MABADILIKO ya sheria za soka ambazo kimsingi zitaanza kufanya kazi wakati wa Kombe la Dunia 2026 kabla ya kuhamia karika ligi mbalimbali, yamemuibua mkufunzi wa waamuzi nchini, Soud Abdi ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi Tanzania, akisema yataondoa tabia ya janjajanja ya kupoteza muda ambayo imekuwa ikiharibu ladha ya mchezo.
Akizungumza kuhusu maboresho hayo ya sheria ambayo yataanza kufanya kazi Novemba 8, 2026, Abdi alisema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuboresha kasi ya mchezo na kuhakikisha mashabiki wanaona mpira unachezwa kwa ushindani bila mbinu za kuchelewesha muda.
Alisema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa mashabiki, makocha na wadau wa soka kuhusu baadhi ya timu kutumia mbinu za kupoteza muda hasa wanapoongoza.
“Tusubiri kuona kwa namna gani zitafanya kazi, binafsi naona zitakuwa msaada mkubwa sana, nafikiri baada ya Kombe la Dunia tutaona sasa zikifanya kazi katika ligi nyingine, hivyo ni vizuri klabu zetu (ikiwemo Simba na Yanga), wachezaji, waamuzi na timu zetu za taifa zikajiandaa na mabadiliko hayo,” alisema mwamuzi huyo wa zamani.
Kwa mujibu wa Abdi, sheria hizo zitawafanya waamuzi kuwa na mamlaka zaidi ya kudhibiti mchezo na kuzuia vitendo vya kuchelewesha kuanzishwa kwa mpira kama vile kupiga kona, kurusha mpira wa pembeni au kipa kuchelewa kuanzisha mchezo.
Alisema kuwa waamuzi wanatakiwa kujifunza kwa kina mabadiliko hayo ili waweze kuyasimamia kwa ufanisi pale yatakapoanza kutumika katika mashindano mbalimbali duniani.
Abdi aliongeza kuwa mabadiliko hayo yanaweza pia kusaidia kuongeza nidhamu kwa wachezaji ambao mara nyingi wamekuwa wakitumia ujanja kuchelewesha mchezo ili kulinda matokeo.
Kwa upande mwingine alisema wadau wa soka nchini wanapaswa kuanza kuyafahamu mapema mabadiliko hayo ili kuepuka mkanganyiko pale sheria hizo zitakapoanza kutumika.
Miongoni mwa mabadiliko hayo ni sheria ya muda kwa kurusha mpira ambapo mchezaji anatakiwa kurusha ndani ya sekunde tano baada ya mwamuzi kuruhusu mchezo kuendelea na akichelewa itakuwa faida kwa wapinzani.
Sheria nyingine inamuhusu kipa, ikiwa atachelewesha kuanzisha shambulizi, timu pinzani inapewa kona kama adhabu.
Pia mabadiliko yamegusa utaratibu wa mabadiliko ya wachezaji ambapo mchezaji anayefanyiwa mabadiliko anatakiwa kutoka nje ya uwanja ndani ya sekunde 10 mara baada ya namba yake kuonyeshwa kwenye ubao wa mabadiliko. Ikiwa mchezaji atachelewesha kutoka uwanjani, mchezaji anayetarajiwa kuingia atalazimika kusubiri kwa dakika moja kabla ya kuruhusiwa kuingia ili kuzuia mbinu za kupoteza muda.
Sheria mpya inasema kuwa mchezaji ambaye mchezo umesimamishwa kwa ajili ya kupewa matibabu atalazimika kutoka nje kwa dakika moja kabla ya kuruhusiwa kurudi uwanjani. Lengo la hatua hiyo ni kuzuia baadhi ya wachezaji kujifanya wameumia ili kuchelewesha mchezo au kupunguza presha kutoka kwa wapinzani.