Morogoro. Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema Serikali inaendelea kushughulikia changamoto za miundombinu zinazokwamisha usambazaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia, hasa vijijini na pembezoni mwa miji.
Akizungumza leo Machi 17, 2026 mkoani Morogoro wakati wa kufungua kongamano la wadau wa nishati safi ya kupikia lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati, amesema Serikali inatambua umuhimu wa kushirikiana na sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kutatua changamoto hizo.
Ameeleza kuwa jitihada zinaendelea kuvutia uwekezaji katika sekta hiyo, zikiwemo ruzuku kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ambapo mitungi ya gesi na majiko banifu yanasambazwa kwa bei nafuu hadi vijijini.
Waziri wa nishati Deogratius Ndejembi (katikati) akipokea maelekezo kutoka kwa Mathias Imani wa kampuni ya Matima Investment. Ndejembi amekagua majiko hayo kabla ya kuzindua kongamano la wadau wa nishati safi ya kupikia lililofanyika mkoani Morogoro. Picha Hamida Shariff
Aidha, amekumbusha kuwa Mei 2024, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua mkakati wa Taifa wa miaka 10 unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034. Amesema hatua hiyo inalenga kuboresha maisha, kulinda mazingira na kupunguza ukataji wa miti kwa matumizi ya kuni na mkaa.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo amesema kongamano hilo linalenga kuharakisha matumizi ya nishati safi ili kupunguza athari za kiafya, kulinda mazingira na kuchochea uchumi. Ameongeza kuwa Tanzania ina fursa ya kunufaika na biashara ya kaboni kupitia miradi ya majiko banifu na teknolojia nyingine rafiki kwa mazingira.
Afisa masoko kutoka kampuni ya Envotec akionesha majiko yanayosambazwa na kampuni hiyo ambayo yanatumika kwenye shule, hospitali, magereza na taasisi nyingine za umma zinazotoa huduma za chakula. Picha na Hamida Shariff
Naye Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay amewataka wadau kuhamasisha vijana kutumia fursa za kiuchumi katika sekta hiyo, ikiwemo uzalishaji wa mkaa mbadala na teknolojia za kupikia.
Baadhi ya wadau wamesema changamoto kubwa ni uelewa mdogo wa jamii na mitazamo potofu kuhusu nishati safi. Mathias Imani kutoka Matima Investment amesema majiko ya gesi yanaweza kupunguza gharama hadi asilimia 45 na kutoa matokeo bora zaidi, akiiomba Serikali kusaidia wabunifu kupata masoko ili teknolojia hizo zisambae zaidi nchini.
