Dar es Salaam. Miaka mitano tangu kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, John Pombe Magufuli, kumbukumbu zake zinaendelea kugusa mioyo ya wengi, huku viongozi waliowahi kufanya kazi naye wakikumbuka uongozi wake uliotawaliwa na uchapakazi, uzalendo na msimamo mkali dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.
Akizungumza wakati wa kumbukumbu ya miaka mitano ya kifo cha kiongozi huyo, Waziri Mkuu mstaafu Kassim Majaliwa amesema Magufuli alikuwa kiongozi aliyethamini uwajibikaji, uadilifu na matokeo ya kazi, sifa ambazo zilijenga taswira yake kama mtumishi wa wananchi.
Magufuli alifariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam, kwa maradhi ya moyo ya muda mrefu.
Wakati huo, Kassim Majaliwa alikuwa akihudumu kama Waziri Mkuu wa Tanzania kabla ya kustaafu mwaka jana. Kufuatia tukio hilo kwa mujibu wa Katiba, Machi 19,2021 aliyekuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Leo hii tupo hapa kwenye kumbukizi hii, hatuwezi kujitenga na sifa hizi kwa Magufuli. Alikuwa mchapakazi, alikuwa za ndani ya darasa lakini hata nje katika kutekeleza majukumu yake, alikuwa ni kiongozi mzalendo,” amesema Majaliwa.
Amesema uzalendo wa Magufuli ulijengwa juu ya misingi ya uwajibikaji, uaminifu na dhamira ya kuona Taifa linapiga hatua za maendeleo.
Majaliwa ameeleza kuwa hayati Magufuli alikuwa mtu mkweli na mwenye msimamo mkali katika kusimamia maadili ya uongozi, akiwakemea vikali wale waliokuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa na ubadhirifu.
“Hayati alikuwa ni mtu mkweli, lakini pia alikuwa hana mzaha katika mambo yake na ni mkali. Alikemea maovu, wezi, wala rushwa na wabadhirifu wa mali za umma. Yeyote ambaye hakufuata misingi hii aliachana naye, huo ndio ulikuwa utaratibu wake,” amesema.
Majaliwa amesema wale waliokuwa karibu na Magufuli walipata nafasi ya kushuhudia na kujifunza busara na hekima zake katika kuongoza Taifa.
Ameongeza kuwa kiongozi huyo alikuwa na uwezo mkubwa wa kutambua na kusimamia rasilimali za nchi kwa manufaa ya wananchi, hususan makundi ya wanyonge.
“Leo pia tunamkumbuka Magufuli sisi tuliokuwa karibu naye tuliweza kushuhudia na kunufaika na busara zake na hekima zake katika kuongoza Taifa hili, na hasa kutambua rasilimali za nchi na wananchi wenyewe na wanyonge wakiwemo,” amesema.
Majaliwa amesema mbali na kuwa rais, Magufuli alikuwa pia mwalimu kwa viongozi waliokuwa wakifanya kazi naye, jambo lililowawezesha kupata uzoefu na mafunzo ya uongozi.
Amesema mafunzo hayo yameendelea kuonekana hata baada ya kifo chake, ambapo miradi mingi ya kimkakati aliyoianzisha imeendelea kutekelezwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
“Magufuli alikuwa pia mwalimu. Tuliyekuwa naye jirani kwa kipindi kirefu tulijifunza mengi kutoka kwake katika kipindi chake. Na hii ndiyo iliyopelekea hata alipotangulia mbele ya haki na Samia kuingia madarakani aliweza kutekeleza miradi yote ya kimkakati iliyoachwa na marehemu,” amesema.
Majaliwa amesema licha ya Watanzania kuhisi kumpoteza kiongozi huyo, mchango wake utaendelea kukumbukwa kwa muda mrefu.
“Leo tukiwa hapa tunatambua kwamba Watanzania tunajiona kama tumempoteza, lakini ukweli ni kwamba bado tuko naye, yupo kwenye mioyo yetu,” amesema.