Bakari Mahundu
March 18, 2026
0 Comments
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Iringa imemhukumu kunyongwa hadi kufa Joseph Mhulilwa, dereva bajaji na mkazi wa Mtwivila B, Manispaa ya Iringa, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa makusudi mtoto wake wa kumzaa, Timothy Mhulilwa (4), akidaiwa kufanya tukio hilo kwa lengo la kujipatia utajiri.
Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Angaza Mwipopo katika kesi namba 25532 ya mwaka 2025, akibainisha kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi uliothibitisha pasipo shaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu.
Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, tukio hilo lilitokea Aprili 12, 2025 ambapo mshtakiwa alimuua mtoto wake kisha kuukatakata mwili vipande vidogo na kuvitupa kwenye shimo la choo.
Mahakama ilieleza kuwa mshtakiwa alikiri kufanya kitendo hicho ikiwemo kuponda mifupa mikubwa kwa jiwe ili kurahisisha utupaji wa mabaki hayo.
Ilielezwa pia kuwa baada ya kukamatwa kwake, mabaki ya mwili wa marehemu yalipatikana katika tenki la maji taka na kufanyiwa uchunguzi wa vinasaba (DNA), uliothibitisha kwa asilimia 99 kuwa yalikuwa ya mtoto huyo na yana uhusiano wa kibaolojia na mshtakiwa.
Katika kuthibitisha shtaka hilo, upande wa Jamhuri uliwasilisha jumla ya mashahidi 13, ambao ushahidi wao uliisaidia mahakama kufikia uamuzi wa kumtia hatiani mshtakiwa na kumhukumu adhabu ya kifo kwa kunyongwa.
Hata hivyo, wakili wa utetezi, Geoffrey Mwakasege, alipinga hukumu hiyo akidai kuwa mahakama haikuzingatia ipasavyo baadhi ya vielelezo muhimu, ikiwemo ramani ya eneo la tukio, ripoti ya uchunguzi wa DNA pamoja na maelezo ya onyo ya mshtakiwa.