Halmashauri za Mtwara zapewa neno upandaji miti

Mtwara. Halmashauri tisa za Mkoa wa Mtwara zimetakiwa kuongeza kasi ya upandaji miti ili kufikia malengo ya Serikali ya kupanda zaidi ya miti milioni 1.5 kwa kila halmashauri, kufuatia utekelezaji usioridhisha ulioonekana mwaka 2025.

Wito huo umetolewa baada ya mkoa huo kupanda miti milioni tano pekee mwaka jana, idadi inayotajwa kuwa ndogo kulinganisha na malengo yaliyowekwa kitaifa.

Akizungumza leo Jumatano Machi 18, 2026 wakati wa uzinduzi wa upandaji miti kwa mwaka 2026 uliofanyika katika Shule ya Sekondari Mkunwa, Wilaya ya Mtwara, Kaimu Mkuu wa Mkoa huo, Michael Mntenjele amesema ni lazima kuongeza juhudi ili kufikia malengo ya uhifadhi wa mazingira.

Amesema upandaji miti si suala la hiari bali ni wajibu wa kila mwananchi, akisisitiza kuwa mkoa unapaswa kuwa kinara katika uhifadhi wa mazingira nchini.

“Lengo letu ni kuona Mtwara inakuwa kinara wa uhifadhi wa mazingira. Kupanda miti zaidi ya milioni 13 siyo hiari tena, ni wajibu wa kila mmoja wetu,” amesema Mntenjele.

Amefafanua kuwa idadi ya miti iliyopandwa mwaka 2025 haikufikia hata nusu ya malengo yaliyokusudiwa, hivyo kuna haja ya kuongeza juhudi na ushirikiano kati ya Serikali, taasisi na wananchi.

Kwa mujibu wa Mntenjele, mkoa umejipangia kupanda miti zaidi ya milioni 13 kila mwaka, huku mwaka 2026 ukitarajiwa kupandwa miti zaidi ya milioni saba kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kuongeza uzalishaji wa matunda.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS) Kanda ya Kusini, Muhifadhi Mwandamizi, Hassan Sengerere amesema taasisi hiyo inaendelea kuzalisha miche ya miti ya misitu na matunda kwa wingi ili kusaidia juhudi hizo.

Amesema lengo ni kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa ya kushiriki katika upandaji miti, huku akibainisha kuwa miti ya matunda ina mchango mkubwa kiuchumi kwa wananchi pamoja na kulinda mazingira.

“Tunazalisha miche kwa wingi ili wananchi waweze kushiriki kikamilifu katika zoezi hili. Miti siyo tu inalinda mazingira bali pia inaleta manufaa ya kiuchumi,” amesema Sengerere.

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mkunwa wamepongeza jitihada hizo, wakisisitiza umuhimu wa kupewa miche zaidi ya miti ya matunda. Mkazi wa kijiji hicho, Shadya Abdallah, alisema miti hiyo ina faida nyingi ikiwemo kivuli, chakula na kipato.

Katika uzinduzi huo, jumla ya miti 500 ya aina mbalimbali ilipandwa, ikiwemo ya matunda kama mipera, mipapai, miembe na michungwa. Aidha, miche mingine 2,000 iligawiwa kwa wananchi kwa ajili ya kupandwa katika maeneo yao.