Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetangaza mpango wa kutoa ajira 1,300 kwa wataalamu wa sekta ya afya, katika jitihada za kukabiliana na upungufu wa watumishi na kupunguza msongamano katika hospitali za rufaa.
Hatua hiyo inatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa, huku wataalamu hao wakipangiwa kufanya kazi zaidi katika zahanati na vituo vya afya, ambako ndiko kunakokabiliwa na uhaba mkubwa wa watumishi.
Akizungumza leo Jumatano, Machi 18, 2025, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, Dk Saada Mkuya, amesema serikali imebaini kuwapo kwa uhitaji mkubwa wa wataalamu katika ngazi za chini za huduma za afya.
Amesema ukosefu wa wataalamu katika zahanati na vituo vya afya umekuwa chanzo kikuu cha wananchi wengi kukimbilia hospitali kubwa, hali inayosababisha msongamano na kupunguza ufanisi wa utoaji huduma.
“Tunatarajia kutangaza ajira 1,300 katika sekta hii, na wengi wa wataalamu hao wataelekezwa katika ngazi za chini, ili kuimarisha huduma na kupunguza mzigo kwa hospitali za juu,” amesema Dk Mkuya ambaye pia ni Kaimu Waziri wa Afya.
Kwa mujibu wa takwimu za wizara, hadi Februari 2026, uwiano wa daktari kwa mgonjwa umeimarika kutoka daktari mmoja kwa wagonjwa 6,272 hadi kufikia daktari mmoja kwa wagonjwa 2,963.
Hata hivyo, kiwango hicho bado kiko mbali na mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO), unaopendekeza daktari mmoja kwa wagonjwa 1,000.
Dk Mkuya amesema kuwa pamoja na juhudi za serikali kujenga hospitali na kuboresha miundombinu, changamoto ya uhaba wa wataalamu imeendelea kuwepo, hali inayosababisha wagonjwa wengi kusongamana katika hospitali za juu.
Amewataka vijana wazawa wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi kuomba nafasi hizo pindi zitakapotangazwa, ili kunufaika na fursa hiyo ya ajira, akisisitiza umuhimu wa wananchi wa ndani kushiriki kikamilifu katika kujenga sekta ya afya.
Katika kuimarisha huduma za kibingwa, wizara imepanga kuongeza idadi ya madaktari bingwa kutoka 126 mwaka 2024/25 hadi 136 mwaka 2025/26, huku madaktari bingwa 53 wakiwa masomoni.
Aidha, madaktari bingwa bobezi wameongezeka kutoka watatu hadi wanne, wakiwemo wataalamu wa moyo, radiolojia, figo, na upandikizaji figo.
Pia, idadi ya wauguzi bingwa imeongezeka kutoka 95 hadi 107, huku wauguzi bingwa 13 wakiwa wanaendelea na masomo.
Sambamba na hilo, serikali inaendelea na ujenzi wa hospitali nne za mikoa katika maeneo ya Kusini na Kaskazini Unguja pamoja na Kusini na Kaskazini Pemba, miradi inayotarajiwa kugharimu Sh129 bilioni.
Mradi wa hospitali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja katika eneo la Mahonda, unaojumuisha jengo la huduma za mama na mtoto unaofadhiliwa na Serikali ya Oman, umefikia asilimia 95 na unatarajiwa kukamilika Machi 2026. Ujenzi wa jengo kuu la hospitali hiyo unaendelea baada ya kusainiwa kwa mkataba Januari 2026.
Kutokana na juhudi hizo, serikali imesema vifo vya kinamama vimepungua kutoka 145 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2023 hadi 123 mwaka 2025, huku vifo vya watoto wachanga vikishuka kutoka 13.2 hadi 10.7 kwa kila vizazi hai 1,000 katika kipindi hicho.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameeleza kuendelea kukumbana na changamoto ya upatikanaji wa huduma, wakidai kuwa wakati mwingine hulazimika kusubiri muda mrefu kuanzia asubuhi hadi jioni bila kuhudumiwa kutokana na uhaba wa wahudumu wa afya.
