Wafanyabiashara Mkuti watinga Mahakama Kuu kupinga ujenzi wa soko bila fidia

Mtwara. Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Mkuti lililopo Halmashauri ya Mji wa Masasi, wamefungua shauri la madai katika Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara kupinga mpango wa ujenzi wa soko jipya la kisasa katika eneo hilo, bila kufanyika tathmini ya mabanda yao na kulipwa fidia stahiki.

Hatua hiyo imekuja baada ya mvutano wa zaidi ya mwaka mmoja kati ya wafanyabiashara hao na uongozi wa halmashauri, huku wafanyabiashara wakisisitiza kuwa uwekezaji walioufanya unapaswa kuthaminiwa na kulipwa kabla ya kuhamishwa.

Akizungumza nje ya Mahakama Kuu, Leo Jumanne Machi 16, 2026, Makamu Mwenyekiti wa Soko Kuu Mkuti, Shaban Fadhil amesema  uamuzi wa kufungua shauri unatokana na madai ya kulipwa fidia ya fedha taslimu badala ya utaratibu wa mikopo unaopendekezwa, pamoja na kupewa eneo rasmi na muda wa kujiandaa kabla ya kuondoka.

Amesema kuanza kwa mradi huo bila uthamini na ulipaji wa fidia kunaweza kuwasababishia hasara kubwa wafanyabiashara, wengi wao wakiwa wamewekeza fedha nyingi katika mabanda wanayotegemea kama chanzo kikuu cha kipato.

Kwa mujibu wa Fadhil, soko hilo lilianzishwa mwaka 1968 baada ya wafanyabiashara kufyeka na kusafisha eneo hilo na kuanza kujenga vibanda. Hivi sasa lina zaidi ya wafanyabiashara 700.

“Tunatambua ardhi ni mali ya Serikali, lakini tunachohitaji ni fidia stahiki kwa kila mfanyabiashara ili aweze kuondoka kwa hiari. Pia tunahitaji uthamini ufanywe na wataalamu huru tunaowaamini,” amesema.

Wafanyabiashara hao wanasema wako tayari kupisha ujenzi wa soko jipya, lakini wanasisitiza kufanyike uthamini huru wa mali zao na kulipwa fidia kabla ya kuhamishwa.

Katibu wa wafanyabiashara hao, George Kabura amesema walikubaliana awali kufanyika kwa uthamini kabla ya hatua nyingine, lakini baadaye kulikuwa na mabadiliko yasiyoendana na makubaliano hayo.

Amesema kushindwa kubadilika kwa msimamo wa halmashauri kumewaongezea wasiwasi wafanyabiashara.

Katika hatua ya usikilizwaji, shauri hilo lilitajwa kwa mara ya kwanza Machi 16, 2026 kwa ajili ya upatanishi mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Said Ding’oi.

Jumla ya wafanyabiashara 150 walifika mahakamani kufuatilia shauri hilo, ambapo 73 waliruhusiwa kuingia ndani kusikiliza mwenendo wa kesi.

Pande zote zilishiriki katika upatanishi, lakini hazikufikia mwafaka hata baada ya kupewa muda wa ziada kujadiliana. Kutokana na hali hiyo, Jaji Ding’oi aliahirisha shauri hilo hadi Aprili 13, 2026.

Upande wa halmashauri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, ambaye hakutaka kuzungumzia kilichojiri mahakamani.

Mradi wa ujenzi wa soko jipya la kisasa Mkuti ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Kupitia mradi huo, Halmashauri ya Mji wa Masasi imepangiwa kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa barabara za lami, stendi ya kisasa na soko jipya katika eneo la Mkuti lenye ukubwa wa takribani mita za mraba 4,412, kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza mapato ya halmashauri.