Na Mwandishi Wetu, Lindi
Fursa ya biashara ya kaboni imeelezwa kuwa mkombozi mpya wa uchumi wa misitu nchini, huku Serikali ikihimiza wananchi na wadau kuchangamkia rasilimali hiyo kwa manufaa ya kiuchumi na uhifadhi wa mazingira.
Hayo yamebainishwa Machi 18, 2026 katika Uwanja wa Ilulu, Manispaa ya Lindi, wakati wa Jukwaa la Majadiliano ya Biashara kwa Biashara (B2B) lililoandaliwa kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na kampeni ya kitaifa ya upandaji miti.
Akiwasilisha mada kuhusu biashara ya kaboni, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Meneja wa Baiolojia ya Mbegu za Miti kutoka TFS, Fandey Mashimba, amesema biashara hiyo ni fursa kubwa ya kiuchumi unaowezesha nchi kama Tanzania kunufaika kwa kuhifadhi misitu au kupanda miti ambayo husaidia kufyonza gesi joto ya CO₂.
Amesema biashara ya kaboni ilianzishwa kimataifa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na ongezeko la gesi joto, huku nchi zilizoendelea zikitakiwa kulipia juhudi za nchi zinazoendelea katika kuhifadhi mazingira kwa kufyonza gesijoto ikiwemo CO₂ kupitia misitu na sekta nyingine.
“Misitu yetu ni hazina kwa sababu inafyonza gesijoto ambapo kutokana na hilo viwango vya kaboni (carbon credits) hupatikana na kuuzwa. Amefafanua, tani 1 ya CO₂ iliyo fyonzwa kwa mwaka na mimea au kiasi hichohicho cha gesi joto kilichozuiwa kusambaa hewani ndio huuzwa kama kiwango cha Kaboni kulingana na mradi na uthibitisho baada ya upimaji.
Tukisimamia vizuri na kuwa na takwimu sahihi, tunaweza kuuza kaboni ( ‘carbon credits’) na kupata mapato,” amesema Mashimba.
Amefafanua katika biashara hiyo hakuna ardhi, msitu, miti au rasilimali yeyote inayouzwa au wananchi kunyang’anywa ardhi (land grabbing) bali mwekezaji huwa ana haki na viwango vya kaboni tu vilivyo zalishwa wakati wa uwekezaji kinyume na taarifa potofu ambazo zimekuwa zikibeza biashara ya Kaboni.
Amesema, bidhaa ya kaboni ni sawa na bidhaa nyingine na pia zina masoko yake kwenye soko la kimataifa na kama nchi tayari kuna kanuni na muongozo chini ya sheria ya mazingira inayo simamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira.
Hata hivyo, amesema wananchi wengi bado wana hofu na uelewa mdogo kuhusu biashara hiyo, akisisitiza umuhimu wa elimu na uwekezaji katika tafiti na mifumo ya upimaji wa kaboni ili kuondoa hofu.
Akichangia mada hiyo, Mbunge wa Jimbo la Mchinga Mkoani Lindi na Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mhe Salma Kikwete, amesema kuna haja ya kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuelewa thamani ya misitu na kuepuka uharibifu unaotokana na matumizi ya nishati kama mkaa.
Katika wasilisho jingine ambalo limetambulisha miti mingine ambayo haijulikani lakini baada ya utafiti imeonekana kufaa katika matumizi ya mbao, amesema pamoja na ongezeko la thamani ya miti ya asili, wananchi wengi huuza mazao ya misitu kwa bei ndogo kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi za soko na thamani halisi ya rasilimali hizo na kuomba elimu itolewe ili wananchi wanufaike na misitu yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe Zainab Telack, ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha wananchi wengi kushiriki katika biashara ya kaboni.
Amesema mkoa huo una vijiji zaidi ya 70 vyenye misitu ya hifadhi vinavyoweza kunufaika na biashara hiyo endapo vitapewa elimu na miongozo sahihi.
Mhe Telack pia ameshauri vibali vya uvunaji wa misitu viambatane na masharti ya upandaji miti ili kuhakikisha uendelevu wa rasilimali hizo kama inavyo fanyika kwa watumiaji wa miti wanapo sindika tumbaku.
Jukwaa hilo limejadili mada nane muhimu ikiwemo biashara ya kaboni, matumizi ya teknolojia, sera na kanuni pamoja na namna ya kuongeza thamani ya mazao ya misitu.
Kesho Machi 19, 2026, uzinduzi rasmi wa maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Kampeni ya Upandaji Miti Kitaifa unatarajiwa kufanywa na Makamu wa Rais, Mhe Emmanuel Nchimbi, huku Serikali ikiendelea kusisitiza kaulimbiu ya mwaka huu: “Misitu ni Uchumi Endelevu, Tuihifadhi kwa Maendeleo ya Taifa.”







