Tanga. Utafutaji wa watu watatu waliopotea kufuatia kuzama kwa jahazi katika Bahari ya Hindi, eneo la Nungwi kisiwani Unguja, bado unaendelea huku matumaini ya kuwapata yakiwa yameanza kupungua.
Jahazi hilo lililosajiliwa kwa ajili ya kubeba mizigo, lilikuwa limebeba watu 12 kinyume na taratibu wakati lilipopata ajali Machi 14, 2026.
Miili ya watu wawili ilipatikana jana, huku watu watatu wakiwa bado hawajulikani walipo, saba wakiokolewa wakiwa hai.
Baadhi ya wapakiaji wa mizigo kwenye majahazi wakiendelea na shughuli za upakiaji katika Bandari ya Pangani kwa ajili ya safari ya kwenda Bandari ya Mkokotoni Unguja.
Jahazi hilo la kubeba mizigo lililokuwa likisafiri kutoka Bandari ya Pangani mkoani Tanga kwenda Bandari ya Mkokotoni kisiwani Unguja, lilikuwa na watu 12 wakiwamo abiria tofauti na sheria inavyowataka.
Watu wanaotafutwa ni Idarous Said Mohd ambaye ni baharia, Issa Khamis Issa mfanyabiashara na Omar Bakari ambaye pia ni mfanyabiashara.
Kaimu Ofisa Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), Mhandisi Christopher Mlelwa amesema juhudi za utafutaji zinaendelea licha ya changamoto zilizopo baharini.
Amesema baada ya kupita kwa zaidi ya siku tatu tangu ajali hiyo ilipotokea, matumaini ya kuwapata watu hao wakiwa hai yanazidi kupungua kutokana na hali ya maji na mazingira ya bahari.
Mlelwa ameongeza kuwa uchunguzi bado unaendelea kubaini iwapo kulikuwa na watu wengine ndani ya jahazi hilo, pamoja na uwezekano wa miili kusukumwa na mawimbi au kuliwa na viumbe wa baharini.
Mjomba wa mmoja wa watu watatu wanaotafutwa majini baada ya Jahazi lao kuzama Nungwi March 14 kufuatia hali mbaya ya hewa, akielezea matumaini kidogo waliyonayo kama familia juu ya kumpata mpendwa wao.
Mjomba wa mmoja wa watu wanaotafutwa baada ya kupotea kwenye ajali hiyo, Mngwali Usi alisema tangu ajali hiyo ilipotokea, familia imepoteza matumaini ya kumpata mpendwa wao.
“Tunatarajia kusoma dua ya mjomba wangu Idarous Said (35) ambaye alikuwa baharia leo Jumanne Machi 17, 2026, familia hadi hapa tulipofikia tumepoteza matumaini kwa kiwango kikubwa, kila mtu anajua Nungwi ni eneo la bahari ambalo lina kina kirefu sana cha maji, ajali ikitokea maeneo yale madhara yake yanakuwa makubwa,”amesema Usi.
Awali, Mlelwa, alisema jahazi hilo lililozama linajulikana kwa jina la Mv Talawanda na lilikuwa likifanya safari zake za kusafirisha mizigo kati ya Pangani (Tanga) na Mkokotoni (Unguja).
“Kimsingi tunasisitiza vyombo vyote vinavyosafiri kwa njia ya maji vinatakiwa kusajiliwa na kuthibitishwa ubora na mamlaka husika ambayo ni Tasac,” alisema Mlelwa.
