Dar es Salaam. Gharama za maisha zinapoongezeka, mara nyingi kila mtu huangalia namna ya kukabiliana nazo, ikiwamo kutafuta kipato cha ziada ili kupata uhuru wa kuishi.
Hali hiyo huwafanya wengi kufikiria nje ya boksi na kuangalia kitu gani kinachoweza kufanyika kwa urahisi bila kuathiri shughuli zao za kila siku, na hapo ndipo kila mtu huja na wazo la biashara kulingana na sehemu aliyopo.
Anitha Edward (26) ni kati ya watu hao ambao sasa wanaona matunda ya uthubutu na uamuzi aliowahi kuufanya akiwa chuoni.
Akiwa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Ustawi wa Jamii, akichukua shahada ya ustawi wa jamii na saikolojia, anakiri kuwa kiwango cha fedha alichokuwa akikipata kutoka nyumbani kilishindwa kukidhi mahitaji yake, wakati alipenda kuwa na muonekano mzuri, jambo lililohitaji fedha nyingi.
“Unajua unaweza kupiga simu nyumbani kuomba hela ya kusuka, ukatumiwa labda Sh25,000 ambayo haitoshi, labda unataka kusuka nywele za Sh60,000, hii ndiyo ilinifanya nijiulize nifanye nini ili niweze kutoka huku,” anasema.
Baada ya kufikiria kwa muda, wazo moja rahisi lakini lenye matumaini lilimjia akilini— kutengeneza juisi na kuuza, akiwa mwaka wa kwanza chuoni hapo.
Hata hivyo, anasema malengo hayo yalishindwa kufanikishwa kutokana na mtaji mdogo. Alihitaji Sh500,000 ili kuanza biashara, lakini kila alipokuwa akiweka akiba alishindwa kufikia malengo.
Anitha anasema kila alipojaribu kukusanya fedha, shida nyingine ziliibuka, na baadaye alitumia akiba hiyo kutatua changamoto zilizoikabili, jambo lililofanya aendelee kusubiri kila wakati.
Anasema siku aliyoamua kuanza na alichokuwa nacho, alitumia Sh30,000 kununua matunda na vifungashio, huku akitumia blenda ya mwenye nyumba aliyekuwa akiishi, kuanzia safari yake ya ujasiriamali.
Kupitia fedha hiyo, anasema alikwenda katika soko la Mabibo akitafuta matunda kwa bei ya jumla, ambayo hayakuwa mengi, lakini yalimsaidia kupata juisi ambayo aliiuza na kupata faida ya kuendelea na biashara hiyo kama alivyopanga.
“Nilianza kuuza juisi hizo kwa wanafunzi wenzangu na watu waliokuwa karibu na chuo. Kila nikiuza juisi, nilikuwa nampiga picha mteja na kuchapisha katika mitandao yangu ya kijamii ya WhatsApp, Instagram na TikTok, kumbe watu wakawa wanapenda, taratibu wateja wakaanza kuongezeka, nikaona kumbe hili linawezekana,” anasema.
Anasema wateja wakubwa mwanzoni walikuwa wanafunzi wa chuo alichokuwa akisoma, mara zote alikuwa akitembea na biashara yake kila alipokwenda katika vipindi hadi alipomaliza chuo.
“Baada ya miezi miwili ya mwanzo ya kufanya biashara hii, nikaona matokeo makubwa, nikaona nitafute eneo, nikaanza kupambana kupata eneo karibu na sehemu niliyokuwa naishi ambayo ni Mwenge na Sinza, lakini gharama ilikuwa kubwa, mwisho wa siku nilipata kontena,” anasema.
Anasema alipata kontena, alikaa miezi mitatu bila kufungua akijiuliza ikiwa anastahili kufanya biashara hiyo wakati amebakiza miezi michache kumaliza shahada yake ya ustawi wa jamii na saikolojia.
“Niliwaza sana, nikasema, yaani nimesoma nimemaliza ili nije kuuza juisi kwenye kontena. Nilimuomba sana Mungu anifunue kama ninachokiwaza ni sahihi, baadaye nilipata amani nikaamua kulitengeneza kontena langu kwa kiwango kidogo cha fedha nilichokuwa nimejaaliwa ili lionekane, nikaanza biashara. Nilifanya hivyo ili mtu mwingine akiona aone ni kitu ambacho naweza kujivunia,” anasema.
Alipomaliza chuo mwaka 2024, aliamua kuweka nguvu zake zote katika biashara hiyo, huku mitandao ikiwa ni sehemu mojawapo ya kujitangaza. Hadi sasa, Anitha anauza zaidi ya aina 20 za juisi, ikiwemo zile zinazosaidia kujenga afya ya binadamu.
“Ninachouza siyo juisi tu, nahakikisha mtu anywe si kwa ajili ya kukata kiu bali pia kujenga mwili, kwani zipo detox zinazosaidia kutoa sumu mwilini, kupunguza kitambi, mafuta, kusafisha ini, kuweka mwili sawa na kuongeza kinga ya mwili,” anasema.
Zaidi ya mwaka mmoja katika biashara hiyo, Anitha anajivunia uamuzi wake alioufanya kwa kutumia kiwango kidogo cha fedha, kwani amemudu maisha na gharama zake za kila siku.
“Mungu ni mwema, tangu nimemaliza chuo mwaka 2024 sihangaiki kiuchumi, nalipa kodi ya nyumba na ofisi, maisha yangu yanaenda. Siwezi kujilinganisha na mhitimu ambaye hakuwa na kitu kidogo cha kujiingizia kipato,” anasema.
Licha ya mafanikio aliyoyapata, bado hajasahau mchango aliowahi kuupata kutoka kwa watu maarufu waliotambua kile alichokifanya, jambo lililongeza umaarufu wake mtandaoni na wateja.
“Kuna siku Niffer (Janifer Jovin) aliona kile ninachokifanya, akaniweka kwenye ukurasa wake, nilipata soko kubwa, nilisaidika sana, wateja walikuwa wengi,” anasema.
Licha ya kumiliki biashara hiyo, Anitha, mtoto wa mwisho kati ya watoto watatu, bado anatamani kupata nafasi ya kuisaidia jamii kupitia kile alichokisoma, kwani anaamini itakuwa msaada kubadili mitazamo ya watu wengi.
“Nilichosoma kina mchango mkubwa kwenye jamii, na bado kuna pengo kubwa la utaalamu wetu, hivyo nikipata kazi nitaenda, lakini nitahakikisha biashara yangu inaendelea. Siwezi kuiacha kwani itakuwa nimetoa ajira kwa wengine,” anasema.
Anitha anawakilisha kundi kubwa la vijana walioamua kujiajiri baada ya kumaliza masomo yao badala ya kusubiri kuajiriwa, jambo linalopigiwa chapuo na serikali.
Suala hilo linapigiwa chapuo kwani nafasi za ajira zilizopo ni chache ukilinganisha na idadi ya wahitimu wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka, jambo ambalo limeilazimu Serikali kuanzisha mtaala wa amali ili kuhakikisha wanafunzi wanapomaliza masomo wanakuwa na ujuzi utakaowawezesha kujiajiri.
Hilo limefanyika wakati takwimu za Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) za mwaka 2024 zinaonesha ongezeko la wahitimu wa vyuo hadi kufikia 62,570 mwaka 2024, kutoka 48,621 mwaka 2020.
Hata hivyo, ripoti ya utafiti wa ajira na mapato katika sekta rasmi Tanzania ya mwaka 2022/2023 inabainisha kuwa asilimia 22.3 ya wahitimu wa vyuo vikuu ndio waliopata nafasi ya kuajiriwa katika sekta rasmi, jambo ambalo linaonesha ulazima wa kuwajenga watu katika namna wanayoweza kujiajiri.
