Dar es Salaam. Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) limewakumbusha wananchi wanaotumia usafiri wa majini kutumia vyombo vya usafiri vilivyoidhinishwa kubeba abiria na kuepuka kupanda vyombo vya mizigo ambavyo haviruhusiwi kubeba abiria.
Tasac imetoa wito huo siku moja baada ya kuripotiwa jahazi lililosajiliwa kwa ajili ya kubeba mizigo kuzama na kusababisha vifo vya watu wawili, huku watu wengine watatu wakiwa bado hawajulikani walipo. Watu saba waliokolewa wakiwa hai.
Jahazi hilo la kubeba mizigo, lililokuwa likisafiri kutoka Bandari ya Pangani mkoani Tanga kwenda Bandari ya Mkokotoni kisiwani Unguja, lilikuwa na watu 12, wakiwamo abiria tofauti na sheria inavyowataka. Lilizama katika Bahari ya Hindi, eneo la Nungwi kisiwani Unguja.
Watu wanaotafutwa ni Idarous Said Mohd ambaye ni baharia, Issa Khamis Issa mfanyabiashara na Omar Bakari ambaye pia ni mfanyabiashara.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Tasac, Mohamed Salum, leo Jumanne, Machi 17, 2026, imewahimiza wananchi kuchukua tahadhari kutokana na matukio yaliyoripotiwa ya baadhi ya wananchi kupanda vyombo vya mizigo kinyume cha sheria, jambo linaloongeza hatari ya ajali na kuathiri usalama wa maisha.
“Vyombo vya mizigo havijaundwa wala kuidhinishwa kubeba abiria, hivyo kuvitumia ni kinyume na masharti na pia kunazidisha hatari, hasa wakati wa hali mbaya ya hewa au safari za usiku.
“Kila chombo cha usafiri majini kinapaswa kutumika kwa madhumuni yake yaliyoidhinishwa kisheria. Wamiliki na waendeshaji wanatakiwa kuzingatia kanuni za usalama ili kulinda maisha ya abiria na mali zao,” ameesema Salum.
Salum amewataka wananchi kuhakikisha wanapanda vyombo vinavyotambulika rasmi, vilivyo na vifaa vya usalama ikiwemo majaketi okozi, na vinazingatia idadi halali ya abiria.
Pia, amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wamiliki au waendeshaji watakaokiuka sheria kwa kubeba abiria kwenye vyombo vya mizigo au kuvuka idadi halali ya abiria.
“Tasac inaendelea kutoa wito kwa wananchi kushirikiana na mamlaka husika katika kuhakikisha usalama wa usafiri majini unazingatiwa kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa,” amesema.
