Manula arejea Stars Gamondi akiita 25

KOCHA wa Taifa Stars, Miguel Gamondi ametangaza kikosi cha wachezaji 25 akiwemo kipa Aishi Manula wa Azam kujiandaa na michezo miwili ya FIFA Series 2026 ambayo itachezwa Kigali nchini Rwanda.

FIFA Series ambayo imekuwa ikifanyika katika kipindi cha kalenda ya FIFA, Machi 26, 2026 Taifa Stars itacheza dhidi ya Liechtenstein kwenye Uwanja wa Kigali Pelé uliopo Kigali nchini Rwanda.

Mshindi wa mechi hiyo, atacheza fainali Machi 29, 2026 na mshindi kati ya Aruba na Macau, huku atakayepoteza pia atacheza kusaka nafasi ya tatu na moja kati ya timu hizo.

Baada ya kuwa nje ya kikosi hicho kwa miaka miwili, hatimaye Manula amerejea Stars huku akiitwa sambamba na kipa mwenzake wa Azam, Zuberi Foba na Yona Amosi wa Pamba Jiji.

Manula ambaye anatajwa kama ‘Tanzania one’ amekuwa nje ya Stars tangu 2023 wakati huo akiwa mchezaji wa Simba.

Mbali na Manula pamoja na Foba, wachezaji wengine kutoka Azam ambao wameitwa kwenye kikosi hicho ni Twalib Nuru, Elias Lameck, Feisal Salum na Idd Suleiman ‘Nado’.

Kwa upande wa Simba, waliotwa ni Nickson Kibabage, Yusuph Ngoma na Suleiman Mwalimu, huku Yanga wakiitwa Bakari Mwamnyeto, Mohamed Hussein, Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ na Mudathir Yahya. Pamba Jiji ni Yona na Kelvin Nashon. Wengine ni Mohamed Mussa (Mashujaa FC), Bakari Msimu (Coastal Union) na Paul Peter (JKT Tanzania).

Kikosi hicho kimejumuisha wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya mipaka ya Tanzania ambao ni Haji Mnoga (Salford City, Uingereza) na Novatus Dismas (Goztepe FC, Uturuki).

Wengine ni Alphonce Mabula (Shamakhi, Azerbaijan), Simon Msuva (Al-Talaba, Iraq), Kelvin John (Aalborg BK, Denmark), Tarryn Allarakhia (Rochdale AFC, Uingereza) na Charles M’Mombwa (Floriana FC, Malta).

Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ambaye anacheza soka la kulipwa Ufaransa akiwa na Le Havre, anatajwa kuomba kupumzika katika kipindi hiki cha kalenda ya FIFA huku akitamani kuona damu changa zikipata nafasi zaidi.

Wiki chache zilizopita kule Morocco wakati wa Afcon, Samatta alisema wazi kuwa hajioni akiwa na nguvu kubwa ya kutumika katika fainali zijazo za mataifa ya Afrika ambazo zitafanyika kwa mara ya kwanza ukanda wa Afrika Mashariki japo anaweza kuwa tayari kusaidia kutokana na uzoefu wake.

Na kwa sasa Gamondi anaonekana kutaka kuendeleza pale ambapo aliishia katika fainali za Morocco ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya 2027.