RC LINDI AONGOZA UPANDAJI MITI LINDI, AONYA HATARI YA JANGWA

……..

_Asisitiza upandaji miti si hiari bali ni wajibu wa kila mwananchi kulinda chakula, mvua na uhai wa binadamu.

Na Mwandishi Wetu, Lindi

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe Zainabu Telack, ameongoza wananchi kushiriki zoezi la upandaji miti huku akionya vikali juu ya uharibifu wa misitu, akisema hatua hiyo inaweza kuigeuza Lindi kuwa jangwa na kuhatarisha upatikanaji wa chakula na mvua za uhakika.

Akizungumza leo Machi 17, 2026 katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Kiwalala, Halmashauri ya Mtama, Telack alisema upandaji miti si jambo la hiari bali ni wajibu wa kila mwananchi kwa kuwa misitu ni msingi wa maisha ya binadamu.

“Tunapopanda miti hatumfanyii mtu mwingine, tunajifanyia sisi. Misitu ni chakula, ni biashara, ni dawa na chanzo cha hewa safi na mvua. Tukiharibu misitu, maisha yetu yatakuwa magumu,” alisema.

Alisema mkoa wa Lindi bado una bahati ya kuwa na misitu mingi ikilinganishwa na maeneo mengine nchini, lakini akaonya kuwa kasi ya uharibifu ikiongezeka, hali hiyo inaweza kubadilika na kuathiri kizazi cha sasa na kijacho.

Katika zoezi hilo, jumla ya miti 1,347 ilipandwa na wananchi, wanafunzi na viongozi wa serikali ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Kampeni ya Upandaji Miti Kitaifa 2026.

Aagiza ulinzi wa miti, akemea wafugaji na wakataji haramu

Telack aliwataka viongozi wa ngazi zote kuanzia vitongoji hadi wilaya kuhakikisha wanasimamia na kulinda miti yote inayopandwa, huku akisisitiza hatua kali zichukuliwe kwa waharibifu wa mazingira.

Aliyataja baadhi ya matendo yanayopaswa kudhibitiwa kuwa ni pamoja na ukataji miti bila vibali, uchomaji moto ovyo pamoja na uingizaji wa mifugo katika maeneo ya hifadhi na yale yaliyopandwa miti.

“Tukiuza maeneo yetu na kuruhusu mifugo kuingia kwenye maeneo ya misitu, tutapoteza uoto wote. Tusikubali hilo litokee,” alisisitiza.

Aidha, aliwataka wananchi kupanda miti ya matunda majumbani mwao ili kusaidia lishe kwa familia na wanafunzi, akieleza kuwa miti hiyo pia ni chanzo cha kipato na maarifa kwa jamii.

Atoa wito utafiti wa maembe ya Lindi

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa aliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kufanya utafiti wa kitaalamu kuhusu aina ya maembe yanayozalishwa Lindi, akisema yana ladha ya kipekee na yanaweza kuwa zao la kimkakati kiuchumi.

“Maembe ya Lindi ni matamu sana na yana soko. Tunahitaji kujua aina yake na namna ya kuyaendeleza ili yaweze kuingia kwenye masoko makubwa zaidi,” alisema.

TFS: Mti wa mwembe ni lishe na uchumi

Awali, Kamanda wa Kanda ya Kusini wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), SACC Manyisye Mpokigwa, alisema mti uliopandwa na Mkuu wa Mkoa ni mwembe (Mangifera indica), ambao una faida nyingi ikiwemo lishe, kivuli na kipato.

Alisema matunda ya mwembe yana mchango mkubwa katika afya ya watoto huku yakitoa fursa za kiuchumi kupitia biashara ya matunda na bidhaa zake kama juisi.

Zaidi ya miti milioni 113 yapandwa kitaifa

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Daniel Pancrasi, alisema tangu kuanza kwa kampeni hiyo mwezi Januari mwaka huu, zaidi ya miti milioni 113 imepandwa nchini kote.

Alisema kwa Mkoa wa Lindi pekee, miti zaidi ya milioni 1.2 imepandwa katika wilaya zote ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuongeza uoto wa asili na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Pancrasi aliahidi kuwa wizara itaendelea kushirikiana na halmashauri na taasisi zake kuhakikisha miti inayopandwa inalindwa na kustawi.

Lengo: Shule zote zipate miti ya matunda

Katika hotuba yake, Telack aliweka bayana azma ya serikali ya mkoa kuhakikisha shule zote za sekondari zinakuwa na miti ya matunda ili kusaidia lishe kwa wanafunzi na walimu.

Alisema hatua hiyo itaenda sambamba na mpango wa kuimarisha kilimo shuleni ili kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula cha mchana na matunda, hali itakayochochea afya na ufaulu wa masomo.

Awali, akitoa taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama, Afisa Misitu Saumu Ramadhani Sambara alisema juhudi za upandaji miti zinaendelea kuimarishwa wilayani humo ili kufikia malengo ya uhifadhi na maendeleo endelevu.

Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani mwaka huu yanafanyika huku serikali ikiendelea kusisitiza ushiriki wa wananchi katika kupanda na kulinda miti, ikiwa ni njia ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda rasilimali za asili.

*Kuelekea kilele Machi 21*

Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Kampeni ya Upandaji Miti Kitaifa mwaka 2026 yanatarajiwa kufikia kilele Machi 21 katika Uwanja wa Ilulu, mkoani Lindi, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ambaye atazindua rasmi maadhimisho hayo Machi 19, 2026.

Serikali imeendelea kuhimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo kwa kupanda na kutunza miti, ikiwa ni njia muhimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha uhifadhi endelevu wa rasilimali za misitu nchini.