Vijana 3,967 waomba fedha kuendeleza biashara zao

Dar es Salaam. Benki ya CRDB imepokea maombi 3,967 kutoka kwa vijana wajasiriamali nchini kupitia mradi wake wa Go Green na Imbeju ili wapate mitaji ya kuendeleza mawazo yao ya kibunifu, huku mikoa 10 ikiwa kinara, ikiwemo Dar es Salaam na Mwanza.

Programu hiyo ilizinduliwa Februari 12 mwaka huu ikiwa na lengo la kuwawezesha vijana wenye miradi bunifu inayohusiana na kilimo himilivu, nishati safi na jadidifu, teknolojia za maji, usimamizi wa taka, uhifadhi wa mazingira na ubunifu wa kidijitali kwa mitaji nafuu kuanzia Sh500,000 hadi Sh50 milioni.

Akitangaza matokeo hayo baada ya kufungwa kwa dirisha la maombi, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema hatua inayofuata sasa ni tathmini ya kiufundi itakayofanywa na jopo la wataalamu kutoka CRDB na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

Pia, tathmini hiyo itahusisha Tume ya Tehama (ICTC) na Wizara ya Maendeleo ya Vijana, pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais inayosimamia Mazingira.

“Tathmini hiyo itazingatia ubunifu wa wazo la biashara, uendelevu wa mradi, uwezo wa biashara kujiendesha, pamoja na mchango wake katika kulinda mazingira. Mchakato huo,” amesema.

Amesema idadi hiyo ni ishara kuwa wazo la uchumi wa kijani linaanza kueleweka na kukubalika na vijana katika maeneo mengi.

Kupitia Go Green na Imbeju, amesema CRDB Bank Foundation inakusudia kuwawezesha vijana wanaomiliki kampuni changa, wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo, wakiwemo ambao biashara zao hazijarasimishwa, pamoja na wanafunzi waliopo vyuoni wenye mawazo ya biashara ambayo yanaweza kugeuzwa kuwa biashara halisi.

“Sifa muhimu kwa makundi yote matatu ni kuwa na ubunifu au biashara zenye uelekeo wa uchumi wa kijani, kama vile kilimo himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, uvuvi, matumizi ya nishati safi na jadidifu, teknolojia za maji na umwagiliaji, usimamizi wa taka na mazingira, pamoja na ubunifu wa kidijitali unaosaidia kulinda mazingira na kuboresha uzalishaji,” amesema.

Uchambuzi wa maombi yaliyopokelewa na CRDB Bank Foundation katika dirisha la maombi la Mradi wa Go Green na Imbeju, unaotekelezwa kwa kushirikiana na Benki ya CRDB kupitia Programu ya Tanzania Agriculture Climate Adaptation Development Program (TACATDP), pamoja na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (GCF) na FursaHub, unaonesha asilimia 58 ya waombaji ni wanaume, huku asilimia 42 wakiwa wanawake.

Kijiografia, idadi kubwa ya maombi imetoka Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Iringa, Morogoro, Arusha, Zanzibar, Pwani, Mara na Kilimanjaro.

Amesema wiki moja baada ya mchujo wa maombi hayo, waombaji waliopitishwa watakuja Dar es Salaam kupata mafunzo yatakayowasaidia kuboresha biashara na kuwaunganisha na wawekezaji mbalimbali, kama vile Warioba Ventures.

“Hatua ya tatu itakuwa kuhakiki biashara zinazofanya kazi, kuona kama kweli zinaendana na mawasilisho yao. Zoezi hili litachukua takribani wiki tatu, kwani biashara zote zitatembelewa kuona uhalisia wake kabla ya kutangaza biashara zilizokidhi vigezo vya kupata mtaji wezeshi,” amesema.

Kwa wanafunzi wa vyuo vikuu ambao wametuma mawazo yao ya biashara, yale yanayoweza kushindanishwa watapewa kati ya Sh500,000 na Sh10 milioni kuwasaidia kuyatekeleza mawazo hayo ili kushiriki kutatua changamoto zilizopo katika jamii.

Alipokuwa akizindua programu hiyo Februari, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alisema zinaendana kikamilifu na malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa 2050.

Alisema Serikali imekuwa ikiweka mkazo katika kuwawezesha vijana kiuchumi, kukuza uchumi wa kijani na kujenga mifumo imara ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.

“Miradi ya vijana inayolinda mazingira, kama tunavyoiona leo, ni utekelezaji wa moja kwa moja wa Dira ya Taifa 2050 kwa vitendo,” alisema Profesa Mkumbo.