Dar es Salaam. Katika mapitio ya uamuzi wa shauri la kupinga Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, tunaangalia hoja za Serikali dhidi ya hoja za waombaji.
Baada ya mawakili wa waombaji kuwasilisha hoja zao kufafanua sabau za kuipinga tume hiyo, wajibu maombi wa kwanza (AG) na wa pili mpaka wa tisa (mwenyekiti na wajumbe wa tume hiyo) walijibu hoja hizo wakizipinga vikali.
Wajibu maombi hao wote waliwakilishwa na jopo la mawakili wa Serikali wanne kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, lililoongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Vivian Method (PSA) akisaidiwa na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Daniel Nyakiha na Narindwa Sekimanga na Wakili wa Serikali, Erigh Rumisha.
Kuhusu hoja ya uhalali wa tume hiyo, wakili Rumisha, alipinga madai ya tume hiyo kutokuwa halali, huku akidai kuwa undwaji wa tume na uteuzi wa makamishna ulifanywa kwa mujibu wa masharti ya sheria.
Wakili Rumisha akijibu hoja ya aina ya makamishna wa tume hiyo, alieleza kuwa kifungu cha 3 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi hakijaweka kikomo wala vigezo vya makamishna wanaopaswa kuteuliwa.
Hivyo, wakili Rumisha alisisitiza kuwa uteuzi wa makamishna wa tume hiyo upo kabisa ndani ya mamlaka ya utashi wa Rais.
Alisema kuwa, kama Bunge lingekusudia kuweka vigezo au sifa za makamishna, lingeziweka wazi katika sheria hiyo.
Ili kutia nguvu hoja yake hiyo, Wakili Rumisha aliomba Mahakama itumie kanuni ya maana ya kawaida ya maneno ya sheria.
Katika hilo aliielekeza katika uamuzi wa mashauri ya Pan African Tanzania Limited dhidi ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), rufaa ya madai namba 172 ya 2020, Mahakama ya Rufani Dar es Salaam, na Jamhuri dhidi ya Mwesige Geofrey na mwenzake, rufaa ya jinai namba 355 ya 2014.
Wakili Rumisha alifafanua kwamba pale ambako maneno ya sheria yako wazi, Mahakama lazima ichukulie kwamba, Bunge lilimaanisha kile kilichoandikwa katika sheria husika.
Hivyo, wakili Rumisha alieleza kuwa, kwa mujibu wa masharti ya sheria hiyo ya Tume za Uchunguzi, Rais yuko huru kuipa tume jina lolote analoona linafaa.
Akijibu madai ya waombaji kuwa uundwaji na uteuzi wa makamishna wa tume hiyo haukuwa wa busara, wakili Rumisha alisema mtu hawezi kusemwa ametenda bila busara wakati anapotumia mamlaka aliyopewa na sheria iliyotungwa ipasavyo na kupitishwa na Bunge.
Kwa kusisitiza hoja yake hiyo wakili Rumisha aliielekeza Mahakama katika uamuzi Mahakama ya Rufani na wa Mahakama Kuu.
Mashauri hayo ni baina ya Zuberi Mussa dhidi ya Halmashauri ya Mji wa Shinyanga, maombi ya madai namba 100/2004, lililoamriwa na Mahakama ya Rufani iliyoketi Mwanza.
Shauri lingine ni Umoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania (Uwamata) dhidi ya Surface and Marine Transport Authority (Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini – Sumatra), shauri la madai namba 87 la mwaka 2019, lililoamuriwa na Mahakama Kuu Dar es Salaam.
Kwa maelezo hayo, wakili Rumisha alidai kuwa malalamiko ya waombaji yangekuwa na uzito kama wangeipinga sheria yenyewe.
Akijibu hoja kuhusu maudhui ya tume hiyo (mambo ambayo inapaswa kuyachunza, wakili Rumisha aliirejesha mahakama kwenye Tanazo la Serikali (GN) la Novemba 20, 2025) linalozungumzia tume hiyo, ambalo kiambatanisho cha mjibu maombi wa kwanza (AG).
Kwa kuzingatia kiambatanisho hicho, wakili Rumisha alieleza kuwa, kinaeleza kwa uwazi na kwa usahihi kile ambacho tume hiyo inaelekezwa kukifanya.
Hivyo, alidai kuwa maombi ya waombaji yalijengwa katika msingi wa maoni yao binafsi na dhana tu (si uhalisia).
Kuhusu madai ya upendeleo wakili Rumisha alidai kuwa, madai hayo pia ni dhana tu zisizo na msingi wa ushahidi, huku akifafanua kuwa ni kanuni ya sheria kwamba anayetoa madai ana wajibu wa kuthibitisha madai yake.
Wakili Rumisha aliieleza Mahakama kuwa licha ya madai hayo, lakini waombaji walishindwa kuthibitisha kuwepo kwa upendeleo dhidi ya makamishna hao.
Akirejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika uamuzi wa mashauri mawili, wakili Rumisha alidai kwamba, Mahakama haiwezi kutenda kwa kutegemea dhana au mawazo tu.
Mahakama ya Rufani ilieleza msimamo huo kwenye mashauri ya David Joseph Mahende dhidi ya Afriscan Group (T) Ltd, rufaa ya madai namba 200/2017, na la Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wengine wawili dhidi ya Bob Chacha Wangwe, rufaa ya madai namb 138/2019
Kwa kuzingatia msimamo huo wa Mahakama ya Rufani, wakili Rumisha aliiomba Mahakama iyapuuze madai ya waombaji, kwa madai hayo ya kujengwa juu ya dhana.
Vilevile wakili Rumisha aliieleza Mahakama kuwa, kifungu cha 10 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi kinaeleza kwa uwazi mazingira ambayo makamishna wa tume wanaweza kuwa na maoni yanayokinzana.
Hivyo, wakili Rumisha alidai kuwa uwepo wa mjibu maombi wa tisa peke yake (Tax, ambaye waombaji walidai kuwa anaweza kuwa mmoja wa watuhumiwa kwa kuwa wakati wa vurugu hizo alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) hauwezi kuleta upendeleo katika Tume.
Huku akiielekeza Mahakama kwenye Ibara ya 278(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Ghana, wakili Rumisha alidai kwamba, utafiti wa utaratibu bora katika nchi nyingine unaonesha kuwa muundo wa tume unahitaji wajumbe wenye maarifa ya kutosha kuhusu jambo linalochunguzwa.
Wakili Rumisha alieleza kwamba, tume ya uchunguzi haitoi uamuzi wala kuamua haki ya mtu yeyote, bali hukusanya ukweli na kutoa mapendekezo tu.
Kwa kuzingatia hoja hizo zote, wakili Rumisha aliiomba Mahakama hiyo itupilie mbali shauri hilo kwa gharama, yaani amri ya waombaji kulipa gharama za shauri hilo,
Hata hivyo, akijibu hoja hizo za mawakili wa wajibu maombi, mawakili wa waombaji, Jebra Kambole na Hekima Mwasipu walizipinga.
Wakili Kambole alidai kuwa, mamlaka ya utashi wa Rais katika kuteua makamishna hao hayakutumika ipasavyo, huku akisisitiza kuwa, kwa kuangalia Gazeti la Serikali la Novemba 20, 2025, madhumuni ya tume hiyo hayaonekani kwa uwazi.
Pia, wakili Kambole alisema kuwa, wajibu maombi hawakuweza kuthibitisha kuhusu hoja ya makamishna hao kutokuapa kabla ya kuanza jukumu lao na kwamba hilo lilikuwa ni wajibu wa wajibu maombi kuleta ushahidi wa viapo vyao ili kupinga madai ya waombaji.
Kwa upande wake, wakili Mwasipu alidai kuwa kesi ya Umoja wa Madereva iliyorejewa na wakili Rumisha wa wajibu maombi mazingira yake ni tofauti na shauri hilo.
Wakili Mwasipu alisisitiza kwamba, waombaji wanapinga uteuzi wa makamishna, si namna tume inavyofanya kazi, huku akisihi Mahakama isitumie mfano wa Katiba ya Jamhuri ya Ghana, kama ilivyorejewa na wajibu maombi, akisema ina nguvu ya ushawishi tu lakini haiifungi Mahakama hiyo.
Baada ya mchuano huo wa hoja za mawakili wa pande zote usikose sehemu inayofuata, Mahakama inaanza kuchambua hoja za pande zote kabla ya kufikia hitimisho la uamuzi wake.
