JKT Tanzania yakomaa na mambo manne

KATIKA kipindi hiki kirefu ambacho JKT Tanzania haina mechi ya mashindano, kocha mkuu wa kikosi hicho, Ahmad Ally ameweka wazi mpango wao kuhakikisha hawatoki kwenye mstari.

Katika mpango huo, kocha huyo ametaja mambo manne anayokomaa nayo kuwa ni uimara wa mwili, ubora wa kiufundi, mbinu na mifumo ya uchezaji, pamoja na utayari wa kisaikolojia.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ally alisema licha ya kuwepo kwa mapumziko hayo marefu, lakini bado wataendelea kuwa makini ili kuhakikisha hawapotezi mwelekeo wa timu kuelekea malengo waliyojiwekea msimu huu.

Alisema kikosi hicho kitapumzika wiki moja tu ila baada ya mapumziko ya sikukuu wachezaji wataendelea na ratiba ya mazoezi kama kawaida.

“Mapumziko yapo ndiyo, ila tutapumzika kwa wiki moja tu na tutaanza maandalizi baada ya sikukuu ili kuendelea kujinoa zaidi.

“Tayari tumeweka ratiba maalum ya kurejea kambini na kuanza maandalizi rasmi kwa ajili ya mechi zijazo ambazo zinatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

“Tutaendelea kuijenga timu katika misingi uhimu ya mchezo ikiwemo uimara wa mwili, ubora wa kiufundi, mbinu na mifumo ya uchezaji pamoja na utayari wa kisaikolojia ili tuwe imara katika kila idara hizo.

“Tunajua ligi ikirudi itakuwa ngumu sana, hivyo tuna kazi kubwa ya kufanya, zaidi ya yale ambayo tumefanya,” alisema.

JKT Tanzania inayoshika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi tangu ilipocheza na Yanga na kuchapwa mabao 5-0, Februari 25, 2026, haijacheza mechi yoyote ya Ligi Kuu hadi Aprili 4, 2026, itakapokuwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi, kucheza dhidi ya Namungo.