Leo Tanzania inaadhimisha miaka mitano tangu kuondoka kwa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli nyumbani kwake wilayani Chato mkoani Geita nhuku Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwa ameshawasili tayari kuongoza maadhimisho hayo ya kitaifa.
Maadhimisho haya yanatarajiwa kupambwa na Misa Takatifu itakayofanyika nyumbani kwa Hayati Magufuli, ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kushiriki. Uwepo wa viongozi hawa wakuu unadhihirisha heshima ya kipekee na namna taifa linavyoendelea kumuenzi shujaa huyu wa Afrika.
Katika kuelekea kilele hiki, binti wa Hayati, Mhe. Jesca Magufuli (Mbunge wa Viti Maalum, Geita), jana aliongoza matembezi maalum ya hisani kumuenzi baba yake. Jesca alitembea bega kwa bega na wananchi wa Chato, akiamsha ari ya umoja na uzalendo ambayo ilikuwa ni moja ya nguzo kuu za uongozi wa Dkt. Magufuli.
Safari ya upendo ya Jesca ilihitimishwa kwa matendo makubwa ya huruma, ambapo alitembelea Gereza la Wanawake Chato na kutoa msaada wa mahitaji muhimu kwa wafungwa. Aidha, alifika katika Hospitali ya Wilaya ya Chato na kuwafariji wagonjwa kwa kutoa vifaa na misaada mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa kuwajali wanyonge kama alivyofanya baba yake.
Leo, wakati taifa likijumuika Chato, matendo hayo ya Jesca na uwepo wa viongozi wa juu wa nchi yanatoa ujumbe mzito kuwa maono ya JPM bado yanaishi. Chato imekuwa kitovu cha kumbukumbu na tafakari, huku Watanzania wakikumbuka kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu” na moyo wa dhati wa utumishi kwa umma.
.jpeg)

.jpeg)


.jpeg)


