Daktari aeleza kitaalamu chanzo majeraha ya mastaa Yanga

KAMA wodi ya wagonjwa sasa huko Jangwani inaelekea kujaa kufuatia idadi ya majeruhi kuongezeka ikiwa ni siku chache tangu kutangazwa kuwa nahodha msaidizi wa kikosi hicho, Dickson Job na Clement Mzize watakuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya wiki sita, huku mmoja wa madaktari bingwa akitaja sababu na suluhisho lake.

Madaktari wa klabu hiyo wamethibitisha ongezeko la majeruhi hadi kufikia sita huku katika orodha mpya ya sasa, akitajwa beki wa kati, Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ na mshambuliaji Laurindo Dilson ‘Depu’.  

Depu mwenye mabao sita na asisti moja katika ligi msimu huu, amepata jeraha la nyama za paja, Bacca (nyonga), Chadrack Boka (enka ya mguu wa kushoto) na Edmund John (bega), wote watakuwa nje ya uwanja angalau wiki mbili.

Nyota hao watakosekana katika mechi ya leo Jumatano ambapo Yanga itacheza ugenini dhidi ya TRA United, hivyo kocha wa kikosi hicho, Pedro Goncalves atakuwa na kazi ya kufanya kutokana na eneo la beki wa kati kuonekana kuathirikika zaidi tofauti na maeneo mengine.

Hadi sasa, wodi ya majeruhi ya Yanga ina mabeki wawili wa kati ambao mara nyingi wamekuwa wakicheza pamoja, Job na Bacca, hivyo Pedro atakuwa na Bakari Mwamnyeto kama chaguo la kwanza sambamba na Frank Assinki ambaye amekuwa akitumika kama mchezaji wa akiba zaidi.

Akizungumzia idadi kubwa ya majeruhi inayoikumba Yanga na suluhisho lake, Dk Robert Kamau ambaye aliwahi kufanya kazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na sasa makazi yake Hispania, alisema: “Kwanza kabisa, ni muhimu kuelewa kuwa mlipuko huu wa majeraha hautokei kwa bahati mbaya tu. Kuna sababu nyingi zinazochangia wachezaji kukumbwa na majeraha mara kwa mara.

“Sababu za ndani ni muhimu. Wachezaji wanapofanya mazoezi kupita kiasi au kushiriki mechi nyingi bila muda wa kutosha wa kupumzika, misuli na ‘tendon’ zinabeba mzigo mkubwa zaidi, jambo linalosababisha kuvunjika kwa nyuzi za misuli. Wengine wana historia ya majeraha ya zamani na pale wanapokumbana na mazoezi mengi au mechi mfululizo huwa kunakuwa na hatari kubwa sana.”

Jambo lingine, alisema lishe na unywaji wa maji pia ni sababu za ndani kutokana na misuli kuhitaji virutubisho vya kutosha na maji ili kufanya kazi kwa ufanisi. Ukosefu wa virutubisho unaweza kudhoofisha misuli na kufanya wachezaji kuwa katika hatari ya kuumia.

“Sababu za nje pia zipo tena nazo zina nafasi, moja ni hali ya uwanja, kama nyasi zina shida, udongo mgumu au kuna sehemu hakuna uwiano sawa, huongeza hatari ya kuumia paja, enka au nyonga.”

Daktari huyo alienda mbali kwa kumtolea mfano Bacca aliyepata jeraha la nyonga ambalo linaathiri moja kwa moja kasi yake huku Depu ambaye aina yake ya jerah, linatokana na uchovu wa misuli na kuendelea na mazoezi makali bila mapumziko ya kutosha.

“Kuna hatua kadhaa za kufanya ili kupunguza wimbi hili la majeraha. Kwanza, kupanga ratiba ya mazoezi yenye uwiano, ikijumuisha mapumziko ya kutosha na ‘recovery sessions’, jambo lingine ni kuhakikisha lishe bora na unywaji wa maji ya kutosha kwa wachezaji, mwisho najua Yanga ni klabu kubwa, hivyo waimarishe kitengo chao cha afya kwa kutumia mbinu za matibabu nzuri na bora zaidi na ufuatiliaji wa karibu kwa wachezaji waliopo kwenye hatari ya majeraha,” alisema Robert na kuongeza;

“Pia ni muhimu kufanya tathmini ya kina ya hali ya uwanja na kuhakikisha wachezaji wanajua mbinu za kuepuka majeraha wakati kwa kuchukua hatua hizi, klabu inaweza kupunguza hatari ya mlipuko wa majeraha na kuhakikisha wachezaji wanarejea kwenye kiwango cha juu bila hatari ya kukumbana tena na majeraha yaleyale ya mwanzo.”

Akizungumzia majeraha ndani ya kikosi chake, Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves alisema: “Hii ni changamoto mpya ambayo inatukabili hawa wote ni wachezaji muhimu lazima tuwe na hesabu mpya kuhakikisha mambo yanakuwa sawa licha ya kuwakosa hao wachezaji, kama unavyofahamu ni kama idadi imeongezeka kwa kuwa wpo wengine walikuwa na majeraha ya muda mrefu kama Mzize (Clement) na Job (Dickson).”

Pedro amechekelea kuanza kurejea kwa baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi akiwemo Pacome Zouzoua akisema itaongeza nguvu kwenye kikosi chake kutokana na ubora wa kiungo huyo

“Kwa sasa naona baadhi ya wachezaji wetu wanarudi, ni hatua nzuri kwani unapokuwa na mchezaji wako bora kama Pacome unazidi kuwa imara kwenye mechi zako akishirikiana na wenzake, bado tuna timu imara.”

Pacome aliingia kipindi cha pili dakika ya 60 kwenye mchezo dhidi ya Azam akichukua nafasi ya Mudathir Yahya baada ya kukosa mechi tano ambapo mara ya mwisho kuwa uwanjani ilikuwa Februari 15, 2026 wakati Yanga ikicheza mechi wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Kabylie ya Algeria.

Mbali na ishu za majeraha, Pedro amezungumzia ishu ya matokeo inayopata kikosi chake kinachoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara akisema suluhu dhidi ya Azam haijawaharibia hesabu zao za kutetea ubingwa wa ligi hiyo.

Pedro alisema bado ana imani kubwa na kikosi chake licha ya sare hizo mbili dhidi Azam na Simba na kwamba ligi bado ina mechi nyingi ambazo zinaweza kuwarudishia pointi nne ilizoziangusha ikikutana na klabu hizo kubwa mbili.

“Huwezi kusema hizi sare mbili dhidi ya Simba na Azam kwamba zimetuharibia kwenye mbio za ubingwa lakini ukweli ni kwamba klabu yenye hadhi ya Yanga inahitaji kushinda katika kila mchezo ulio mbele yetu na haya ndio malengo yetu wakati wote,” alisema Pedro.

“Kwetu tungeweza kupata ushindi lakini kuna maeneo hatukupata maamuzi sahihi na kupoteza nafasi zetu za kubadilisha matokeo, hatuwezi kuendelea kulia tutainuka kwenye mechi zinazofuata ili turudi kwenye njia ya ushindi.”