Mwanga. Serikali kupitia Wizara ya Maji imesema itaendelea kuhakikisha wananchi wanaozungukwa na mradi mkubwa wa maji wa Same–Mwanga–Korogwe wanapata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika wakati wote.
Hatua hiyo inalenga kuboresha maisha ya wananchi pamoja na kulinda afya za jamii zinazoishi katika maeneo yanayonufaika na mradi huo.
Akizungumza leo Jumanne Machi 17, 2026 wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira ilipotembelea mradi huo, Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew amesema serikali imejipanga kusimamia upatikanaji endelevu wa huduma hiyo muhimu.
Mradi huo unapata maji kutoka Bwawa la Nyumba ya Mungu lililopo Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, na ulianza kutekelezwa mwaka 2014. Awamu ya kwanza imekamilika na kuzinduliwa mwaka jana na Rais Samia Suluhu Hassan, ukiwa umegharimu zaidi ya Sh300 bilioni.
Kwa mujibu wa Kundo, mradi huo kwa sasa unahudumia wananchi 456,931 katika wilaya za Mwanga, Same na Korogwe.
Amesema awamu ya pili ya mradi huo, inayotarajiwa kukamilika mwaka 2038, itapanua zaidi wigo wa huduma na kuongeza idadi ya wanufaika, huku gharama zake zikifikia zaidi ya Sh406 bilioni.
“Huu ni uwekezaji mkubwa ambao umeleta matumaini kwa wananchi waliokuwa na changamoto kubwa ya maji katika wilaya hizi. Unaonesha kuwa inawezekana kwa Watanzania kupata maji safi na salama,” amesema Kundo.
Ameongeza kuwa Wizara ya Maji itaendelea kupokea na kufanyia kazi maoni ya wabunge ili kuhakikisha malengo ya serikali ya kutoa maji ya uhakika, yenye gharama nafuu na endelevu yanafikiwa.
Aidha, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya maji, akisema hatua hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi waliokuwa wakikabiliwa na uhaba wa maji kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Profesa Pius Yanda, ameitaka wizara kuhakikisha inaharakisha utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo ili wananchi wengi zaidi wanufaike.
Amesema licha ya uwekezaji mkubwa uliofanyika, bado vijiji 12 pekee ndivyo vinavyonufaika kwa sasa, hivyo kuna haja ya kuongeza kasi ili kufikia maeneo yote yaliyokusudiwa.
“Kama tunazungumzia vijiji 12 pekee, bado lengo la kumtua mama ndoo kichwani halijafikiwa kikamilifu. Wananchi wanahitaji huduma hii sasa, siyo kusubiri hadi mwaka 2038,” alisema Profesa Yanda.
Ameshauri wizara kuandaa mkakati madhubuti utakaoiwezesha Serikali kupata fedha za kukamilisha mradi huo mapema zaidi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mangwala, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, alisema mradi huo umeleta nafuu kubwa kwa wananchi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta maji.
Amesema zaidi ya wananchi 96,000 kutoka vijiji 12 tayari wananufaika na huduma hiyo, huku awali wakilazimika kutembea zaidi ya kilomita tano kutafuta maji na kulipia kati ya Sh500 hadi Sh1,000 kwa ndoo.
“Mradi huu umeleta mabadiliko makubwa katika maisha ya wananchi. Zamani upatikanaji wa maji ulikuwa changamoto kubwa, lakini sasa hali imeanza kuimarika,” amesema Mangwala.
