekiboko alisema utekelezaji wa mradi wa HEET umepita matarajio yaliyopangwa katika mkataba kwani kuna maeneo utekelezaji umefikia asilimia 70 hadi 80.

“Mradi huu utaleta tija kwa Taifa kwani udahili utaongezeka, maeneo ya kujifunzia yataongezeka kwani bado kuna hekari nyingi,” alisema

Aliongeza kuwa kutokana na ongezeko la watu, uwiano kati ya daktari na mgonjwa uko chini hivyo wakipanua vyuo vinavyohusika na kuandaa madaktari ili kupunguza uhaba wa madaktari na kuwa na nafasi nzuri ya kutoa huduma bora.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano nzuri na Benki ya Dunia kwani imeweka katika mradi huu zaidi ya Shilingi bilioni 115 ambazo zinafanya upanuzi wa kampasi hii na maana yake ana makusudi ya kuongeza tija katika sekta ya afya,” alieleza

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema eneo la Mlonganzila litakuwa eneo maalum la tiba kwani wanatarajia kujenga Hospitali maalum kwa ajili ya tafiti, kujifunzia na kufundishia za tiba ya kinywa na meno, magonjwa ya moyo na saratani.

Alisema wanaenda kuwa kituo cha umahiri Afrika Mashariki ambapo watachochea utalii tiba kwa kupokea wagonjwa kutoka nje ya nchi pamoja na wanafunzi watakaosomea ubobezi na umahiri katika fani mbalimbali kutoka nchi za nje.

Kaimu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Balandya alisema jinsi wanavyoongeza kampasi wanavutia wawekezaji wa kutengeneza viwanda vya dawa.

“Mradi utakuwa na tija kwani kwa sasa wanaoomba kozi ya udaktari ni 5,400 na wote wanavigezo lakini wanaowachukua ni 230 pekee hivyo wanawaacha wengine,” alisema.

Aliongeza “Wataalamu wanawatengeneza wenyewe Kwa mujibu wa vigezo vya Taasisi Vyuo Vikuu (TCU) wanaelekeza uwiano kati ya wanafunzi na walimu ni wanafunzi 10 kwa mwalimu moja na chuo hicho uwiano ni 11:1 hivyo wakiongeza udahili wanahitaji kuongeza walimu.”