******
Serikali imetoa maelekezo nane ya kimkakati yanayolenga kuimarisha utendaji wa kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuharakisha safari ya Tanzania kuelekea hadhi ya nchi ya kipato cha kati cha juu kama ilivyo ainishwa kwenye Dira 2050.
Dira hiyo inalenga kukuza uchumi wa Tanzania kutoka ukubwa wa sasa wa takribani dola za Marekani bilioni 85 hadi kufikia dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050, lengo ambalo linahitaji kuimarika kwa uwekezaji wa umma, ikiwemo kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa za wachache.
Akifungua Mkutano wa Wakurugenzi wa Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache (MIF 2026) unaofanyika kwa siku tatu jijini Arusha, Jumatatu, Machi 16, 2026, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Dkt. Khamis Mussa Omar, alisema kuwa maelekezo hayo yanalenga kuhakikisha kampuni hizo zinaendeshwa kwa misingi ya mikakati thabiti, uwazi na ufanisi wa kibiashara, ili ziweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika mageuzi ya uchumi wa taifa.
Wakati wa Mkutano huo ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, alisema bodi za wakurugenzi na menejimenti zinapaswa kuoanisha mikakati ya kampuni zao na vipaumbele vya maendeleo ya taifa pamoja na mwenendo wa uchumi wa dunia, ili uwekezaji uweze kukidhi mahitaji ya masoko yanayobadilika na wakati huo huo kuleta ukuaji shirikishi wa uchumi.
Aidha, Waziri huyo alizitaka kampuni hizo kutumia teknolojia kama nyenzo ya kuimarisha uwazi, kuongeza imani ya umma na kuboresha mifumo ya utawala bora katika taasisi zao.
Alieleza kuwa maelekezo hayo pia yanasisitiza umuhimu wa kuwa na uongozi unaotazama mbele, unaowawezesha wakurugenzi na watendaji wakuu kutambua mapema hatari zinazoweza kujitokeza na kutumia fursa mpya katika mazingira ya uchumi wa dunia yanayozidi kuwa na ushindani mkubwa.
Vilevile, Serikali inahamasisha kuimarishwa kwa ushirikiano na ubia kati ya kampuni mbalimbali ili ziweze kubadilishana uzoefu, kufungua fursa mpya za kiuchumi na kuongeza matokeo chanya kwa pamoja.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, kuimarishwa kwa mifumo madhubuti ya utawala inayozingatia uwajibikaji, uwazi na uongozi wenye maadili ni jambo la msingi katika kuhakikisha uwekezaji wa umma unaleta tija endelevu.
Alisisitiza kuwa kampuni zinapaswa kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia matokeo, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kiutendaji, kukuza faida na hatimaye kuongeza thamani kwa wanahisa pamoja na Serikali.
Mhe. Omar pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha uchambuzi wa taarifa za kiuchumi na ushindani ili maamuzi ya kibiashara yafanywe kwa kuzingatia takwimu sahihi na taarifa za soko, hatua itakayosaidia kuongeza tija na ushindani katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, akibainisha kuwa ubia imara kati ya pande hizo ni nyenzo muhimu katika kufungua fursa za uwekezaji na kuharakisha maendeleo ya taifa.
Serikali kupitia Dira 2050 imejipanga kuongeza mchango wa mapato yasiyotokana na kodi katika bajeti ya taifa kutoka asilimia tatu ya sasa hadi kufikia asilimia kumi ndani ya miaka mitano ijayo, sawa na lengo la kukusanya takribani shilingi trilioni tano kila mwaka.
Waziri alisema kuwa kufikiwa kwa lengo hilo kunahitaji mabadiliko ya makusudi katika fikra na mifumo ya uendeshaji wa taasisi.
“Hii inahitaji kuondoka katika mtazamo wa uangalizi wa kawaida na badala yake kujenga uongozi unaotazama mbele, unaozingatia ubunifu, wepesi wa kufanya maamuzi na uwezo wa kutabiri mwelekeo wa maendeleo,” alisema Mhe. Omar.
Alisisitiza kuwa mabadiliko hayo yanapaswa kwenda sambamba na matumizi bora ya kila uwekezaji katika kampuni husika ili uweze kuleta matokeo makubwa zaidi ya kiuchumi na kifedha.
Bila mabadiliko hayo, alisema, itakuwa vigumu kufikia malengo yaliyowekwa katika Dira 2050.
Waziri huyo aliwataka wakurugenzi na watendaji wakuu wa kampuni hizo kuwa viongozi wanaotazama mbele na kushughulikia kikamilifu changamoto zinazoathiri utendaji wa taasisi wanazosimamia.
“Ni lazima tukubali mabadiliko na tuwe viongozi wanaotafakari kwa kina, kuchukua hatua mapema, na kutambua changamoto zinazoathiri utendaji wa kampuni zetu, huku tukitafuta suluhisho endelevu,” alisema.
Aidha, aliwataka viongozi wa kampuni hizo kuchukua jukumu la moja kwa moja katika kuimarisha utendaji na uendelevu wa taasisi wanazoongoza.
“Kupitia mkutano huu, nawapa changamoto kila mmoja wenu kutekeleza kikamilifu wajibu wenu kama viongozi wa kampuni zenye umiliki wa hisa chache,” alisema.
“Ni lazima tuje na mikakati madhubuti itakayoboresha kwa kiasi kikubwa utendaji wa kampuni hizi huku tukihakikisha zinadumu na kuendelea kustawi.”
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Uwekezaji, Dk. Fred Msemwa, alieleza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ili kuimarisha sekta binafsi.
“Tutafanya kila linalowezekana, ikiwemo kupitia upya sheria na sera mbalimbali kwa lengo la kuboresha zaidi mazingira ya biashara, kwani tunatambua kuwa sekta binafsi ni chachu ya kufanikisha malengo ya Dira 2050,” alisisitiza.
Awali akizungumza katika mkutano huo, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alisema jukwaa hilo ambalo linafanyika kwa mara ya tatu tangu kuanzishwa kwake mwaka 2024, limekuwa sehemu muhimu ya viongozi wa kampuni hizo kujadili masuala ya utawala bora, utendaji na mchango wao katika mageuzi ya uchumi wa Tanzania.
Alisema kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu inayosema “Kutoka Ufuatiliaji wa kawaida hadi Uongozi wa Kimkakati unaotazama mbele:” inaakisi umuhimu wa bodi za wakurugenzi na viongozi wakuu kuacha mtazamo wa usimamizi wa kawaida na badala yake kuwa na uongozi unaoweza kutambua mapema changamoto na fursa za baadaye.
“Katika dunia ya leo inayobadilika kwa kasi kiuchumi na kiteknolojia, uongozi hauwezi tena kujikita tu katika kusimamia hali ya sasa, bali pia unapaswa kutazama mbele na kujiandaa kwa siku za usoni,” alisema.
Aliongeza kuwa taasisi zinazojenga utamaduni wa kufikiri mbele, ubunifu na wepesi wa kufanya maamuzi ndizo zitakazoweza kukabiliana na shinikizo la mabadiliko na pia kuongoza mwelekeo wa maendeleo.
Bw. Mchechu alisema mkutano huo pia unaendana na malengo ya Dira 2050, inayolenga kujenga uchumi imara, shindani na unaochochewa na ubunifu, unaoungwa mkono na taasisi zenye ufanisi, uwajibikaji na uongozi unaotazama mbele.
Alifafanua kuwa mkutano huo unatoa fursa kwa wakurugenzi na watendaji wakuu kubadilishana uzoefu, kuimarisha mifumo ya utawala bora na kujenga uwezo katika maeneo muhimu kwa ushindani na uendelevu wa taasisi zao.
Bw. Mchechu pia alieleza kuwa uwekezaji wa Serikali katika kampuni ambazo Serikali ina hisa chache umeongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kutoka Sh821 bilioni hadi kufikia Sh3.6 trilioni, jambo linaloonesha kuendelea kuimarika kwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.
Aidha, michango ya gawio kutoka katika kampuni hizo imeongezeka kwa kiwango kikubwa, kutoka Sh58 bilioni hadi kufikia Sh266 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 357 katika kipindi hicho.
Mkutano wa MIF 2026 umewakutanisha zaidi ya wakurugenzi 200, Maafisa Watendaji Wakuu, watunga sera na wataalamu kutoka ndani na nje ya Tanzania kwa lengo la kujadili mikakati ya kuimarisha utendaji na utawala wa kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache, ili ziweze kuchangia kwa ufanisi zaidi katika maendeleo ya uchumi wa taifa kwa muda mrefu.





