MJUMBE wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Swedi Mkwabi amesema suala la Jonathan Sowah bado lipo katika kamati ya nidhamu ya klabu hiyo, hivyo uamuzi wake utatolewa kila kitu kitakapokuwa sawa.
Mkwabi aliyasema hayo baada ya kuwepo kwa taarifa za Sowah kujibu tuhuma zinazomkabili zilizofanya uongozi wa klabu kumsimamisha tangu timu ilipokuwa ikijiandaa na mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji iliyochezwa Februari 25, 2026.
“Kama viongozi hatujajua hatma yake kwa kuwa suala lake lipo mbele ya kamati ya nidhamu, itakapomaliza procedure (utaratibu) zake, ndio uongozi wa klabu utajulishwa,” alisema Mkwabi.
Machi 5, 2026, zilitoka taarifa za Sowah kupewa siku tatu kutoa maelezo kwa kujibu yale anayotuhumiwa nayo ikiwamo maelezo kuhusu kuchelewa kwenye mikutano kadhaa ya timu, kukataa kufanya mazoezi ya ziada, kuchelewa mazoezini, kusafiri kwenda Angola kucheza dhidi ya Petro Atletico akiwa amevaa jezi ya SL Benfica badala ya mavazi rasmi ya klabu na kufanya faulo za makusudi zinazoweza kusababisha kadi nyekundu, ikiwemo kwenye mechi dhidi ya Azam FC na Espérance.
Taarifa kutoka kwa mtu wa karibu na Sowah zinasema amejibu kila kitu alichotakiwa. “Yapo mengi ila kuhusu kadi alizopewa kama alikuwa anatumika amekanusha na ameumizwa na matokeo mabaya wakati alikuwa hatumiki na hapewi muda wa kutosha kwani mara nyingi amekuwa akiingizwa wakati timu ipo kwenye presha kubwa ya matokeo na muda mchache.
“Ila kitu ambacho analalamika ni kutopewa nafasi ya kufanya mazoezi na bado ana nia ya kutaka kuendelea kutumikia mkataba wake Simba. Kwa sasa anajifua peke yake ‘gym’ kwenye hoteli moja kubwa hapa hapa jijini Dar es Salaam, ni matumaini yetu baada ya muda kila kitu kitarejea kama kilivyokuwa awali,” kilisema chanzo hicho.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Sowah katika yale aliyotakiwa kujibu ameyatolea ufafanuzi kwamba hayana ukweli, hivyo anasubira uamuzi wa Kamati ya Nidhamu ambayo muda wowote itatoa majibu ya hilo sakata.
Ikumbukwe kuwa Sowah aliyetua Simba kipindi cha usajili wa dirisha kubwa msimu huu akitokea Singida Black Stars, alitoka kutumikia adhabu ya kusimamishwa mechi tano na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu aliyofanya dhidi ya Azam FC, katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Desemba 7, 2025. Alifungiwa sambamba na Alassane Kante ambaye kwa sasa anaendelea na majukumu baada ya adhabu hiyo kumalizika, huku Sowah akikumbana na ishu nyingine ndani ya klabu.
Mshambuliaji huyo raia wa Ghana, Simba ilimsajili baada ya kuuwasha Singida Black Stars msimu uliopita akicheza miezi sita akifunga mabao 13 katika mechi 14.
Akiwa Simba, msimu huu Sowah amecheza mechi 11 kwa dakika 477. Mechi hizo ni Ligi Kuu Bara (4), Ligi ya Mabingwa Afrika (6) na Kombe la Mapinduzi (1) ambapo Sowah amefanikiwa kufunga mabao matatu yote kwenye Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate, JKT Tanzania na Mbeya City.
1. Kugomea mazoezi, Sowah amekanusha kukataa mazoezi (Februari 17 dhidi ya Greenland).
Alisema alishiriki kikamilifu licha ya kuwa amesimamishwa na hivyo kutoruhusiwa kucheza au kufanya mazoezi uwanjani. Baada ya kumaliza mazoezi hayo, kocha wa viungo alimruhusu kuondoka.
2.Mazoezi ya ziada (Februari 22)
Alieleza kuwa mkanganyiko ulitokana na changamoto za kiutendaji, basi la timu kuchelewa na kukosekana kwa vifaa vyake vya mazoezi. Alisema mazoezi yalifanyika baadaye hotelini pamoja na wachezaji wenzake chini ya usimamizi wa kocha wa viungo. Aliongeza kuwa kuna ushahidi wa video.
3.Kuchelewa mazoezini (Februari 16)
Alikiri kuchelewa kwa takribani dakika tano baada ya kusinzia bila kukusudia kufuatia kikao cha uchambuzi wa video. Alisema alimjulisha kocha mara moja na kuchelewa huko hakukuwa kwa makusudi.
Alikataa vikali madai kwamba amewahi kuchelewa kwenye vikao vya timu.
5.Kuvaa jezi isiyo rasmi (safari ya Angola)
Alikataa kuvaa jezi ya SL Benfica, akisisitiza kuwa alivaa jezi rasmi ya Simba. Alisema hilo linaweza kuthibitishwa kupitia picha zilizochapishwa kwenye mitandao rasmi ya klabu.
6.Tuhuma za kufanya faulo zisizo za kawaida.
Alisema faulo zake zilikuwa sehemu ya ushindani wa kawaida uwanjani, si jaribio la makusudi kumdhuru mpinzani au kutafuta kadi nyekundu.