Mwamuzi: Ile ya Dube ni penalti, Bacca alistahili nyakundu

MATOKEO ya 0-0 katika Dar es Salaam Derby kati ya Azam dhidi ya Yanga, mechi iliyochezwa Jumapili Machi 15, 2026, imeiacha na gumzo kubwa kufuatia tukio la dakika ya 90+2 ambapo mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube kuangushwa eneo la hatari na beki wa Azam, Fuentes Mendoza, kisha mwamuzi Ally Mnyupe kusema hakuna penalti.

Mbali na hilo, matukio kadhaa ya faulo yaliyofanywa na wachezaji akiwamo beki wa Yanga, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, mwamuzi huyo hakutoa adhabu ya kadi ingawa ilionekana ilistahili kwa mchezaji husika kuadhibiwa.

Hali hiyo imewaibua wataalamu na kuyachambua matukio kadhaa ya mechi hiyo, ambapo mwamuzi wa zamani, Abdallah Kambuzi kusema: “Ile ya Dube ni penalti.”

Kauli ya Kambuzi iliungwa mkono na Mwenyekiti wa zamani wa waamuzi nchini, Nassor Said ambaye alipozungumza na Mwanaspoti alisema alichokigundua kwa Mnyupe ni uoga wa kuamua matukio ikiwamo hilo la penalti na kadi nyekundu aliyotakiwa kuonyeshwa Bacca.

Aliifafanua kauli yake ya kwa nini ilitakiwa iwe penalti akisema ni kutokana na Mendoza kumzuia Dube ndani ya boksi wakati anaenda kufunga, kisheria ni makosa na ilitakiwa ipulizwe filimbi ya kuweka mpira eneo la penalti.

“Kwa lugha ya waamuzi refa alikuwa na uoga wa kuamua matukio, pengine aliona limetokea dakika za mwishoni, ila kisheria penalti inatakiwa itolewe muda wowote linapotokea tukio hata zingebaki sekunde tano, mweye haki apewe haki anayostahili ili kuendelea kulinda heshima ya mpira wa miguu nchini,” alisema Said na kuongeza:

“Ili mwamuzi uheshimike ni kufanya maamuzi magumu bila kujali presha ya mashabiki itakuwaje, kwani mbali na penalti hiyo ya wazi pia Bacca alifanya makosa mengi yaliyostahili apewe kadi nyekundu kwa lengo la kulinda nidhamu uwanjani na kuwafanya wachezaji wengine wasione ni kawaida kucheza mpira usiokuwa wa kiungwana, hivyo ushauri wangu waamuzi wasimamie sheria bila kujali nani atasema nini,” alisema.

Kuhusu tukio la Dube na Mendoza, Kambuzi alisema Mnyupe alikuwa katika muono mzuri, ambapo Dube alikuwa anapambana kwenda kufunga, lakini akakutana na beki aliyeinua mguu kumzuia asipite.

“Katika uamuzi kuna lugha inaitwa mwamuzi hatakiwi kukaa zaidi ya yadi 10 ingawa Mnyupe alikuwa zaidi ya 10, lakini macho yake yalikuwa katika tukio mpira ulipotoka hadi beki kumzuia Dube, kwa kipande hicho binafsi nimeona ni penalti ya wazi, ni hivyo tu siwezi kuzungumza sana,” alisema Kambuzi.

Kwa upande wa staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella, alisema: “Sisi wengine mashabiki hatutakiwi kuingilia wasimamizi wa sheria wanaokuwa wamepewa dhamana ya kuchezesha mechi, kwani hao ndiyo waamuzi wa mwisho wa mchezo.” Kocha wa zamani wa Standa United, Athuman Bilal ‘Bilo’ ambaye kwa sasa anamiliki kituo cha soka kinachofundisha wavulana na wasichana kilichopo jijini Mwanza, alisema: “Labda nizungumze kwa kifupi, tukio limeshatokea, mwamuzi kasema siyo penalti, hata nikisema penalti nini kitabadilika ama kutokea.”

Bilo anayeinoa timu ya Mapinduzi FC inayoshiriki First League huku akimiliki timu ya wanawake ya Bilo Queens inayocheza Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (TWPL), aliongeza: “Katika kozi zetu za ukocha tunafundishwa tukio likitokea katika shimo linapaswa kuamuliwa kulingana na sheria zake, ukisema uwasahihishe utaonekana unaingilia eneo siyo lako, kwa maana ya sisi tunatakiwa kujikita na ufundi, hivyo kwa lugha nyepesi wajisahihishe maana hata TFF imekuwa ikiwafungia mara kadhaa, ila unaona mambo ni yale yale.”