Meli kubwa nne za mizigo zitakavyoifungua Tanzania kiuchumi

Katavi. Ujenzi wa meli kubwa nne za mizigo katika Bandari ya Karema umefikia zaidi ya asilimia 95, huku fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi wa mikoa inayopitiwa na Ziwa Tanganyika na kuongeza kipato cha kaya na Taifa zikibainishwa.

Kati ya meli hizo ambazo zitakuwa zikifanya safari zake nchi za Congo, Zambia, Burundi na Tanzania mbili zimekamilika, moja inasubiri kibali cha Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac).

Wakati meli hizo tatu zikiwa hatua hiyo, nyingine ya nne jana Jumatatu, Machi 16, 2026 imeshushwa majini kwa mara ya kwanza ikisubiri mchakato wa kupata kibali.

Ujenzi wa meli hizo ulianza Aprili 2025 na ukitarajiwa kukamilika Julai 2026.

Msimamizi Msaidizi wa Bandari ya Karema kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Anthony Poyo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu meli nne kubwa za mizigo zilizojengwa bandarini hapo.

Oktoba 2023, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ilipokea maombi kutoka Kampuni ya Gold Voyage Logistics Limited, kampuni tanzu ya Zijin Mining Group Co. Ltd kutoka China, ikiomba kukodishwa eneo katika Bandari ya Karema ili kujenga meli hizo.

Msimamizi Msaidizi wa Bandari ya Karema, Anthony Poyo amesema kukamilika kwa meli hizo kubwa kutaimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani kama Congo, Burundi na Zambia.

Amebainisha manufaa ya meli hizo ni kuwa kichocheo cha usafirishaji wa madini kama ya lithium, shaba na dhahabu kutoka eneo la Manono nchini DRC, yanayochimbwa na kampuni hiyo ambapo kupitia Manono, Bandari ya Kalemie hadi Kigoma, Dar es Salaam na Tanga zitatumika kabla ya kusafirisha Kwenda nje ya nchi.

Meli ya nne iliyojengwa Bandari ya Karema, Mkoa wa Katavi ikishushwa majini kwa mara ya kwanza baada ya ujenzi wake kukamilika.

Poyo amesema kupitia meli hizo, wakulima nao watanufaika kwa mazao ya kilimo pamoja na ajira kwa Watanzania hususan mabaharia ambapo kila meli moja inahitaji si chini ya mabaharia 15.

Aidha, shughuli za usafirishaji, upakiaji wa mizigo, huduma bandarini pamoja na biashara ndogondogo zitakazozunguka bandari hiyo zitapiga hatua kubwa.

“Ujenzi wa meli hizi umetokana na Serikali kufungua fursa ya uwekezaji. Umeleta fursa kwa vijana, wananchi wa Karema na maeneo jirani na hii imekuwa mlango wa kiuchumi kwa Taifa letu na wananchi mmojammoja,” amesema Poyo.

“Hivi sasa tuna reli ya SGR, wamiliki wa malori watanufaika kwa kuchukua mizigo katika bandari hii. Na kuongeza shehena ya mizigo tunayohudumia,” amesema.

Amesema kwa sasa wamehudumia zaidi ya tani 10,000 za mizigo katika bandari hiyo ambayo imeboreshwa na kuwa ya kisasa yenye uwepo wa kupokea meli yenye urefu wa mita 150.

Kuhusu wakulima na wafanyabiashara, Poyo amesema utarahisisha usafirishaji wa mazao kwenda katika masoko makubwa ya kikanda na kimataifa, kuongeza thamani ya mazao, kupanua masoko na kuongeza kipato cha wananchi wa Mkoa wa Katavi na maeneo jirani kama ya Kigoma na Rukwa.

Wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), wawakilishi wa Kampuni ya Gold Voyage Logistics Limited, kampuni tanzu ya Zijin Mining Group Co. Ltd na watumishi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) wakishuhudia meli ikishushwa majini.

Mei 12, 2025, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile alifanya ziara Karema kujionea ujenzi wa meli hizo akisema kuwa zitainufaisha zaidi Tanzania, kwani usafirishaji wa shehena ya mizigo kutoka Bandari ya Kigoma unategemea kutumia miundombinu ya reli zilizopo za MGR na SGR hadi Bandari ya Dar es Salaam na Tanga.

“Sisi ndio tumeunganishwa na bahari, unaweza kuona tupo kwenye eneo la mkakati. Hii kampuni inayojenga hizi meli inachimba madini mbalimbali DRC na hii kwetu ni fursa kwani watayapitisha Kwenda nje ya nchi kupitia kwetu,” amesema Kihenzile.

Alisema kazi kubwa ambayo Serikali inaifanya ni kuhakikisha inaboresha bandari zake, miundombinu ya reli ya kati na ile ya kisasa (SGR) na jengo la abiria kwenye Uwanja wa Ndege Kigoma ili sekta ya usafirishaji iwe bora na isiwe kikwazo kwa wananchi na wawekezaji.

Kihenzile alisema reli ya kati kutoka Tabora – Mpanda hadi Karema ikikamilika itarahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini hapo hadi Dar es Salaam, na malengo ya Serikali SGR itasambaa nchini na hiyo ndiyo dhamira ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Meneja Rasilimali Watu kutoka Kampuni ya Ankola Shipyard Co. Ltd ambao ndiyo waliounda meli hizo, Mohammed Mohamed Chande amesema mradi huo ulianza April 2025 na unatarajia kukamilika Julai 2026,huku kwa sasa meli zote zimeshashushwa majini.

“Mradi umekuja kufungua njia na mlango wa kiuchumi Ziwa Tanganyika. Tunashukuru kwa ushirikiano ambao tuliupata kutoka serikalini na TPA hadi kutuwezesha kumaliza kwa wakati,” amesema.

Amesema fursa za ajira kwa vijana zimepatikana tangu mradi ulipoanza kwani wengi wamepata ujuzi na kuwa na manufaa kwa Taifa,” amesema Chande.

Kuhusu changamoto, Chande amesema wakati wa utekelezaji walikumbana na mabadiliko ya hali ya hewa, hata hivyo walifanikiwa kukabiliana nayo.

Baadhi ya wananchi wamepongeza hatua hiyo ya kukamilika kwa ujenzi wa meli hizo kwani shughuli zao za kilimo, uvuvi na mifugo huenda zikapata masoko ya ndani na nje, kwani usafirisaji utakuwepo.

Mkazi wa Karema, Augustino Heneriko amesema wanaishukuru Serikali kwa kuweka mazingira ya uwekezaji hali ambayo inawafanya kuwa na matumaini ya kufungua fursa za kiuchumi kwao wenyewe na nchi.