WAKATI Pamba Jiji ikijipanga kuipokea Simba SC, kocha wa kikosi hicho, Francis Baraza amesema kazi kubwa waliyonayo ni kuwashika wekundu hao pabaya.
Mechi hiyo itakayochezwa Machi 19, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Baraza alisema eneo lenye nguvu zaidi kwa Simba ni kiungo, hivyo watadili nalo kuhakikisha wanapata ushindi kirahisi wakiwa nyumbani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Baraza alisema kuelekea mechi dhidi ya Simba ambayo itakuwa ya mwisho kwa mwezi huu wa Machi, maandalizi bado yanaendelea.
Alisema faida ya kwanza waliyonayo ni kucheza mechi kubwa kama hiyo wakiwa nyumbani, uwanja ambao wanaufahamu vizuri.
“Katika mechi hii maandalizi ni mazuri na lipo eneo ambalo tutalifanyia kazi kubwa ili kuhakikisha tunatoka na pointi tatu nyumbani.
“Timu yetu ikifanikiwa kuwatuliza eneo moja la Simba ambalo ni viungo, basi mechi hii inaweza kuwa upande wetu na haitakuwa na ugumu sana,” alisema Baraza.
Kocha huyo raia wa Kenya, aliongeza kuwa: “Simba nguvu yao kubwa ipo eneo la kiungo ambao ndiyo wamekuwa wafungaji wa mabao ya timu hiyo, lakini tunajipanga kwa ugumu kwenye mchezo huo. Tunajua namna ya kupata ushindi kwa kutumia makosa ya wapinzani wetu.”
Pamba ambayo imecheza mechi 15 za Ligi Kuu Bara msimu huu, imeshinda sita, sare sita na kupoteza mitatu, ina pointi 24, ikiwa nafasi ya tano katika msimamo wa ligi. Kwa msimu huu, hii ni mara ya kwanza timu hizi kukutana, lakini mechi ya mwisho Simba ilipocheza nyumbani kwa Pamba ilipata ushindi wa bao 1-0, msimu uliopita. Pia Pamba haikupata ushindi ugenini ikichapwa 5-1 na Simba.