Iringa. Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, imemuhukumu kunyongwa hadi kufa Joseph Mhulila baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumuua mtoto wake, Timotheo Mhulila (4), kinyume na vifungu namba 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya mwaka 2022.
Hukumu hiyo ilitolewa katika kesi ya jinai namba 25532/2025, Jamhuri dhidi ya Joseph Mhulila, na Jaji Angaza Mwipopo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, aliyekuwa amepewa mamlaka ya ziada kusikiliza mashauri ya Mahakama Kuu.
Katika uamuzi wake uliotolewa jana Jumanne Machi 16, 2026 na mahakama hiyo Mjini Iringa, ilieleza kuwa imeridhishwa na ushahidi wa kimazingira uliowasilishwa na upande wa mashtaka, licha ya kuwepo kwa dosari na kukinzana kwa baadhi ya ushahidi, ikiwamo ule uliotolewa na mashahidi 13 kuhusu vipande vya mwili wa mtoto vilivyodaiwa kutupwa chooni.
Awali, mshtakiwa alishtakiwa kwa kosa la mauaji ya kukusudia, akidaiwa kutenda kitendo hicho kwa nia ya kujipatia utajiri kupitia imani za kishirikina.
Kwa mujibu wa ushahidi wa shahidi wa kwanza upande wa Jamhuri, mshtakiwa ambaye ni baba mzazi wa mtoto huyo, alimchukua mtoto kutoka kwa mama yake kama ilivyokuwa desturi, akiahidi kumrudisha siku ya Jumapili.
Hata hivyo, alishindwa kufanya hivyo na kuanza kumpotosha mama wa mtoto kwa madai kuwa mtoto alikuwa amesafiri na angerudi baadaye.
Juhudi za mama huyo kutaka kuwasiliana na mtu aliyedaiwa kusafiri na mtoto hazikufanikiwa, hali iliyozua mashaka zaidi. Baadaye, taarifa zilipatikana kuwa mtoto huyo alikuwa amefariki dunia.
Baada ya kukamatwa, mshtakiwa alikiri kuhusika na tukio hilo, akieleza kuwa alimkata mtoto vipand vipande kwa kutumia kisu, kisha akapondaponda baadhi ya mifupa kwa jiwe kabla ya kutupa mabaki hayo katika shimo la choo la nyumba aliyokuwa akiishi katika Kata ya Mkwawa.
Mahakama ilieleza kuwa Jeshi la Polisi lilipofika eneo hilo lilithibitisha utambulisho wa mshtakiwa kupitia mama mwenye nyumba aliyemtambua kama mpangaji wake.
Baada ya kupata kibali, polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Iringa (Iruwasa), walibomoa shimo la choo na kutoa vipande vya mwili vilivyowasilishwa mahakamani kama vielelezo namba A1 hadi A9.
Hata hivyo, Jaji Angaza alisema uchunguzi wa kitabibu uliibua mashaka kuhusu utambuzi wa mabaki hayo iwapo yalikuwa ya binadamu au la, hali iliyozua mjadala katika ushahidi uliowasilishwa.
Mahakama ilibainisha kuwa vielelezo vikuu vilivyowasilishwa vilikuwa ni maelezo ya onyo, ushahidi wa vinasaba (DNA) na ushahidi wa eneo la tukio.
“Hata hivyo, maelezo ya onyo na ushahidi wa DNA vilikuwa na mashaka, kwa hiyo mahakama ilitegemea zaidi ushahidi wa mazingira katika kufikia uamuzi wake,” alisema Jaji Angaza.
Kwa upande wa utetezi uliokuwa ukiongozwa na Wakili, Geofrey Mwakasege uliieleza Mahakama kuwa kesi hiyo ilikuwa na changamoto kubwa kutokana na uzito wake na kuwepo kwa ushahidi unaokinzana kutoka kwa mashahidi wa upande wa mashtaka.
Akizungumza baada ya hukumu, Wakili Mwakasege alisema haikuwa rahisi kupambana na hoja za upande wa Jamhuri, lakini alisisitiza kuwa walitumia mbinu zote za kisheria kumtetea mteja wao.
“Kwa sasa tumekubaliana na hukumu iliyotolewa kwa sababu bado sijapata nafasi ya kuzungumza kwa kina na mteja wangu ili tujadili hatua zinazofuata, ikiwemo ya uwezekano wa kukata rufaa,” alisema Wakili Mwakasege.
