Zanzibar mguu sawa ujenzi kituo cha mikutano kimataifa

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeanza mkakati kabambe kujenga Kituo cha Kimataifa cha kumbi za mikutano na maonesho ya biashara Fumba ambacho kitagharimu zaidi ya Dola za Marekani 124.518 milioni sawa na Sh324.680 bilioni.

Katika kuimarisha ukuaji na utafutaji masoko hapa nchini, Kituo hicho kinalenga kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kuunganisha biashara.

Akizungumza kuhusu ujenzi wa kituo hicho Machi 16, 2025 alipoulizwa na Mwananchi, Waziri wa Kazi na Uwekezaji ambaye pia ni kaimu Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Shariff Ali Shariff amesema biashara zitakazounganishwa ni za sekta muhimu za utalii, fedha, mawasiliano, miundombinu, elimu, afya na kilimo pamoja na kukuza biashara za ndani na za kimataifa.

Waziri wa Kazi na uwekezaji ambaye pia ni kaimu waziri wa Biashara na maendeleo viwanda Zanzibar, Shariff Ali Shariff

“Hili eeno litakuwa na facilities zote, kutakuwa na hoteli na malls na kiasi kwamba mtu akiwa anakuja kwenye mikutano kila kitu anakikuta palepale hatakuwa an sabau ya kuangaiaka kwenda kutafuta huduma sehemu nyingine isipokuwa tu kutoka hapo kwenda kutembeela maeneo mengine kama mji mkongwe na maeneo mengine ya utalii,” amesema

Sharrif amesema kituo hicho kitakuwa na ukubwa wa ekari 10.7 ambapo mshauri elekezi kutoka Nchini Korea ambaye anatarajiwa kuanza kazi ya upembuzi yakinifu   tayari amefika nchini mwishoni mwa Februari 2026 na matayarisho ya awali ya kazi hiyo yanaendelea.

Kuhusu hatua hizo, baadhi ya wadau kisiwani hapa wamepongeza hatua hiy wakisema huenda ukawa mwarobaini kwani Zanzibar inakosa baadhi ya matukio kutokna na kutokuwa na ukumbi mkubwa wa mikutano.

“Ukiangalia Zanzibar ukumbi mkubwa uliopo kwasasa hauzidi watu 1000 ambapo kwa kiasi kikubwa inapotokea mikutano mikubwa ya kimataifa hakuna sehemu ya kuwaweka watu,” amesema Haji Idd Haji.

Katika hatua nyingine Waziri Sharrif amesema serikali imeweka msukumo maalumu katika uwekezaji wa viwanda bila kuangalia ukubwa wa viwanda hivyo bali viweze kuzalisha mali ghafi kwa ajili ya maslahi ya Zanzibar na kwamba serikali itatoa kila aina ya msaada kuongeza uwekezaji katika maeneo hayo.

Kwa upande wa eneo la Viwanda Dunga Zuze tayari miradi mikubwa mitatu ya viwanda yenye thamani ya Sh203.906 bilioni inaendelea kujengwa.

Amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutazidi kuimarisha mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa kutoka asilimia 20.8 ya sasa na kufikia asilimia 25 mwaka 2030, pamoja na kuchangia upatikanaji wa ajira, kupunguza uagizaji bidhaa kutoka nje na kuchochea kuimarika biashara nchini.

Kwa upande wa biashara, amesema Serikali imeendelea kusimamia biashara ya zao la karafuu ambapo wakulima wa karafuu wameendelea kulipwa Sh15,000 kwa kilo moja, ikiwa ni zaidi ya asilimia 80 ya bei ya soko ya kuuzia nje.

Amesema idadi ya wateja wameongezeka na kufikia wateja wakubwa saba kutoka wateja watatu wa awali. Shirika la Biashara (ZSTC) limeuza jumla ya tani 3,702 za karafuu nje ya nchi kwa thamani ya Sh59.88 bilioni kwa kipindi cha siku 100 ambapo matarajio ya awali ilikuwa ni kuuza tani 2,827.

Kadhalika, katika jitihada za kuongeza thamani ya ufanyaji biashara Wizara kupitia Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) limeweza kuzalisha jumla ya tani 3,423.65 za karafuu  zenye thamani ya Sh55.45 bilioni, ambapo matarajio ya awali ilikuwa ni kununua tani za karafuu 2,870.