Israel yadai kumuua waziri wa ujasusi wa Iran, mvutano wazidi kupamba moto

Dar es Salaam. Mvutano wa kijeshi kati ya Israel na Iran umeingia hatua mpya kufuatia madai ya Israel kuwa imemuua Waziri wa Ujasusi wa Iran, Esmail Khatib, katika mashambulizi ya anga yaliyofanyika usiku wa kuamkia jana Jumanne.

Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, aliyesema operesheni hiyo pia ilimuua kiongozi wa juu wa usalama wa Iran, Ali Larijani.

Mamlaka za Iran zimethibitisha kifo cha Khatib na kueleza kuwa maziko yake yamefanyika leo.

Katz amesema mashambulizi hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuwadhibiti viongozi wa vyombo vya usalama vya Iran, akisisitiza kuwa operesheni hiyo ilipangwa kwa umakini mkubwa.

Katika hatua hiyo, Israel pia imedai kumuua kamanda wa vikosi vya Basij, Gholamreza Soleimani, jambo linaloonesha ukubwa wa operesheni hiyo dhidi ya miundombinu ya kiusalama ya Iran.

Aidha, Katz amesema yeye pamoja na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wameagiza Jeshi la Ulinzi la Israel kuendelea kuwasaka viongozi wa Iran wanaodaiwa kuhusika na kile walichokiita “utawala wa ugaidi na ukandamizaji.”

Hata hivyo, sambamba na mashambulizi hayo, kumekuwepo na sintofahamu iliyosambaa kwa kasi mitandaoni kuhusu madai ya kifo cha Netanyahu. Taarifa hizo zimeenea haraka kabla ya kiongozi huyo kuonekana hadharani akiendelea na majukumu yake, hatua iliyotafsiriwa kama kukanusha uvumi huo.

Tukio hilo limeibua mjadala kuhusu ongezeko la vita ya taarifa, ambapo propaganda na taarifa zisizothibitishwa zinachangia kuongeza taharuki miongoni mwa wananchi.

Kwa upande wa Iran, Mkuu wa jeshi la nchi hiyo, Amir Hatami, ameonya kuwa Iran itachukua hatua za kulipiza kisasi kwa kile alichokiita shambulio la kikatili.

Amesema kwa wakati na mahali muafaka, Iran itatoa jibu la uamuzi na la kuzuia dhidi ya Marekani na Israel, akisisitiza kuwa vifo vya viongozi wake havitapita bila hatua stahiki kuchukuliwa.

Wakati huohuo, Walinzi wa Mapinduzi wa Iran (IRGC) wamedai kurusha makombora kuelekea maeneo ya kati ya Israel kama sehemu ya kulipiza kisasi, hatua inayoongeza hatari ya mzozo huo kugeuka kuwa vita ya wazi.

Nje ya mipaka yake, Israel imeripotiwa kuendeleza mashambulizi katika mji wa Beirut, Lebanon, ikidai kulenga taasisi ya kifedha inayohusishwa na kundi la Hezbollah.

Taarifa kutoka eneo hilo zinaeleza kuwa watu wasiopungua 10 wamefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa, huku mamlaka za Lebanon zikieleza wasiwasi kuhusu kulengwa kwa maeneo ya kiraia.

Wakati hali hiyo ikiendelea Mashariki ya Kati, mgawanyiko umeibuka ndani ya Marekani kuhusu mwelekeo wa vita dhidi ya Iran.

Ofisa wa kupambana na ugaidi, Joe Kent, amejiuzulu akipinga operesheni ya kijeshi na kuitaka serikali ya Donald Trump kubadili mkakati.

Katika barua yake, Kent amesema Iran haikuwa tishio la haraka kwa Marekani, akionya kuwa vita hiyo inaweza kusababisha madhara makubwa bila manufaa ya moja kwa moja kwa Wamarekani.

Hata hivyo, Ikulu ya Marekani imepuuza hoja hizo, huku Trump akimtaja Kent kama mtu mzuri lakini dhaifu katika masuala ya usalama, akisisitiza kuwa uamuzi wa kuhusika katika operesheni hiyo ulikuwa sahihi.